Dar es Salaam. Wakati Chama cha Demokrasia na Maendeleo (Chadema) kikilaani wimbi la ukamataji, utekaji na vitisho vinavyoendelea dhidi ya viongozi na wanachama wake katika Kanda ya Victoria, hususani mkoani Kagera, Jeshi la Polisi limesema baadhi yao walikamatwa kwa mujibu wa taratibu za kisheria kwa tuhuma za kihalifu.
Taarifa ya Msemaji wa Jeshi la Polisi nchini, David Misime iliyotolewa leo Oktoba 17, 2025 imesema miongoni mwa watu sita waliotajwa katika taarifa ya Chadema, walikamatwa kwa mujibu wa taratibu za kisheria kutokana na ushahidi uliokuwa umekusanywa kuhusu tuhuma mbalimbali za kihalifu.
Baadhi ya tuhuma hizo amesema ni za matumizi mabaya ya mitandao kwa kufanya uchochezi, kuhamasisha maandamano ambayo ni kinyume cha sheria na uvunjifu mwingine wa sheria za nchi.
Kwa mujibu wa taarifa ya Chadema ya Oktoba 16, 2025, viongozi na wanachama zaidi ya saba wamekamatwa na vyombo vya dola mkoani Kagera katika mazingira yenye utata, tena bila maelezo yoyote kutoka kwenye vyombo vya ulinzi na usalama wa raia.
Mkurugenzi wa Mawasiliano na Uenezi wa Chadema, Brenda Rupia alisema katika taarifa hiyo, kuwa matukio hayo yanajiri wakati ambao Samia Suluhu Hassan, mgombea urais wa CCM akiendelea na kampeni kwenye kanda hiyo inayojumuisha mikoa ya Mwanza, Geita, Mara na Kagera.
Chadema iliwataja miongoni mwa waliokamatwa kuwa ni Chief Adronicus Kalumuna (mwenyekiti wa Chadema Jimbo la Bukoba Mjini na Mjumbe wa Kamati ya Utendaji Kanda ya Victoria).
Wengine ni Paulo Musisi (mjumbe wa Mkutano Mkuu wa Taifa), Daniel Lwebugisa (katibu wa Chadema Mkoa wa Kagera), Egbert Kikulega, Ramadhan Fadhiri na Levocatus Willison (wanachama wa Chadema) na Baziri Waziri (Katibu wa Jimbo la Kyerwa).
“Pamoja na matukio haya kutokea kwenye mikoa ya kanda hii ya Victoria, tulitegemea Samia kwenye kampeni zake angekemea, lakini tunasikitika hakufanya hivyo na haoneshi dalili zozote za kukemea matendo haya yanayokiuka haki za binadamu,” ilieleza taarifa hiyo.
Vilevile ilieleza Khalid Swarehe (makamu Mwenyekiti wa Chadema Kanda ya Victoria), bado anashikiliwa gerezani baada ya kupewa kesi ya wizi wa kutumia silaha, tofauti na kosa walilomtuhumu mara ya kwanza alipokamatwa.
“Tunatoa wito kwa Watanzania wote, wadau wa demokrasia, mashirika ya haki za binadamu na jumuiya za kimataifa kuendelea kukemea matendo haya yanayoendelea kushamiri nchini Tanzania,” ilieleza taarifa ya Chadema.
Jeshi la Polisi katika taarifa yake limesema linapenda kutoa ufafanuzi juu ya mambo mawili yanayosambazwa kupitia vyombo vya habari, likiwamo la majina ya watu saba, ambao inaelezwa walikamatwa katika mazingira ya kutatanisha na kwamba ni ukandamizaji.
“Ni kwamba, miongoni mwa watu sita waliotajwa katika taarifa hiyo, walikamatwa kwa mujibu wa taratibu za kisheria kutokana na ushahidi uliokuwa umekusanywa kabla ya kukamatwa kuhusiana na tuhuma mbalimbali za kihalifu, zikiwepo za matumizi mabaya ya mitandao kwa kufanya uchochezi, kuhamasisha maandamano ambayo ni kinyume cha sheria na uvunjifu mwingine wa sheria za nchi,” imeeleza taarifa ya Misime.
Jeshi hilo limesema wakati wa ukamataji watu walishuhudia na baadhi ya viongozi wao walifika katika ofisi za makamanda wa polisi wa mikoa na vituo vya polisi kuwaulizia, ikiwa ni sambamba na kupiga simu na walijulishwa walikamatwa watu sita na kushikiliwa na walielezwa tuhuma zao.
Misime amewataja watuhumiwa ambao walijulishwa kushikiliwa kuwa ni Chief Adronius Kalumuna, Paulo Musisi, Daniel Lwebugisa, Egbert Kikulega, Ramadhan Fadhiri na Baziri Waziri.
Wakati huohuo, Jeshi la Polisi limetoa ufafanuzi kuhusu taarifa ya Godbless Lema, aliyoandika na kusambaza kupitia mitandao ya kijamii kuwa, usalama wa maisha yake upo hatarini.
“Ufafanuzi ni kwamba, Jeshi la Polisi linaendelea kufuatilia kwa karibu na tunamsisitiza (Lema) afike katika kituo cha polisi ili awasilishe taarifa yake hiyo rasmi kwa hatua zingine, kwani ndiyo utaratibu wa kisheria,” imeeleza taarifa ya polisi.
Jeshi la Polisi limesema linaendelea kutoa wito na kusisitiza kwa baadhi ya viongozi na wananchi waendelee kuzingatia utaratibu wa kisheria wa kuwasilisha taarifa sahihi kwa jamii na mamlaka za haki jinai, ili kuepusha upotoshaji na taharuki zisizo za lazima.
Ufafanuzi huo wa Polisi, umekuja kutokana na madai ya Lema kupitia mitandao ya kijamii ya Instagram na X:
“Mheshimiwa Rais, maisha yangu yako katika hatari kubwa. Tafadhali, naomba kwa unyenyekevu mkubwa unisikilize. Ningependa kuishi ili niweze kuwaona watoto wangu wakikua, kuoa na kuolewa mbele ya macho yangu, na ikiwezekana, niweze kufurahia wajukuu wangu ikiwa Mungu atanijalia maisha marefu.”
Ameongeza kuwa kila mtu anatamani kuishi maisha marefu yenye amani na uzee mwema, akieleza kwa sasa kuna watu ambao wanamfuatilia kwa karibu sana.
“Hata jioni ya leo (Oktoba 16), wameonekana maeneo ya nyumbani kwangu, na nina hofu kwamba wangeweza hata kumdhuru mtu yeyote ambaye si mimi. Kwa hali hii, naona ni bora nijiweke mikononi mwa mamlaka kwa hiari yangu, kuliko kuendelea kuishi kwa hofu kila siku,” amendika na kuongeza:
“Niko tayari kuwekwa mahabusu kwa hiari yangu hadi kipindi cha uchaguzi kipite, kwa sababu naamini kufanya hivyo kutaleta utulivu kwa wazazi wangu, mke wangu Neema, na watoto wangu. Najua watahisi angalau faraja kwamba niko salama.”
Baadaye alindika: “Nimefika kituo cha Polisi Central, kujua kama ni wao wana shida na mimi.”