Profesa Mkenda aahidi kuboresha huduma za afya Rombo

Rombo. Mgombea ubunge wa Jimbo la Rombo kupitia Chama Cha Mapinduzi (CCM), Profesa Adolf Mkenda amesema endapo atachaguliwa kuwa Mbunge wa Jimbo hilo atahakikisha anaboresha Zahanati ya Kidale iliyopo Kata ya Katangara Mrere, ili ipandishwe hadhi na kuwa kituo cha afya cha mfano katika jimbo hilo.

Akizungumza leo, Oktoba 17, 2025, katika mkutano wa kampeni uliofanyika katika ofisi za Kijiji cha Katangara, Profesa Mkenda amesema mpango huo unalenga kuboresha huduma za afya kwa wananchi wa maeneo ya Mashati na vijiji jirani, ili waweze kupata huduma za matibabu karibu na kuondokana na adha ya kutembea umbali mrefu.

“Kidale ni zahanati ya zamani sana, yenye zaidi ya miaka 100, nataka niwahakikishie wananchi wa Mashati kwamba tutajenga zahanati hii iwe kituo cha afya cha mfano, ili wananchi waweze kupata huduma bora kwa urahisi,” amesema Profesa Mkenda.

Amesema kuwa serikali ya awamu ya sita chini ya Rais Samia Suluhu Hassan imefanya maboresho makubwa katika sekta ya afya jimboni humo , ikiwa ni sehemu ya juhudi za kuhakikisha kila tarafa inakuwa na kituo cha afya.

“Wakati Mheshimiwa Mramba anaondoka madarakani, Jimbo la Rombo lilikuwa na vituo vya afya vinne pekee, huku tarafa zikiwa tano, kwa sasa, kutokana na uwekezaji uliofanywa na Rais Samia, tuna vituo vya afya Saba vinavyofanya kazi, na lengo letu ni kuhakikisha Kidale kinakuwa kituo cha afya cha mfano,” amesema Profesa Mkenda.

Kwa upande wake, Diwani wa Kata ya Katangara Mrere, Venance Mallel, amesema endapo atachaguliwa ataweka kipaumbele katika kuboresha miundombinu ya barabara ndani ya kata hiyo.

“Barabara ya Mangi Temba bado haijakamilika, vivyo hivyo barabara ya Shauritanga kutoka barabara kuu ya lami kwenda kwa wananchi, tupo kwenye mazungumzo na Tarura na mipango ipo kuzikamilisha barabara hizo, naomba wananchi waendelee kuwa na imani, tutafanya makubwa,” amesema Mallel.

Aidha, aliwaomba wananchi kumpa ushirikiano ili kwa pamoja waweze kusukuma mbele maendeleo ya kata hiyo kwa kushirikiana na mbunge atakayechaguliwa.

“Profesa Mkenda amefanya mambo makubwa katika Jimbo la Rombo, naomba siku ya Jumatano mkatupe kura za kishindo kwa maendeleo ya Kidale na kata yetu kwa ujumla,” amesema Mallel.