SERIKALI imetangaza ongezeko la wastani wa asilimia 33.4 katika Kima cha Chini cha Mshahara kwa sekta binafsi, kutoka Shilingi 275,060/= hadi 358,322/=, hatua inayolenga kuboresha ustawi wa wafanyakazi na kuongeza tija katika uzalishaji.
Kima hicho kipya kitaanza kutumika rasmi kuanzia Januari 1, 2026, baada ya kukamilika kwa mchakato wa tathmini na ushauri uliofanywa na Bodi ya Kima cha Chini cha Mshahara, chini ya usimamizi wa Ofisi ya Waziri Mkuu.
“Serikali imeamua kuongeza kima cha chini cha mshahara kwa sekta binafsi ili kuhakikisha wafanyakazi wanapata ujira unaokidhi mahitaji yao ya msingi na unaoakisi ukuaji wa uchumi wa nchi,” alisema Mhe. Ridhiwani.
Kwa mujibu wa Waziri huyo, idadi ya sekta zilizoorodheshwa katika amri mpya imeongezeka kutoka 13 mwaka 2022 hadi 16 mwaka 2025, huku sekta ndogo zikiongezeka kutoka 25 hadi 46.
“Tumezingatia vigezo vya Shirika la Kazi Duniani (ILO) pamoja na vigezo vya kitaifa vinavyojumuisha uwezo wa waajiri kulipa, mfumuko wa bei, tija katika biashara, na malengo ya taifa ya kukuza uchumi na ajira zenye staha,” alisisitiza.
Sekta zitakazonufaika na kima kipya ni pamoja na kilimo, afya, mawasiliano, usafirishaji, hoteli, madini, biashara na viwanda, shule binafsi, ulinzi binafsi, nishati, uvuvi, huduma za baharini, michezo na utamaduni, miongoni mwa nyingine.
Aidha, Waziri aliwataka waajiri wote wa sekta binafsi kuzingatia na kutekeleza amri hiyo kwa mujibu wa sheria, akisisitiza kuwa Serikali haitasita kuchukua hatua dhidi ya watakaokaidi.
“Ofisi yangu itaendelea kufuatilia, kutoa elimu na kufanya tathmini ya utekelezaji mara kwa mara kuhakikisha kima hiki kinazingatiwa ipasavyo,” alisema Mhe. Ridhiwani.
“Lengo letu si tu kuongeza mishahara, bali kuboresha maisha ya wafanyakazi na kuongeza ufanisi kazini. Tunataka kuona sekta binafsi inakuwa mshirika wa kweli wa maendeleo ya taifa,” aliongeza.