Shule ya Sekondari Simbani, Kibaha Mjini ,mkoani Pwani inakabiliwa na changamoto ya ukosefu wa uzio hali inayohatarisha usalama wa mali za shule na wanafunzi na kusababisha utoro kwa baadhi ya wanafunzi.
Changamoto nyingine ukosefu wa hosteli hali inayosababisha matumizi ya madarasa kama vyumba vya kulala na upungufu wa vitanda.
Akizungumza wakati wa mahafali ya 16 ya shule hiyo, Mwalimu Mkuu wa Shule ya Sekondari Simbani, Zamda Komba, alisema ujenzi wa uzio utasaidia kuimarisha usalama na kudhibiti utoro.
Hata hivyo Zamda alieleza kuwa shule hiyo imepiga hatua kubwa za maendeleo, ikiwa ni pamoja na ongezeko la ufaulu kila mwaka, kutokana na mikakati madhubuti kama vile uwepo wa vipindi vya ziada, mazoezi ya kila wiki, mitihani ya mara kwa mara na upatikanaji wa vitabu na madarasa ya kutosha.
Zamda alisema shule hiyo ilianzishwa mwaka 2007 ikiwa na wanafunzi 134 na walimu watatu pekee, hadi kufikia mwaka 2025, shule ina jumla ya wanafunzi 963 na walimu 58, wakiwemo walimu wanawake 85.
Aliongeza kuwa wamejipanga kuondoa daraja la sifuri katika matokeo ya mtihani wa taifa wa kidato cha nne.
Rahma Mdegela na Khalid Mkawa, wakisoma taarifa ya wanafunzi wa kidato cha nne walitaja changamoto nyingine ni uchakavu wa miundombinu, kama mbao za madarasa, kuta na sakafu ambazo hazijafunikwa kwa marumaru, na vyoo vya walimu .
Walisema pia kutokuwepo kwa jiko sanjali na huduma ya chakula shuleni kumesababisha baadhi ya wanafunzi kuwa watoro na kushuka kwa taaluma .
“Tulipoingia kidato cha kwanza tulikuwa wanafunzi 249; wasichana 129 na wavulana 120, sasa tunahitimu 230 wasichana wakiwa 118 na wavulana 112”
Rahma alibainisha, kupungua kwa idadi hii kumesababishwa na utoro, kutofaulu mtihani wa upimaji wa kidato cha pili, pamoja na baadhi ya wanafunzi kuhamia shule nyingine,” alisema Rahma.
Aliishukuru serikali pamoja na Manispaa ya Kibaha Mjini kwa kuboresha mazingira ya ujifunzaji na ufundishaji, hatua ambayo imechangia ongezeko la ufaulu na kuinua kiwango cha taaluma shuleni hapo.
Mgeni rasmi Wakili Magdalena Mlolere, mwakilishi wa Mkurugenzi wa shirika la HAKIELIMU alieleza ,shirika hilo lisilo la kiserikali lina lengo la kuhakikisha kila mtoto anapata elimu bora na sawa.
Aliipongeza shule hiyo kwa kutambua umuhimu wa mazingira salama shuleni, na kusisitiza HAKIELIMU inaunga mkono juhudi za serikali katika kuwalinda wanafunzi dhidi ya ukatili .
“Tutatafuta njia ya kushirikiana na shule hii kutatua changamoto za uzio na hosteli kupitia miradi yetu mbalimbali,” alifafanua.
Magdalena aliwataka wanafunzi wanaohitimu kudumisha nidhamu, kujiepusha na matumizi mabaya ya mitandao ya kijamii, na kuendeleza bidii katika masomo yao.