Morogoro. Chuo Kikuu cha Sokoine cha Kilimo (SUA) kimewalipa wananchi fidia yenye thamani ya zaidi ya Sh1.6 bilioni kufidia ardhi, mali na posho mbalimbali, ikiwa ni pamoja na kifuta machozi kwa makaburi 18 yaliyokuwepo katika eneo lililotwaliwa kwa ajili ya upanuzi wa chuo.
Makamu Mkuu wa Chuo hicho, Profesa Raphael Chibunda, alisema fedha hizo zimelipwa kwa wananchi 197 waliopisha upanuzi wa chuo katika eneo la Kibaoni, Wilaya ya Mlele, Mkoa wa Katavi, lenye ukubwa wa ekari 689.02.
Profesa Chibunda alitoa taarifa hiyo jana wakati wa mahafali ya 46 ya SUA, ambapo alisema hatua hiyo ni sehemu ya utekelezaji wa mipango ya chuo ya kupanua miundombinu na kuongeza uwezo wa kutoa elimu, kufanya tafiti na kutoa huduma kwa jamii.
“Fedha hizi zimehusisha fidia za mali, ardhi, pamoja na posho mbalimbali zikiwemo kifuta machozi kwa makaburi 18 ya wananchi 12,” alisema Profesa Chibunda.
Aliongeza kuwa SUA inaendelea kuonesha mafanikio makubwa katika nyanja ya utafiti na ubunifu, ambapo hadi sasa chuo hicho kinatekeleza jumla ya miradi 143 ya utafiti katika maeneo mbalimbali nchini, ikilenga kutatua changamoto za kijamii na kiuchumi.
“Nataka kuwataarifu kuwa panya buku aitwaye Ronin kutoka SUA aliweka rekodi ya dunia ya Guinness kwa kugundua mabomu 109 ya ardhini nchini Cambodia, akionesha wazi mchango wa SUA katika kuokoa maisha ya watu duniani,” amesema Profesa Chibunda, akipigiwa makofi na wahitimu.
Akiendelea kufafanua, Profesa Chibunda alisema SUA inaendelea na utekelezaji wa Mradi wa Higher Education for Economic Transformation (HEET), unaohusisha ujenzi na ukarabati wa majengo mbalimbali yenye thamani ya Sh58.5 bilioni.
Alisema wakandarasi na washauri elekezi wanaendelea na kazi hiyo katika kampasi za Edward Moringe, Solomon Mahlangu na Mizengo Pinda iliyopo mkoani Katavi, kwa lengo la kuboresha mazingira ya kujifunzia na kufundishia.
Katika mahafali hayo, jumla ya wahitimu 3,560 walitunukiwa vyeti, stashahada, shahada za kwanza, umahiri na uzamivu. Kati yao, wanaume 2,029 na wanawake 1,531, sawa na asilimia 42.95 ya wahitimu wote.
Idadi ya wahitimu wa shahada za kwanza ni 3,274 (wanaume 1,861 na wanawake 1,413); Shahada za Umahiri ni 127 (wanaume 76 na wanawake 51); na wahitimu wa Shahada ya Uzamivu (PhD) ni 18 (wanaume 12 na wanawake 6).
Vilevile, kulikuwa na wahitimu wa stashahada 100 na astashahada 38 waliomaliza masomo yao katika programu mbalimbali 85 zinazotolewa na chuo hicho.
Kwa upande wake, Mwenyekiti wa Baraza la Chuo, Andrew Massawe, alisema baraza limeendelea kutekeleza majukumu yake kwa weledi, uadilifu na uzalendo, likilenga kuhakikisha Sua inabaki kuwa taasisi mahiri ya elimu ya juu, utafiti na huduma kwa jamii.
“Baraza linaendelea kusimamia mikakati ya kuimarisha vyanzo mbadala vya mapato kupitia miradi ya kibiashara, ushauri wa kitaalamu na uwekezaji katika maeneo ya kimkakati,” amesema Massawe.
Ameongeza kuwa baraza linaendelea kuhimiza matumizi ya matokeo ya tafiti zinazofanyika chuoni kuchangia sera na mipango ya maendeleo ya taifa.
“Katika kipindi hiki, miradi 36 mipya ya utafiti imeanzishwa, ikiwemo miradi 10 inayofadhiliwa na wahisani wa nje, miwili na Serikali kupitia COSTECH, na 24 kupitia mapato ya ndani ya chuo,” amesema Massawe, akibainisha kuwa tafiti hizo zimechangia katika sekta za kilimo, mifugo, mazingira na maendeleo ya jamii.
Katika hatua nyingine, Mshauri Mkuu wa Masuala ya Usalama wa Sua, Kamishna Msaidizi wa Polisi Simon Haule amewataka wahitimu kuepuka kujihusisha na uvunjifu wa amani, hasa wakati huu ambao nchi inajiandaa kuelekea uchaguzi.
“Tumia mitandao ya kijamii kwa manufaa ya kitaaluma na maendeleo ya jamii. Msitumiwe kuchafua watu au taasisi,” alisema Kamishna Haule, akihimiza uadilifu na uzalendo miongoni mwa vijana hao.