Serikali ya Tanzania kwa kushirikiana na Shirika la Maendeleo la Umoja wa Mataifa (UNDP) na Umoja wa Ulaya (EU) imezindua maabara maalum zenye thamani ya Shilingi Bilioni 5 kwa ajili ya kuongeza uwezo wa kupima ufanisi wa vifaa vinavyotumia umeme nchini.
Uzinduzi huo umefanyika Oktoba 16, 2025 katika Ofisi za Shirika la Viwango Tanzania (TBS) Jijini Dar es Salaam, ukihudhuriwa na viongozi mbalimbali wa serikali na taasisi za kimataifa.
Akizungumza wakati wa uzinduzi huo, Dk. James Matarajio amesema matumizi ya vifaa vyenye ufanisi wa juu hupunguza mzigo kwa wananchi na taifa kwa ujumla.
Akitolea mfano kiyoyozi chenye nyota moja na kingine chenye nyota tano, amesema: “Kiyoyozi chenye nyota moja huokoa asilimia 35 ya nishati, lakini chenye nyota tano huokoa takribani asilimia 53 ya umeme unaotumika. Hii inaonyesha umuhimu wa kuchagua vifaa vyenye ufanisi mkubwa.”
Dk. Matarajio ameongeza kuwa uzinduzi wa maabara hizo umefanyika wakati muafaka, kwani Tanzania ipo katika kampeni ya kuhamasisha matumizi ya nishati safi.
“Maabara hizi zitasaidia kupima ubora na ufanisi wa vifaa kama televisheni, majokofu, viyoyozi, majiko na feni. Hatua hii itapunguza gharama kwa wananchi na kusaidia serikali kupunguza miradi mikubwa ya uzalishaji wa umeme, sambamba na kukabiliana na ongezeko la hewa ukaa,” alisema.
Kwa upande wake, Mwakilishi Mkazi wa UNDP na UNCDF Tanzania, Bw. Shigeki Komatsubara, amesema kuanzishwa kwa viwango vya matumizi ya nishati kwa vifaa vya umeme ni hatua muhimu katika kutunza nishati na kuhakikisha umeme wa uhakika.
“Utunzaji wa nishati ni nguzo ya maendeleo ya haraka ya taifa. Viwango hivi vitahamasisha uzalishaji wa vifaa vyenye ubora, kuongeza ushindani ndani na nje ya nchi, na kuimarisha ustawi wa kijamii,” amesema.
Ameongeza kuwa UNDP itaendelea kushirikiana na serikali katika kuendeleza sekta ya nishati na kuhamasisha matumizi sahihi ya nishati kwa maendeleo endelevu.
Naye Marc Stalmans, Mkuu wa Ushirikiano wa Umoja wa Ulaya (EU) nchini Tanzania na Jumuiya ya Afrika Mashariki (EAC), amesema hatua hiyo ni ishara ya mafanikio katika ushirikiano kati ya Tanzania na EU.
“Hii ni hatua muhimu kwa jamii kwani wananchi watalipa fedha kidogo kwa ufanisi ule ule. Pia ni fursa kwa wadau wa maendeleo kuwekeza zaidi kwenye miradi yenye matokeo chanya kwa taifa,” amesema Stalmans.
Kwa upande wake, Mkurugenzi Mkuu wa TBS, Dk. Ashura Katunzi, amesema mfumo mpya wa alama za nyota kwenye vifaa utawasaidia wananchi kutambua ufanisi wa kifaa husika.
“Kadri nyota zinavyoongezeka, ndivyo kifaa kinavyotumia nishati kidogo. Kwa mfano, mama lishe akitumia jokofu lenye nyota moja ataongeza gharama zake, lakini lenye nyota nne au tano litamuwezesha kuokoa muda na fedha,” amesema.
Dk. Ashura aliongeza kuwa Tanzania yenye watu takribani milioni 70 sasa inatarajiwa kufikia milioni 100 ndani ya miaka 10 ijayo, hivyo kuna haja ya kutumia umeme kwa ufanisi zaidi bila kuongeza uzalishaji mkubwa.
“Tukitumia nishati kwa busara tutapunguza matumizi ya fedha, tutatunza mazingira na kuongeza tija kwa taifa,” amesisitiza.
Aidha, amesema baada ya mfumo wa viwango kuanza kutumika rasmi, TBS itaendelea kutoa elimu kwa wazalishaji, wasambazaji na watumiaji wa vifaa vya umeme ili wote waendane na matakwa ya viwango vipya vya kitaifa.