TMA yatoa tahadhari upungufu wa mvua

Dar es Salaam. Mamlaka ya Hali ya Hewa Tanzania (TMA) imesema mvua zinazotarajiwa kunyesha Novemba mwaka huu hadi Aprili 2026, zitakuwa za wastani au chini ya wastani, hivyo kutashuhudiwa vipindi vya ukame vya muda mrefu.

Kutokana na hali hiyo, TMA imetoa angalizo kwa sekta ya kilimo, afya, mifugo na uvuvi, utalii, nishati, maji na madini, pamoja na sekta binafsi kuchukua tahadhari.

Kauli hiyo ya TMA, imetolewa na Kaimu Mkurugenzi wa Mamlaka hiyo, Dk Ladislaus Chang’a leo Oktoba 17, 2025 kwenye ukumbi wa Ubungo Plaza jijini Dar es Salaam.

“Kwa wakulima, kuna uwezekano wa kutokea kwa upungufu wa unyevu katika udongo, hivyo kuathiri ukuaji wa mazao na kuzuka kwa wadudu wanaoharibu mazao, kwa upande wa wafugaji watakumbana na upungufu wa maji na malisho.

“Kwa upande wa sekta ya utalii watapitia changamoto ya upungufu wa malisho na maji kwa wanayama pori, ikiwa tofauti na sekta ya usafirishaji ambao watanufaika na hali hii,” ameongeza

Dk Chang’a ametoa wito kwa wakulima kupata ushauri kwa wataalamu ili kupambana na hali ijayo, kwa wafugaji wanashauriwa kuweka na kutekeleza mipango bora ya matumizi na uhifadhi wa maji na vyakula vya mifugo.

Mtaalamu huyo ameshauri kuboreshwa kwa miundombinu katika mbuga za wanyama pori, nishati, maji na madini

Mbali na hayo, Mchambuzi wa Hali ya Hewa kutoka TMA, Ramadhani Omary amesema hali hiyo itaathiri hata wananchi mitaani kwa kusababisha ukosefu wa maji majumbani.

“Kipindi hiki kuna uwezekano wa kutokea kwa upungufu wa maji majumbani, kilimo na mifugo hususani katika maeneo yanayotarajia kupata mvua za chini au wastani, lakini pia vipindi vya mvua kubwa vinaweza kujitokeza na kusababisha uharibifu wa miundombinu na upotevu wa maisha na mali,” amesema Omary

Omary ameshauri serikali za mitaa kuboresha mifumo ya usambazaji maji ili kupunguza athari zinazoweza kusababisha mafuriko sambamba na kutoa elimu kwa jamii juu hatua zinazopaswa kuchukuliwa.

Vilevile, amewataka wadau na wananchi kufuatilia utabiri wa hali ya hewa kwa kila siku ili kupunguza madhara yanayoweza kutokea.

 

Katika utabiri huo, mikoa iliyopo Kanda ya Magharibi ambayo ni Kigoma Katavi Tabora, TMA imeeleza kuwa itapata mvua chini ya wastani hadi wastani zitakazoanza Oktoba mwaka huu hadi Aprili 2026.

Kanda ya Kati yenye mikoa ya Singida na Dodoma mvua zitaanza Desemba mwaka huu hadi Aprili 2026 na zitakuwa chini wastani au wastani.

Kwa Kanda ya Nyanda za juu Kusini, Magharibi yaani mikoa ya Rukwa, Songwe Mbeya Njombe, Iringa na Morogoro mvua zitaanza Novemba 2025 hadi Mei 2026 na zitakuwa chini ya wastani au za wastani.

Kwa mikoa ya Kusini yaani Lindi na Mtwara mvua zitakuwa chini ya wastani au wastani zitaanza Desemba mwaka huu hadi Mei 2026.