Dodoma — Mamlaka ya Dawa na Vifaa Tiba (TMDA) imefanikiwa kuendeleza hadhi ya Kiwango cha Tatu cha Ukomavu wa Mfumo wa Udhibiti wa Dawa na Chanjo (WHO Maturity Level 3), kufuatia ukaguzi wa Shirika la Afya Duniani (WHO) uliofanyika mwaka 2023.

Kwa mujibu wa TMDA, mafanikio hayo yanaonesha uwezo wa mamlaka hiyo kusimamia udhibiti wa dawa na chanjo kwa uwazi, weledi na kwa kuzingatia viwango vya kimataifa, hatua inayohakikisha usalama, ubora na ufanisi wa bidhaa za afya zinazotumika nchini.
Wataalamu wa afya wanasema kiwango hicho pia husaidia kulinda jamii dhidi ya dawa bandia au zisizokidhi viwango, pamoja na kuimarisha uwezo wa nchi kukabiliana na milipuko ya magonjwa na dharura nyingine za kiafya.
Aidha, kuendelea kushikilia hadhi hiyo kunaiweka Tanzania katika nafasi nzuri kimataifa, hususan katika ushiriki wa programu za pamoja za udhibiti wa bidhaa za afya, kuongeza fursa za masoko ya kikanda na kimataifa, pamoja na kuwavutia wawekezaji katika sekta ya dawa na vifaa tiba.
TMDA imeshukuru wadau wote wakiwemo washirika wa maendeleo, wataalamu wa afya na wananchi kwa mchango wao katika kufanikisha hatua hiyo muhimu kwa ustawi wa afya ya jamii.