Kuanzia Oktoba 15 hadi 17, 2025, UNESCO iliendesha mafunzo maalum ya kozi ya mtandaoni ihusuyo elimu ya kina ya stadi za maisha zinazozingatia VVU/UKIMWI, Afya ya uzazi na jinsia (CSE), hatua inayolenga kuwawezesha wanafunzi kupata maarifa muhimu kuhusu afya, usalama na ustawi wao katika maisha ya chuoni na baada ya masomo.
Akizungumza wakati wa mafunzo hayo, Mwakilishi Mkazi na Mkuu wa ofisi ya UNESCO Bw. Michel Toto alisema:
“Ushirikiano huu unaakisi dira yetu ya pamoja ya kuhakikisha kila mwanafunzi anasoma na kustawi katika mazingira salama bila vikwazo.”
UNESCO imejidhatiti kuendelea kutoa msaada wa kiufundi na kitaalamu kwa taasisi za elimu ili kuhakikisha wanafunzi wanamaliza safari zao za kielimu wakiwa na afya njema, uelewa sahihi na ujuzi wa kujilinda dhidi ya changamoto za kijamii na kiafya.
Kwa upande wake, Kaimu Mkurugenzi wa Uendeshaji wa Vyuo kutoka NACTVET, Dkt. Magreth Shawa, ambaye alizungumza kwa niaba ya Katibu Mtendaji wa Baraza hilo, aliipongeza UNESCO kwa kufadhili na kusaidia mafunzo hayo kupitia programu za “Education for Health and Wellbeing (EHW)”. Alisisitiza kuwa mafunzo hayo yatasaidia kujenga misingi imara ya elimu jumuishi inayozingatia afya, usawa wa kijinsia na ustawi wa wanafunzi wote.
Naye Mratibu wa Mradi kutoka NACTVET, Dkt. Vumilia Mmari, aliongeza kuwa ushirikiano huo kati ya UNESCO na NACTVET utaendelea kuimarisha juhudi za kuhakikisha taasisi zote za elimu ya ufundi zinakuwa na mazingira salama, yenye afya, na yanayochochea maendeleo ya kitaaluma na kijamii kwa wanafunzi.
Hatua hii ni sehemu ya mwendelezo wa jitihada za UNESCO kusaidia sekta ya elimu nchini Tanzania kupitia programu zinazolenga kuboresha afya, ustawi na usawa wa kijinsia katika taasisi za elimu ya juu na ufundi.