Dar es Salaam. Katika mazingira ya kazi ya kisasa, afya ya wafanyakazi imekuwa suala muhimu lisilopaswa kupuuzwa.
Ongezeko la magonjwa yasiyoambukiza kama kisukari, shinikizo la damu, saratani, magonjwa ya moyo na matatizo ya kupumua limezidi kuwa tishio kubwa kwa nguvu kazi duniani.
Magonjwa haya kwa kiasi kikubwa huchochewa na mitindo ya maisha isiyo bora hasa ndani ya sehemu za kazi. Wafanyakazi wengi hukabiliwa na changamoto kama kutumia muda mrefu wakiwa wamekaa bila kufanya mazoezi, lishe duni, msongo wa mawazo, na mazingira hatarishi ya kazi.
Takwimu zinaonyesha kuwa kukaa kwa zaidi ya saa sita kwa siku huongeza hatari ya vifo vya mapema kwa asilimia 19.
Msongo wa kazi, ukosefu wa muda wa mapumziko, na uhusiano mbaya kazini pia huongeza hatari ya maradhi ya akili na mwili. Wakati huo huo, ratiba ngumu hufanya wafanyakazi wakose muda wa kufanya mazoezi au kula chakula bora.
Mbali na hayo, mazingira yenye moshi, kelele, au hatari ya ajali husababisha madhara ya moja kwa moja kwa afya ya wafanyakazi.
Katika sekta kama viwanda, ujenzi, au migodi, wafanyakazi mara nyingi hukumbana na majeraha au matatizo ya kupumua.
Ripoti ya Shirika la Kazi Duniani (ILO) ya mwaka 2023 ilionyesha kuwa zaidi ya wafanyakazi milioni mbili hufariki kila mwaka kutokana na sababu zinazohusiana na kazi.
Shirika la Afya Duniani (WHO) pia linaeleza kuwa magonjwa yasiyoambukiza yanasababisha zaidi ya asilimia 70 ya vifo duniani kote. Tanzania pekee, takribani asilimia 33 ya vifo hutokana na magonjwa haya.
Hali hii si tu inasababisha mateso kwa wafanyakazi na familia zao, bali pia inapunguza uzalishaji kazini na kuongeza gharama kwa waajiri kupitia matibabu na likizo za ugonjwa.
Hata hivyo, waajiri wana nafasi ya kubadilisha hali hii. Kwa kuwekeza katika afya ya wafanyakazi, wanaweza kusaidia kupunguza mzigo wa magonjwa kazini.
Miongoni mwa hatua zinazoweza kuchukuliwa ni kuanzisha mipango ya afya katika maeneo ya kazi, kama vile kupima afya mara kwa mara na kutoa elimu kuhusu lishe bora, mazoezi, madhara ya uvutaji sigara na matumizi ya pombe.
Waajiri pia wanaweza kuhamasisha mazoezi kwa kuweka sehemu maalum kwa ajili ya shughuli za kimwili, kuanzisha vilabu vya michezo au hata kuhimiza kupanda ngazi badala ya kutumia lifti.
Kwa upande wa lishe, ni muhimu kuhakikisha chakula kinachopatikana kazini ni bora kiafya, pamoja na kutoa maji safi na matunda kwa wafanyakazi.
Kupumzika mara kwa mara kazini husaidia kupunguza uchovu na msongo wa mawazo. Mapumziko ya dakika chache kila baada ya saa kadhaa yanaweza kuongeza ufanisi kwa kiasi kikubwa.
Huduma za ushauri wa kisaikolojia kazini ni muhimu pia, kwani husaidia wafanyakazi kukabiliana na changamoto za kiakili. Hii huchangia ustawi wa kisaikolojia na kuimarisha morali kazini.
Aidha, bima ya afya ni nyenzo muhimu inayowawezesha wafanyakazi kupata huduma bora za matibabu kwa wakati. Hii si tu huwapunguzia mzigo wa kifedha, bali pia huongeza hali ya kujiamini na kujituma kazini.
Afya ya mfanyakazi si suala la mtu binafsi tu; ni jukumu la pamoja. Mwajiri anayejali afya ya wafanyakazi wake huwekeza katika rasilimali muhimu kwa maendeleo ya taasisi yake.
Wafanyakazi wenye afya huongeza uzalishaji, hupunguza gharama za matibabu, na kuongeza ushindani wa shirika sokoni.
Katika dunia inayobadilika kwa kasi, kampuni zitakazoweka ustawi wa wafanyakazi wao kuwa kipaumbele ndizo zitakazoendelea kustawi kwa muda mrefu.
Ni wakati wa kuchukua hatua sasa ili kulinda afya za wafanyakazi na kujenga jamii yenye uzalishaji imara kwa vizazi vijavyo.
