WAANGALIZI WA UCHAGUZI WATAKIWA KUTOINGILIA MCHAKATO WA UCHAGUZI MKUU

Mjumbe wa Tume Huru ya Taifa ya Uchaguzi, Mhe.Jaji wa Mahakama Kuu Asina Omari akizungumza wakati wa ufunguzi wa kikao kazi cha siku moja baina ya Tume na Waangalizi wa Ndani ya Nchi na Wakimataifa wa uchaguzi Mkuu wa Mwaka 2025 jijini Dodoma leo Oktoba 17, 2025. Kikao hicho kililenga kuwapa waangalizi hao taarifa za maandalizi ya Uchaguzi pamoja na mambo ya kuzingatia ya kiusalama na afya wakati wa uchaguzi. (Picha na INEC).

Mjumbe wa Tume Huru ya Taifa ya Uchaguzi, Mhe.Jaji wa Mahakama Kuu Asina Omari akizungumza wakati wa ufunguzi wa kikao kazi cha siku moja baina ya Tume na Waangalizi wa Ndani ya Nchi na Wakimataifa wa uchaguzi Mkuu wa Mwaka 2025 jijini Dodoma leo Oktoba 17, 2025. Kikao hicho kililenga kuwapa waangalizi hao taarifa za maandalizi ya Uchaguzi pamoja na mambo ya kuzingatia ya kiusalama na afya wakati wa uchaguzi. (Picha na INEC).

Kaimu Mkuu wa Kitengo cha Huduma za Kishereia wa INEC , Ndg. Cyprian Mbugano akiwasilisha mada kuhusu maandalizi ya uchaguzi Mkuu wa Mwaka 2025 kwa Waangalizi wa uchaguzi wa ndani na wa kimataifa.

Afisa wa Jeshi la Polisi akiwasilisha mada kuhusu usalama wakati wa uchaguzi 

Kaimu Mkurugenzi wa Huduma za Dharula na Maafa kutoka Wizara ya Afya, Bi. Yustina Muhaji akiwasilisha mada kuhusu masuala muhumu ya kuzingatia ya kiafta.

****************

Na Mwandishi wetu, Dodoma
Waangalizi wa uchaguzi wa ndani na wa kimataifa wametakiwa kuzingatia sheria za nchi na kuepuka kuingilia au kushiriki katika vitendo vyovyote vinavyoweza kuathiri au kuingilia mchakato wa Uchaguzi Mkuu unaotarajiwa kufanyika tarehe 29 Oktoba 2025 wakati wanapotekeleza majukumu yao ya uangalizi.


Wito huo umetolewa leo tarehe 17 Oktoba 2025 na Mjumbe wa Tume Huru ya Taifa ya Uchaguzi, Mhe. Jaji wa Mahakama Kuu Asina Omari, wakati akifungua kikao cha siku moja na Waangalizi hao kwa lengo la kuwapa maelekezo, taarifa muhimu na miongozo kuhusu namna ya kutekeleza majukumu yao ya uangalizi wa uchaguzi kwa mujibu wa sheria.


Katika hotuba yake, Mhe. Jaji Asina amewakumbusha waangalizi hao kutekeleza majukumu yao kwa uadilifu, uhuru, na kutokuwa na upendeleo, huku wakizingatia sheria za nchi na Mwongozo wa Waangalizi wa Uchaguzi wa mwaka 2025.


“Waangalizi wanapaswa kuepuka kuingilia shughuli za uchaguzi, kutoonyesha dhihaka kwa watendaji wa uchaguzi, au kutoa maelekezo kwa maafisa wa Tume kuhusu namna ya kufanya kazi zao,” amesisitiza Jaji Asina.


Mhe Jaji Asina ameongeza kuwa endapo kuna malalamiko au dosari yoyote inayojitokeza, waangalizi hao hawana budi kuwasilisha malalamiko hayo kwa Tume Huru ya Taifa ya Uchaguzi kwa njia ya Tume.


Katika kikao hicho, mada tatu kuu ziliwasilishwa kwa waangalizi wa uchaguzi ambapo mada ya Maandalizi ya Uchaguzi iliwasilishwa na Mkurugenzi wa Uchaguzi mada ya ma Masuala ya Usalama iliwasilishwa na mwakilishi wa Jeshi la Polisi Tanzania, na mada kuhusu Masuala ya Afya iliwasilishwa na mwakilishi kutoka Wizara ya Afya.


Pia Waangalizi hao walikabidhiwa nyaraka mbalimbali kwa ajili ya kuwawezesha kutekeleza majukumu yao. Nyaraka hizo ni Sheria ya Uchaguzi wa Rais, Wabunge na Madiwani Na. 1 ya 2024, Sheria ya Tume Huru ya Taifa ya Uchaguzi Na. 2 ya 2024, Kanuni za Uchaguzi za mwaka 2025, Kanuni za Maadili ya Uchaguzi wa 2025 na Mwongozo wa Waangalizi wa Uchaguzi wa 2025


Aidha, walikabidhiwa vitambulisho rasmi na kuaswa kuvitumia wakati wote wa kutekeleza majukumu yao. Pia walihimizwa kujitambulisha kwa Wasimamizi wa Uchaguzi katika maeneo watakayofika ili kurahisisha ushirikiano na kupata msaada inapohitajika.

Sehemu ya Washiriki wa kikao cha siku ambao ni Waangalizi wa uchaguzi wa ndani na wa kimataifa wakisikiliza maelekezo, taarifa muhimu na miongozo kuhusu namna ya kutekeleza majukumu yao ya uangalizi wa uchaguzi kwa mujibu wa sheria.