Dar es Salaam. Shirikisho la Vyama vya Magonjwa Yasiyoambukiza Tanzania (TANCDA) limeitaka jamii kubadili mifumo ya maisha kwa kufanya mazoezi zaidi, kula kwa uangalifu na kujali afya ya akili, kama sehemu ya juhudi za kitaifa za kuwa na jamii yenye afya bora.
Mtaalamu wa afya na mazoezi wa TANCDA, Dk Waziri Ndonde, alitoa kauli hiyo wakati wa uzinduzi rasmi wa Smart Health Journey, mpango bunifu unaolenga kubadili namna Tanzania inavyokabiliana na magonjwa sugu na huduma za afya kwa njia ya kidijitali (telemedicine).
“Nawapongeza Jubilee Health Insurance, Medikea Clinic na wadau wote kwa uongozi wao katika kuhimiza taifa lenye afya bora na lililounganishwa zaidi,” alisema Dk Ndonde.
Alisema magonjwa yasiyoambukiza (NCDs) kama vile shinikizo la damu, kisukari na saratani yanaendelea kuwa miongoni mwa visababishi vikuu vya vifo vya mapema nchini Tanzania. Mradi wa Smart Health Journey unaendana na Mpango wa Taifa wa Kukabiliana na Magonjwa Yasiyoambukiza, ukilenga kuzuia, kugundua mapema na kuimarisha ushirikiano kati ya sekta mbalimbali.
“Mpango huu unaimarisha huduma za afya ya msingi na mikakati ya afya ya kidijitali kwa kukuza huduma jumuishi zinazomlenga mtu mmoja mmoja,” aliongeza Dk Ndonde.
Amesema kiini cha Smart Health Journey ni mabadiliko ya fikra kutoka kwenye matibabu ya kutibu magonjwa hadi katika mtazamo wa kuzuia na kujenga afya endelevu.
“Tunapaswa kuacha kuwaona watu kama wagonjwa pekee. Wao ni baba, mama, wataalamu na viongozi wanaohitaji afya njema ili kutimiza malengo yao,” amesema.
“Mazoezi ya mwili, lishe bora na afya ya akili ni zana rahisi lakini zenye nguvu kubwa. Watu wanapofanya mazoezi zaidi, kula na kujali afya yao ya akili, wanaishi sio tu kwa muda mrefu bali pia kwa ubora zaidi.”
Alifafanua kuwa kwa kuunganisha ushauri wa maisha, ufuatiliaji wa kidijitali, msaada wa kijamii na huduma za afya ya akili, mpango huu unaleta huduma za afya karibu zaidi na maisha ya watu nje ya hospitali hadi majumbani, sehemu za kazi na katika jamii.
Mkuu wa Idara ya Ustawi na Mahusiano ya Kampuni katika Medikea Health, Dk Lilian Valerian, alisisitiza kuwa Smart Health Journey si mpango mpya wa kawaida bali ni mapinduzi katika mfumo wa huduma za afya.
“Tunatoka katika mfumo unaosubiri ugonjwa hadi ule unaotembea na mtu katika kila hatua ya safari yake ya kiafya,” amesema.
“Kupitia Medikea Afya App Limited, maono yetu ni rahisi lakini yenye nguvu kufanya huduma za afya ziwe rahisi kufikika, endelevu na zenye huruma.”
Kwa mujibu wa Dk Valerian, Smart Health Journey na jukwaa lake la Telemedicine, lililotengenezwa kwa ushirikiano na Jubilee Health Insurance, yanakusudia kuondoa vizuizi vya umbali na muda kwa kuwapa wateja wote wa Jubilee huduma ya haraka kutoka kwa madaktari na wataalamu popote walipo.
“Huduma za afya kwa njia ya mtandao (telemedicine) si jambo la kesho; ni jambo la sasa,” alisema Dk Valerian. Ndiyo njia ya kusambaza huduma za afya kwa usawa kuwafikia watu ambao hapo awali walikuwa nje ya mfumo wa huduma.”
Alieleza kuwa jukwaa hilo linawezesha huduma endelevu kwa wagonjwa wa magonjwa sugu kama kisukari na presha. Limeundwa kwa ushirikiano wa karibu na wagonjwa, madaktari na timu za huduma ili kushughulikia changamoto halisi kama ufuasi wa matibabu, msaada wa kihisia na ubora wa maisha kwa ujumla.
“Tunashuhudia matokeo halisi udhibiti bora wa magonjwa, kugundua mapema matatizo na kupungua kwa kulazwa hospitalini. Hiyo ndiyo athari halisi na huu ni mwanzo tu,” alisisitiza.
Smart Health Journey inalenga kusajili zaidi ya Watanzania milioni moja katika programu yake ya usimamizi wa magonjwa sugu ifikapo mwaka 2030.
“Tunatamani kuona Tanzania ambayo kila mwananchi anaweza kumfikia daktari kwa kubofya kitufe taifa ambalo kinga ndiyo msingi wa mfumo wa afya, si dharura,” amesema.