MASHINDANO ya kukimbia yaliyopewa jina la Yas Zanzibar International Marathon yamepangwa kufanyika Novemba 23 Novemba 2025 yakiwa na kauli mbiu ya “Kila Hatua ni Special.”
Akizungumza katika hafla ya uzinduzi wa mashindano hayo, Meneja Mawasiliano na Uhusiano YAS, Christina Murimi, amesisitiza umuhimu wa mbio hizi katika kuhamasisha afya, utalii, na maendeleo ya jamii kupitia teknolojia na ushirikiano endelevu.
“Kauli mbiu yetu inabeba ujumbe kwamba kila hatua tunayopiga, iwe ni mbio, maamuzi ya maisha, au juhudi binafsi ina thamani yake. Kila hatua ni fursa ya kujifunza, kukua, na kubadilisha maisha,” amesema Murimi.
Mbio za mwaka huu zitakuwa na njia za 5KM, 10KM, na 21KM, na washiriki wote watajisajili na kulipia kupitia mfumo wa kidigitali wa Mixx, jambo linalorahisisha usajili na kuhakikisha kila mshiriki anapata taarifa muhimu, ikiwemo uthibitisho wa usajili, namba ya mbio, na ratiba ya siku ya tukio.
Kwa upande wake kiongozi wa mbio hizo, Ali Said, amesema: “Mara zote tunapopanga mbio hizi, lengo letu ni kuunda tukio linalowaunganisha watu wa kila umri na hali ya maisha. Tunaamini kila mshiriki anaposhiriki, anakuwa sehemu ya hadithi kubwa ya Zanzibar ya afya, mshikamano, na maendeleo.”
Said ameongeza kuwa mbio hizi hazina maana ya michezo tu, bali pia ni tukio linalounganisha michezo, teknolojia, na utamaduni wa Zanzibar, likiwa kivutio cha utalii wa michezo ndani na nje ya visiwa.
Ametoa wito kwa watu kujisajili mapema mbio hizo zilizoandaliwa na Kampuni ya Mawasilino Yas kwa kushirikiana na Mixx by Yas ili kushiriki katika tukio hili la kipekee.