Bagamoyo. Mtu mmoja amefariki dunia baada ya kupigwa kipande cha mtungi wa gesi uliolipuka katika eneo la Masiwa, Kata ya Dunda, Wilaya ya Bagamoyo mkoani Pwani.
Tukio hilo lilitokea leo Jumamosi Oktoba 18, 2025 saa 11:30 wakati kijana mmoja, Musa Rashid (19), mkazi wa Masiwa, anayejihusisha na ukusanyaji wa vyuma chakavu, alipokuwa akigonga kifuniko cha mtungi wa gesi aina ya Carbon dioxide wenye uzito wa kilo 20 kwa kutumia nyundo.
Kwa mujibu wa taarifa ya Kamanda wa Polisi Mkoa wa Pwani, Salon Morcase, aliyoitoa leo, mlipuko huo ulitokea baada ya kifuniko cha mtungi huo kulipuka kwa kasi na kumgonga kichwani Mengi Waziri (25), mkazi wa eneo hilo, aliyekuwa umbali wa takribani mita 10 kutoka eneo la tukio na kusababishia kifo chake, papo hapo.
Mwili wa marehemu Waziri umehifadhiwa katika Hospitali ya Bagamoyo kusubiri taratibu za uchunguzi na mazishi.
Kamanda huyo ametoa tahadhari kwa wananchi, hasa wanaojihusisha na biashara ya vyuma chakavu, kuacha tabia ya kugonga au kukata vifaa visivyojulikana ambavyo vinaweza kuwa na gesi au mabaki ya kemikali hatarishi, kwani vinaweza kusababisha milipuko na madhara makubwa.
Baadhi ya wakazi wa Mkoa wa Pwani, wameiomba Serikali kuweka utaratibu wa kutoa elimu kwa jamii kuhusu namna salama ya kushughulikia mitungi ya gesi.
Saidi Mwinyimkuu, mkazi wa Kibaha, amesema watu wengi hawajui hatari ya kugusa au kukata mitungi iliyotumika na kwamba Serikali ingeweka kampeni maalumu ya kutoa elimu, hali kama hiyo ingeepukika.
Asha Kombo, mkazi wa Kibaha, amesema wananchi wanapaswa kupewa elimu ya namna ya kutambua mitungi hatarishi kwa kuwa wengi hudhani ni vyuma vya kawaida, kumbe vina gesi.
Kamanda wa Polisi amesema jeshi hilo litaendelea kutoa elimu na kufanya doria kuhakikisha biashara ya vyuma chakavu inafanyika kwa kufuata usalama unaotakiwa.