KOCHA Mkuu wa Pamba Jiji, Francis Baraza amesema ushindi wa mabao 2-1 walioupata dhidi ya Mashujaa FC, ni kama wametoa bahati mbaya kwenye kikosi chao na sasa watacheza kwa kujiamini na kufanya vizuri.
Kauli hiyo ya Baraza imekuja baada ya kikosi chake kuibuka na ushindi huo jana Oktoba 17, 2025 kwenye Uwanja wa CCM Kirumba, Mwanza, huku ukiwa ni ushindi wa kwanza katika Ligi Kuu Bara msimu huu.
Kabla ya ushindi huo, Pamba Jiji ilikuwa imecheza mechi tatu ikiambulia sare mbili dhidi ya Namungo (1-1) na TRA Unit-ed (0-0), na kupoteza kwa mabao 3-0 mbele ya Yanga.
Baraza raia wa Kenya amesema ushindi huo ni matokeo ya pamoja ya jitihada za wachezaji kufuata maelekezo ya benchi la ufundi, na nguvu ya mashabiki ambao waliwaunga mkono na kuleta hamasa kwenye kikosi hicho.
“Matokeo haya ni furaha kwangu vijana wamecheza na presha, niliwaambia kule kambini kuwa waende wafurahie mpira wacheze ushindi utakuja wenyewe, hivyo vijana wangu wajitahidi tena tupate ushindi mwingine na nafikiri wametoa ile gundu (bahati mbaya),” amesema Baraza.
Ameongeza: “Sasa wamepata ushindi unafungua mambo mazuri kwao, hivyo mimi nafurahia pia kwa ushindi wa leo (jana) na nafurahia vijana wangu jinsi walivyocheza, na mashabiki walivyokuja kwa wingi.”
Kocha huyo wa zamani wa Biashara United, Kagera Sugar na Dodoma Jiji, ameshangazwa na namna ambavyo baadhi ya mashabiki wa timu hiyo walivyokuwa wakitoa maneno ya kukatisha tamaa kwa wachezaji.
“Ukiangalia kwenye mitandao ya kijamii watu wanaongea vibaya juu ya Pamba tena ni watu wa hapa unajiuliza huyu ni shabiki wa Pamba na anaongea mambo kama hayo badala ya kumuinua kijana,” amesema Baraza.

Licha ya ushindi huo, Baraza amesema vijana wake walipata wakati mgumu kwa sababu walikutana na miongoni mwa timu ngumu kwenye ligi, huku akitaja mbinu zilizombeba ikiwemo pasi za haraka.
“Nilijiandaa dhidi yao, nilijua mipira mingi wanatumia mirefu na wana maumbo makubwa na vijana wangu walikuwa wadogo, nikawaambia wawe wepesi kwenye mipira, kucheza pasi za haraka na kutoka, nashukuru vijana wamefanya hivyo tukapata goli la mapema.
“Mashabiki wasituachie timu wenyewe waje kwa wingi wasapoti timu yao, hii ni timu yao, hivyo wakinipa sapoti hawa vijana bila Shaka watacheza vizuri na watapata matokeo mazuri,” amesema kocha huyo.
Wakati huohuo, mshambuliaji wa Pamba Jiji, Peter Lwasa amesema malengo yake msimu huu ni kuhakikisha anaweka rekodi ya kufunga mabao ya kutosha.
Lwasa ambaye ndiye aliifungia Pamba Jiji mabao yote mawili katika ushindi huo dhidi ya Mashujaa, ameweka rekodi ya kuwa mshambuliaji wa kwanza kufunga mabao mawili katika mechi moja ya Ligi Kuu Bara msimu huu. Akifuatiwa na Matheo Anthony aliyeifunga KMC leo Oktoba 18, 2025 wakati Mbeya City ikishinda 3-0.
Akizungumza na Mwanaspoti, Lwasa amesema, kinachoendelea kumfanya kuwa bora ni kufuata maelekezo ya timu na ndoto kubwa alizonazo.
Amesema kuwa, matokeo mazuri ambayo timu hiyo inapata kupitia yeye au kwa wenzako, ndicho kinachowaweka sehemu nzuri ya kutimiza malengo ya klabu.
“Nimeweka malengo binafsi, lakini zaidi ni kuhakikisha timu inafanya vizuri. Kwa upande wangu, nataka kuwa miongoni mwa wafungaji bora watatu wa ligi.
“Najua ni kazi ngumu, lakini ninaamini nina uwezo wa kufika huko kwa msaada wa wachezaji wenzangu na kocha wetu.
“Nataka kuacha historia nzuri kwenye soka la Tanzania, wachezaji kama Emmanuel Okwi na Hamis Kiiza wamekuwa mfano wa wachezaji wanaocheza kwa juhudi, heshima na nidhamu, mimi pia napita humo,” amesema Lwasa raia wa Uganda.