Morogoro. Chama cha Mapinduzi (CCM) kimeahidi kuufungua Mkoa wa Morogoro kwa kujenga barabara mbalimbali katika kipindi cha miaka mitano ijayo endapo kitapata ridhaa ya kuendelea kusalia madarakani.
Mbali na hilo, kimeahidi kushughulikia changamoto ya wanyama wanaovamia mazao ya wananchi kwa kutumia ‘drones’ kuwafukuza.
Ahadi hizo zimetolewa leo Jumamosi, Oktoba 18, 2025 na mgombea mwenza wa urais wa CCM, Dk Emmanuel Nchimbi alipofanya mkutano mdogo wa kampeni eneo la Mikumi, Wilaya ya Kilosa mkoani Morogoro.
Mkutano huo, umehusisha majimbo ya Mikumi na Kilosa. Dk Nchimbi amewanadi wagombea ubunge, Profesa Palamagamba Kabudi wa Kilosa na Denis Londo wa Mikumi.
Profesa Kabudi ni Waziri wa Habari, Utamaduni, Sanaa na Michezo na Londo ni Naibu Waziri wa Mambo ya Nje anayeshughulikia masuala ya Afrika Mashariki.
Baadaye amefanya mkutano Kilombero ikihusisha majimbo ya Kilombero na Mlimba. Abubakary Asenga anagombea Kilombero na Dk Kellen-Rose Rwakatale wa Mlimba.
Dk Nchimbi amewaeleza mafanikio mbalimbali kwenye sekta za afya, elimu, kilimo, mifugo na barabara na kuwaomba wananchi wawachague tena wagombea wa CCM akiwemo mgombea urais, Samia Suluhu Hassan.
Amesema katika kipindi cha miaka mitano ijayo, wanakwenda kujenga barabara za mkoa huo kwa kiwango cha lami na changarawe ili ziweze kupitika wakati wote na kurahisisha shughuli za usafiri na usafirishaji ukiwemo wa mazao ya biashara.
Mgombea mwenza huyo ameshangazwa na idadi kubwa ya barabara zilizowekwa kwenye ilani ambazo zitajengwa ukilinganisha na mikoa mingine.
Amezitaja barabara hizo kuwa ni ya; Masumbwe Kipange kilometa 17, Miombo- Kilangali- Mbamba hadi Sambamba kilometa 18, Dumila – Mkundi kilometa 3.3, Msongo – Kipande kilometa 17, Mabawa na Matete kilometa sita.
Barabara zingine ni ya Parakuyo- Twatwatwa, kilometa 24, Rudewa – Kisare kilometa 13, Berega- Mwandiga kilometa 6.3, Fuoni-Idete kilometa sita, Ruaha Mbuyuni- Chad kilometa saba na Rudewa- Unono kilometa 14.
Barabara ya Zombo ya Ulaya 24, Mamboya- Ponela kilometa 17, barabaraya Upo 14, Mvumi -Ngege kilometa 32, barabara ya Ngombe nusu kilometa 18 na barabara Magu- Butimba kilometa 22.
“Hizi zote nilizozitaja zinakwenda kujengwa kwa kiwango cha changarawe ili zipitike muda wote,” amesema Dk Nchimbi.
Barabara zitakazojengwa kwa kiwango cha lami ni Mikumi mjini kilometa mbili, barabara ya Kichangani- Kimamba kilometa 18, Dumila- Kilosa- Mikumi kilometa 143 na sehemu ya Rudewa- Kilosa Kilomita 24.
Dk Nchimbi ametaja Mradi wa ujenzi wa barabara ya Kilosa Wilaya ya Mikumi kilomita 72 na daraja la Kondoa. Ujenzi wa barabara ya Miombo- Lumuma hadi Idete kilometa 72,
“Katika mikoa yote niliyosoma miradi hii hapa imezidi mwenzangu. Imezidi na ni kwa sababu tu ya ukorofi wa wabunge wenu wanalazimisha miradi yote japo hata mikoa mingine isipate,” amesema huku wananchi wakimshangilia.
Akiwa Jimbo la Ifaraka, Dk Nchimbi nako ameahidi barabara mbalimbali za Wilaya ya Kilombero ambazo nazo zitajengwa kwa kiwango cha lami na changarawe.
Katika wanyama waharibifu hususan tembo amesema:”Tumesema kwa kutumia mfumo wa ndege kazi wanaita drones, tutatumia kuzuia wanyama waharibifu wasiingie kwenye mazao ya wakulima, ili mazao ya wakulima yawe salama na nchi yetu iwe salama.”
Ahadi hiyo ameitoa akiijbu kilio cha Asenga ambaye amesema ni kero kwa wananchi wa Kilombero na kuomba ishughulikiwe.
Kuhusu vitambulisho vya kupigia kura, Dk Nchimbi amesema:”Tutunze vitambulisho vyetu vya kupigia kura na siku ya Oktoba 29 nawaombeni wote tuchague madiwani wa Chama cha Mapinduzi.”
Akiwa Ifaraka, Dk Nchimbi amesema wanakwenda kuboresha hospitali ya Wilaya, watajenga zahanati 15, nyumba mpya za watumishi 18 wa kada ya afya, kujenga shule za msingi nne, za sekondari nane na madarasa mapya kwa shule za zamani ili wanafunzi wasibanane.
Awali, mgombea ubunge wa Mikumi, Denis Londo amesema jimbo hilo halikuwa na shule hata moja ya kidato cha tano na sita:”Hivi tunavyozungumza tuna shule tano za kidato cha tano na sita.”
Amesema jimbo hilo lilikuwa na changamoto ya maji na sasa imepungua kwa sehemu kubwa na mkandarasi anayetekeleza mradi wa Sh13 bilioni anaendelea na kazi.
Pamoja yote yaliyofanyika, Londo amesema kero kubwa ya wananchi wa Mikumi ni barabara ya kutoka Mikumi kwenda Kilosa. Ameeleza kuna fedha zimetoka za kuijenga.
“Tumepata fedha za stendi mpya ya mabasi hapa Mikumi zaidi ya Sh3 bilioni, lakini tumeweza kujenga stendi ya malori hapa Mikumi lakini tunamshukuru Rais Samia na Serikali ya Chama cha Mapinduzi. Pale soko lao liliungua na hivi tunavyozungumza tuna zaidi ya Sh2.5 bilion na nusu za kujenga soko la kisasa, lakini itakuwa na hadhi ya kupaki mabasi pale Ruaha.”
Kwa upande wake, Profesa Kabudi amesema amesema ilani ya ucha ina miradi ya mageuzi makubwa na miradi ambayo itakayotekelezwa Tanzania itabadilika: “Na ninahakika katika hilo mkono wako (Dk Nchimbi- akiwa katibu mkuu) umo na wewe utakuwa ni mtu sahihi kabisa kumsaidia Rais Samia Suluhu Hassan kuitekeleza Ilani ya CCM ambayo inaleta mapinduzi makubwa.”
“Ndani ya ilani hii kuna mambo mawili muhimu kwa Kilosa. Niseme na Mikumi, moja kilimo cha umwagiliaji kimeelezwa vizuri ndani ya ilani hii, ufugaji wa kisasa tunaamini utatatua tatizo na migogoro ya wakulima na wafugaji lakini tatu kusukuma kasi ya maendeleo vijijini,” amesema Profesa Kabudi.