CCM yajipanga kuinua uchumi, biashara Nkasi

Rukwa. Ujenzi wa stendi mpya na soko la kisasa eneo la Namanyere, ujenzi wa miundombinu ya barabara kwa viwango vya changarawe na lami, kulinda stahiki za wakulima na ujenzi wa minada mitatu ya mazao, ni miongoni mwa ahadi za Chama cha Mapinduzi (CCM) katika Wilaya ya Nkasi mkoani Rukwa, kikilenga kuinua uchumi na biashara.

Ahadi hizo na nyingine zilizopo kwenye ilani ya CCM ya mwaka 2025/2030 zimetolewa leo Jumamosi Oktoba 18, 2025 na mgombea urais wa chama hicho, Samia Suluhu Hassan katika mkutano wa kampeni uliofanyika katika mji wa Namanyere, wilayani humo.

Samia ambaye amejitambulisha kwa wananchi hao kama suluhu ya matatizo yao, amesema ahadi hizo zitakazotekelezwa kwa kipindi cha miaka mitano zimelenga kukuza na kuinua uchumi wa wananchi hao na kukuza biashara.

Kwenye sekta ya kilimo, ameahidi kuwa Serikali itahakikisha inaendelea kumlinda, kumuwezesha mkulima na kusimamia kuhakikisha wakulima wanalipwa kwa wakati kutokana na jasho lao walilolitoa.

“Tutajenga minada mitatu ya mazao ndani ya Nkasi katika vijiji vitatu ikiwemo Namanyere. Katika hatua nyingine, mji wetu wa Namanyere unaendelea kukua kwa kasi kubwa lakini hakuna soko lenye hadhi na fursa kwa wafanyabiashara na stendi ya mabasi haiendani na hadhi ya mji wa Namanyere,” amesema na kuongeza:

“Hivyo basi, ahadi yetu katika miaka mitano mkituchagua, tunakwenda kujenga soko la kisasa na stendi mpya ya mabasi katika mji wa Namanyere, miradi hii mbali na kuwa chanzo cha mapato ya halmashauri, itachochea biashara na shughuli zingine za kiuchumi kwa wananchi wa Nkasi kama wilaya nzima.”

Amesema katika kipindi cha miaka mitano inayoisha, wamemaliza kuweka umeme katika vijiji vyote nchini na kitaifa wamefikisha umeme katika nusu ya vitongoji vyote na vilivyosalia watamalizia ndani ya miaka miwili ijayo na Tanzania yote itakuwa na umeme.

Akizungumzia miundombinu ya barabara, mgombea huyo amesema barabara zote ikiwemo zinazopitika kwa shida misimu ya mvua wakipewa ridhaa miaka mitano ijayo, CCM itazijenga kwa viwango vya lami na changarawe.

Ametolea mfano barabara itakayojengwa kwa kiwango cha lami ni barabara ya Namanyere – Kizwite – Chelanganya na kuweka taa 270 katika mji wa Namanyere ili wafanyabiasgara wafanye shughuli zako usiku na mchana na barabara ya Mji Mwema – Itekesya kwa kiwango cha changarawe.

Mgombea huyo amesema suala lingine wanalolipa kipaumbele ni maji na kuwa vyanzo vilivyopo Wilaya ya Nkasi havikidhi mahitaji kwani ni vichache, hivyo suluhisho la kupata maji ni kutekeleza mradi wa maji unaotoka Ziwa Tanganyika.

“CCM kazi yetu ni kufanya kazi kustawisha, kunawirisha na kuheshimisha utu wa mtu, niwaombe sana mtupe kura zenu. Chagueni CCM tukafanye kazi tujenge utu wenu. Tuiheshimishe nchi yetu Tanzania kwa sababu watu wakiwa na maisha mazuri na nchi inapata heshima ndani na nje ya nchi,” amesema.

Awali, aliyekuwa Mwenyekiti wa Chadema Kanda ya Ziwa Victoria, Ezekiah Wenje, ambaye amejiunga na CCM hivi karibuni, amesema wapinzani wanajifanya wao ni malaika na mtu akiwa CCM anaonekana hafai kuwa huko.

“Ukiwa huku CCM, wanaona hufai kuwa huku, wao wanajiona ni malaika, wanasahau kwamba sisi sote ni wanadamu wenye upungufu, tunaoutafuta uso wa Mungu na rehema zake kila kukicha,” amesema.

Ameongeza kuwa wapinzani wanasema kwamba nchini kwa sasa demokrasia inaminywa huku akitolea mfano mwaka 2020 baada ya uchaguzi mambo yalikuwa mengi, yeye alikimbia nchini, akaenda Canada na baadhi ya viongozi wenzake wa Chadema.

Ameeleza kuwa baada ya Samia kuingia madarakani na kuanza maridhiano, walirejea nchini bila masharti.

“Hivi demokrasia ni nini, kama hayo yote ulifanya?” amehoji na kueleza kuwa siku nyingine ataeleza kwanini Chadema walisusia uchaguzi.