Changamoto tatu zabainika mwendokasi Mbagala

Dar es Salaam. Wakati huduma za mabasi ya mwendokasi kati ya Mbagala na katikati ya Jiji zimeanza kwa awamu ya majaribio, imebainika kuna changamoto kadhaa ikiwamo matumizi ya kadi, kiwango cha nauli na barabara kutumika na vyombo vingine vya moto.

Hatua hiyo ya majaribio pia inalenga kutathmini ufanisi wa mfumo wa tiketi, mwitikio wa abiria, ratiba za mabasi, usalama barabarani na utayari wa miundombinu kabla ya uzinduzi rasmi wa huduma kamili.

Changamoto hizo zimebainika leo Oktoba 18, 2025 wakati wa ziara ya maofisa wa Mamlaka ya Udhibiti Usafiri Ardhini (Latra), kwa kushirikiana na Wakala wa mabasi yaendayo haraka (DART) na Kampuni ya Mabasi Yaendayo Haraka (UDART) ikilenga kuangalia ufanisi wa majaribio hayo.

Miongoni mwa mambo yalioangaliwa ni uendeshaji wa mabasi hayo pamoja na mifumo ya kutolea huduma ikiwepo mageti janja.

Hata hivyo, baadhi ya abiria waliokuwepo katika kituo cha Mbagala wameelezea changamoto wanazozipata ikiwamo foleni ndefu na masharti ya kukata kadi yanayomtaka msafiri kutumia kitambulisho cha Taifa (Nida) na kiwango cha Sh1,000 kilichowekwa kwa kadi.

“Usafiri mzuri lakini changamoto iliyopo ni foleni ndefu, hasa wakati wa kununua au kujisajili kupata kadi. Watu bado hawajazoea mfumo wa kadi, wengine hawana taarifa sahihi jinsi ya kuipata au kuitumia,” amesema Asha Abdallah.

Mkazi wa Mkuranga, Haji Mpingi amesema kuna haja ya Serikali kukaa na kuangalia upya matumizi ya kadi ili kuepuka kuwa na kadi nyingi bila sababu ya msingi.

“Nimekuja hapa na N-card, lakini nimeambiwa haitumiki katika usafiri huu hivyo nimetakiwa kukata kadi nyingine, huu ni usumbufu kwa sabbau hakuna haja ya kuwa na kadi nyingi wakati tayari kuna kadi ambazo zilitumika tangu awali,” amesema Mpingi.

Kwa upande wake Mkurugenzi wa Kampuni ya Mofat inayoendesha mabasi hayo, Abdulrahman Kassim amesema kuwa mabasi yameanza kufanya kazi kwa utaratibu maalumu wa majaribio na tayari wameona mwitikio mzuri kutoka kwa wananchi.

“Tuko kwenye kipindi cha majaribio, na tunafurahi kuona wananchi wameanza kukubali huduma hii. Changamoto zipo, lakini tunazifanyia kazi. Mfumo wa malipo ni kwa kutumia kadi, ambapo abiria huinunua kadi kwa Sh1,000 na hulipia safari kwa Sh750,” amesema Kassim.

Kwa upande wake, Mkurugenzi wa DART, Said Tunda amesema kwenye suala la kadi bado wako kwenye majiribio kwa kuwa zipo kadi za Dart wanaanza na hizo kwa kuziweka sawa.

“Tumesema na tunaendelea kusema, kuhusu kadi bado tupo kwenye majaribio, tuna kadi za Dart tunaaanza na hizo kuziweka sawa na baadaye tunaweza kutumia hadi kadi za benki kwa maendeleo ya baadaye,” amesema.

Naye, Mkurugenzi Mkuu wa Latra, Habibu Suluo amesema hakuna ongezeko lolote la nauli katika huduma ya usafiri wa mabasi yaendayo haraka (mwendokasi) jijini Dar es Salaam, hadi pale itakapojiridhisha kuwa mifumo yote ya ukusanyaji mapato na utoaji huduma imeboreshwa ipasavyo.

Suluo amesema kuwa uamuzi huo umetokana na hitaji la kuhakikisha kuwa wananchi wanaendelea kupata huduma bora na salama bila kuongezewa gharama.

“Ni kweli gharama za uendeshaji ni kubwa, lakini hatuwezi kuongeza nauli kwa sasa. Tulishaamua tangu awali kwamba kabla hatujaruhusu ongezeko lolote, lazima tujiridhishe kuwa mfumo wa ukusanyaji wa mapato kwa njia ya kielektroniki unafanya kazi vizuri,” amesema Suluo.

Ameeleza kuwa wakati wa awamu ya kwanza ya mradi wa mwendokasi, changamoto kubwa ilikuwa ni ukusanyaji wa mapato usio sahihi kutokana na mfumo wa zamani wa ukusanyaji. Hivyo, Serikali imeamua kwanza kuimarisha mifumo hiyo kabla ya kuruhusu mabadiliko ya nauli.

Kwa mujibu wa Latra, mwaka 2022 mamlaka hiyo ilishafanya tathmini na kubaini kuwa nauli ya Sh1, 000 ingeweza kutumika endapo huduma zingeboreshwa na mfumo wa ukusanyaji mapato ungefanya kazi ipasavyo.

“Nauli ya Sh1, 000 ndiyo iliyowahi kufanyiwa kazi mwaka 2022, na inaweza kutumika kama ya muda, endapo mifumo itakamilika. Kwa sasa tunasema, hakuna ongezeko lolote hadi tutakapojiridhisha kuwa huduma zinatolewa kwa kiwango kinachostahili,” alisisitiza.

Amefafanua kuwa wawekezaji wapya hawataruhusiwa kuomba ongezeko la nauli moja kwa moja bali watapaswa kufuata utaratibu wa kisheria wa kuwasilisha maombi yao kwa Latra, ambayo yatajadiliwa kwa kushirikisha wadau wote kabla ya uamuzi kufanyika.

“Mwekezaji hawezi kuja na kusema nataka kuongeza nauli bila kufuata utaratibu. Tunazo kanuni zinazoeleza wazi kuwa lazima alete maombi, yafanyiwe tathmini, na wadau watoe maoni. Baada ya hapo ndipo mamlaka itaamua,” aliongeza.

Amesisitiza kuwa lengo ni kuhakikisha wananchi wanaendelea kunufaika na usafiri wa uhakika, salama na nafuu, huku wawekezaji wakipata fursa ya kurejesha mikopo na kupata faida halali kutokana na uwekezaji wao.

“Tunataka kila Mtanzania apate huduma bora ya usafiri. Watu wasafiri vizuri, wawe na uhakika wa usafiri, na mwekezaji apate faida yake halali bila kumuumiza abiria,” alisema.