Dk Mwinyi aahidi kujenga viwanda vya kuchaka samaki

Unguja. Mgombea urais wa Zanzibar kwa tiketi ya Chama cha Mapinduzi (CCM), Dk Hussein Mwinyi amesema akiingia madarakani watajenga viwanda vya kutosha vya kuchakata samaki ili wavuvi waendelee kuvua kwa tija.

Pia, amesema watasimamia kupunguza tozo na urasimu wa kupata leseni kwa waendesha bodaboda na bajaji.

Dk Mwinyi ametoa kauli hayo leo Jumamosi Oktoba 18, 2025 katika uwanja wa Kihinani Jimbo la Mfenesini wakati akizungumza na makundi mbalimbali ya wajasiriamali, waendesha bodaboda, bajaji na wavuvi ikiwa ni mwendelezo wa kampeni za kusaka kura kurejea tena madarakani.

“Tutajenga viwanda vya kutosha hapa Kihinani Ili mazao ya baharini hususani samaki ziwe zinasarifiwa hapahapa kukuza wavuvi na wapate tija kwa kazi hiyo,” amesema Dk Mwinyi.

Akizungumza kuhusu waendesha bodaboda na bajaji, amesema licha ya sekta hiyo kurasimishwa lakini bado kuna urasimu mkubwa wa kupata leseni kwahiyo atashughulikia tatizo hilo ili wahuska wanufaike na kazi hiyo.

Amesema wanataka waendesha bodaboda wamiliki za kwao binafsi badala ya kuajiriwa wa na watu wengine.

Kwa upande wa wakulima, amesema wataongeza pembejeo, mbolea na mbegu bora na kuimarisha mazingira ya kilimo walime kwa tija.

“Haya yote tutayafanya ili kuwainua wajasiriamali wafurahie nakuona matunda ya kazi zao,” amesema

Wakati akimnadi mgombea huyo, Naibu Katibu Mkuu wa CCM Zanzibar, Dk Mohamed Dimwa amesema Dk Mwinyi amebadilisha Zanzibar na hicho ndio kinawapa jeuri ya kutembea kifua mbele kuomba ridhaa kuongoza tena Zanzibar.

“Ametembelea katika falsafa tatu za kuondoa ujinga kwa kujenga shule, maradhi kwa kujenga Hospitali nyingi na kuondoa umasikini kwa kujenga masoko na kuwawezesha wajasiriamali,” amesema Dk Dimwa.

Awali akizungumza kwa niaba ya wajasiriamali wa soko la Pindamngongo, Haji Abbas Haji amesema wameboreshewa mazingira, kupatiwa elimu ya biashara na mikopo isiyokuwa na riba.

Hata hivyo amesema muda wa kurejesha mkopo wa miaka miwili ni mdogo hivyo wanaomba waongezewe mpaka miezi 36, sawa na miaka mitatu.

Pamoja na hayo, wameomba kuwekewa taa katika soko hilo na kumwagiwa kifusi Ili kuondosha tope na vumbi linalotokea ndani ya soko hilo.