Na Said Mwishehe,Michuzi TV
MGOMBEA Urais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania kupitia CCM Rais Dk. Samia Suluhu Hassan, amewataka wananchi wote ambao wamejiandikisha katika Daftari la Kudumu la Mpigakura, ikifika Oktoba 29 mwaka huu wajitokeze kwa wingi kuchagua viongozi wa CCM.
Akizungumza leo Oktoba 18,2025 katika mikutano yake ya kampeni kuelekea Oktoba 29 iliyofanyika wilayani Nkasi mkoani Rukwa pamoja na mambo mengine Dk.Samia amewakumbusha wananchi kujitokeza kwa wingi siku ya uchaguzi Mkuu ambayo ni Oktoba 29 mwaka huu.
Mgombea urais Dk.Samia pia amewaelekeza mabalozi wa CCM katika maeneo mbalimbali nchini kuhakikisha hakuna mwananchi aliyejiandikisha akakosa kutimiza haki yake ya msingi kwa kupigakura.
Dk.Samia amesisitiza wakati wa mkutano huo ukiwemo uliofanyika Namanyere kuwa “Kama tulivyojaza viwanja hivi tukajaze masanduku tarehe 29. Wote tulioandikishwa tutoke twende tukapige kura kama ni baba au mama, nenda naye mkapige kura.
“Ameongeza kwamba “Mabalozi hakikisheni kila aliyeandikishwa katika eneo lake anakwenda kupiga kura,” alisisitiza Dk. Samia katika mkutano huo uliohudhuriwa na maelfu ya wananchi.