Hiki hapa chanzo malori kuzagaa mitaani

Dar es Salaam. Uingiaji wa malori mitaani unatajwa kuwa chanzo cha uharibifu wa miundombinu ya majengo na barabara, pia kuhatarisha usalama wa wananchi.

Baadhi ya maeneo yanayokabiliwa na adha ya malori kuingia mitaani na wakati mwingine kuegeshwa ni Temeke, Vingunguti, Tabata, Ilala na Manzese, mkoani Dar es Salaam.

Baadhi ya malori hayo yanaripotiwa kugonga kuta za nyumba, kuangusha nguzo za umeme na kusababisha hitilafu ya utoaji huduma kwa wakazi wa maeneo husika.

Hayo yanatokana na uwepo wa barabara nyembamba ambazo hazikutengenezwa kwa ajili ya kupitisha magari makubwa, hivyo yanapopita huziba njia, hasa wakati wa kugeuza au kuegeshwa.

“Malori yanapita mitaa ya makazi usiku wa manane, yakigonga kuta za watu, baadhi yanazuia kabisa barabara na mengine yakiangusha nyaya za umeme. Tunashindwa kupumzika kwa amani,” amesema Fatuma Mohamed, mkazi wa Vingunguti.

Heri Shaban, mkazi wa Temeke, yeye anasema malori yanayoegeshwa mtaani ni kero hata kwa wanafunzi wanaosoma shule zilizopo Kata ya Temeke.

“Watoto wapo darasani, huku nje mtu anagonga vyuma, hujakaa vizuri gari limewashwa, mara limezimwa. Kelele hupigwa mchana na usiku, ukiongea unaonekana unaziba ulaji wa watu wanaochukua Sh5, 000 au Sh10,000 za ulinzi kwa kuwa mtaani yamekuwa maegesho ya magari,” anasema.

Anaeleza kuna wakati hulala giza kwa sababu ya lori kugonga nguzo za umeme.

Akizungumza na Mwananchi, Julai 23, 2025, Mwenyekiti wa Mtaa wa Temeke, Bakili Makele, amesema uingiaji malori mitaani umeibua maswali kuhusu nani anatoa vibali ili yaegeshwe maeneo yasiyostahili.

“Wakati mwingine napigiwa simu mimi mwenyekiti kuulizwa kuhusu magari hayo, lakini ukweli ni kwamba kuna ngazi nyingine za utendaji kama ofisa mtendaji wa mtaa na wa kata, ambao nao wanapaswa kuwajibika,” anasema.

Makele anasema changamoto hiyo ni ya muda mrefu na inaathiri shughuli za kijamii, hasa katika maeneo ambayo yanapaswa kuwa salama kwa watoto na watembea kwa miguu.

“Hatuungi mkono magari haya kuingia kiholela. Lakini pia kuna changamoto ya ufuatiliaji wa vibali na utekelezaji wa sheria ndogondogo. Hili linapaswa kushughulikiwa ili kuwe na utaratibu maalumu wa maegesho,” anasema.

Anasema wanaolaza magari wamekuwa wakionyesha vibali kutoka mamlaka husika vinavyowaruhusu kuegesha malori.

Mwenyekiti wa wenyeviti wa serikali za mtaa Mkoa wa Dar es Salaam, Mohamed Mwingamno, anasema kuna changamoto ya utekelezaji wa sheria.

“Kuna sheria mama ya usalama barabarani namba 30 ya mwaka 1973, ambayo imefanyiwa marekebisho mwaka 2002. Sheria hii inasimamiwa na Jeshi la Polisi kupitia kitengo cha usalama barabarani, ikitekelezwa kikamilifu hakuna gari litakalovamia barabara zisizostahili,” amesema.

Mwingamno anasema kwa sheria hiyo, sura namba 168 ya mwaka 2002, madereva wote wa malori wanapaswa kuwa na taaluma ya udereva, si tu kuwa na uzoefu. Lakini hali halisi inaonyesha wapo ambao hawajapitia mafunzo, hivyo kushindwa kuzingatia sheria.

“Tatizo siyo kukosa sheria, bali ni usimamizi wake, Tarura (Wakala ya Barabara za Vijijini na Mijini) wamejitahidi kuweka alama za onyo na amri barabarani, lakini bado magari ya mizigo yanapita kwenye barabara hizi za mitaa bila kuchukuliwa hatua madhubuti,” anasema na kuongeza:

“Wenyeviti wa serikali za mitaa hatuna mamlaka ya moja kwa moja ya kuwazuia madereva wanaovunja sheria hizi. Pia si wote wana uelewa wa sheria hizi.”

Anasema hali ni mbaya zaidi maeneo ya pembezoni, akitoa mfano wa Kigamboni ambako barabara nyingi hazina alama wala miundombinu rasmi ya usalama barabarani.

Akizungumza na Mwananchi, Julai 18, 2025, Meneja wa Tarura Mkoa wa Dar es Salaam, Godfrey Mkinga amesema licha ya kuwapo alama kuonyesha uzito wa magari yanayopaswa kutumia baadhi ya barabara, bado wapo madereva wa malori hupita kinyume cha sheria.

“Kwa mfano, kuna barabara zimewekwa alama kuwa mwisho ni tani 10, lakini unakuta lori la tani zaidi ya 15 linapita. Barabara hizi zipo za Tarura na za halmashauri, lakini wanazivamia,” amesema.

Mkinga amesema Tarura hawana Jeshi la Polisi wala mamlaka ya moja kwa moja ya kuzuia magari hayo, hivyo hutegemea ushirikiano wa wananchi na askari wa usalama barabarani ili kuwachukulia hatua wanaokiuka sheria.

“Tunaomba wananchi wakiona jambo la namna hiyo watujulishe ili tushirikiane na polisi. Tunashirikiana pia na halmashauri kwa wale wanaoegesha maeneo yasiyostahili au wanaoingiza magari maeneo yaliyopigwa marufuku,” amesema.

Amewasisitiza wananchi kulinda barabara akieleza uwepo wa alama siyo mwisho wa utekelezaji, bali anahitajika mtu wa kusimamia.

Hivyo, ametoa rai kwa wananchi kuwa sehemu ya usimamizi huo kwa kutoa taarifa pale wanapoona sheria zinavunjwa au uharibifu wa barabara unafanyika.

“Tunawahimiza wananchi na viongozi wao kuwa walinzi wa barabara, kwa sababu ni wao wanaoishi nazo. Ushirikiano huu ni muhimu kwa maendeleo endelevu ya miundombinu yetu,” amesema.

Baadhi ya wakandarasi wanaotekeleza miradi ya ujenzi wa barabara za mitaani wameeleza ubora na uwezo wa barabara hizo kupitisha magari makubwa unategemea kiwango cha ujenzi na miundombinu iliyowekwa, huku wakisisitiza hazipaswi kutumika kupitisha magari mazito.

Mmoja wa wakandarasi wa barabara, Debora Sengati anasema barabara nyingi zinazojengwa na kusimamiwa na Tarura na halmashauri za wilaya huwa na upana wa kati ya mita sita hadi nane, zikilenga kuhudumia magari ya kawaida yenye uzito usiozidi tani 10.

“Barabara hizi si za magari makubwa ya mizigo, mara nyingi zinajengwa kwa kiwango cha changarawe au lami nyepesi na makaravati yake hayawezi kuhimili uzito mkubwa. Zinakusudiwa kusaidia wananchi kufika kwao kwa urahisi, si kuhimili shehena nzito,” anasema.

Mkandarasi, Mussa Nziku, anasema baadhi ya watu wamekuwa wakitumia barabara hizo kinyume cha matumizi yake, hali inayochangia kuharibu miundombinu ndani ya muda mfupi baada ya ujenzi kukamilika.

“Wengine wanapitisha malori ya tani 20 kwenye barabara za kawaida za mitaani, hii ni hatari kwa makaravati na madaraja ya mitaa, ambayo hayajajengwa kwa kiwango hicho. Ni lazima jamii ielimishwe kuhusu matumizi sahihi ya barabara hizi,” anasema.

Akizungumza na Mwananchi Julai 23, 2025 Kamanda wa Kanda Malaamu ya Dar es Salaam, Jumanne Muliro amesema watawachukulia hatua na kuwakamata wote wanaovunja sheria, akiwataka wenyeviti wa serikali za mtaa kuwa wakali.

“Sisi tutachukua hatua tunapoona sheria zinavunjwa kwa sababu jukumu letu ni kusimamia sheria, lakini na wenyeviti wa mitaa na wao wasikubali kuona malori yanaingia mtaani kwao, kwani yanaharibu miundombinu,” amesema.

Amesema haiwezekani walione lori linaingia wakaona ni kitu cha kawaida wakati linaharibu nguzo za umeme na barabara zao, hivyo wanapaswa kuchukua hatua ili kulinda miundombinu yao.

Mwenyekiti wa Chama cha Wamiliki wa Malori ya Kati na Madogo (Tamstoa), Chuki Shabani amesema chanzo cha malori kuingia huko ni kutokana na mahitaji ya wateja.

“Leo hii magari makubwa yanaingia katikati ya makazi kutokana na uwepo wa stoo na maduka ya bidhaa ambazo tumezibeba kutoka ndani na nje ya nchi, hivyo ni vigumu kushusha katika barabara zilizoruhusiwa kupita malori na kuanza kubeba kwa magari madogo,” anasema.

Chuki amesisitiza kuwa wamiliki wa malori si adui wa maendeleo, bali wanahitaji mazingira rafiki ya kufanya kazi bila kuathiri jamii.

“Sisi si wabaya tunataka kuishi kwa amani na wananchi wote tunapata tabu na haiwezekani kontena la futi 20 ukaingiza mzigo kwenye kirikuu ili kupeleka kwenye viwanda na maeneo mengine ya ndani ya mji,” amesema.