Ibenge awakomalia mastaa Azam FC

LICHA ya Azam kushinda mabao 2-0 katika mechi ya kwanza ya raundi ya pili ya Kombe la Shirikisho Afrika dhidi ya KMKM, ila kocha wa timu hiyo raia wa DR Congo, Florent Ibenge, amesema hajabweteka na ushindi huo, hivyo bado ana kazi kubwa ya kufanya katika marudiano.

Katika mechi hiyo iliyopigwa leo Oktoba 18, 2025 kwenye Uwanja wa New Amaan Complex visiwani Zanzibar, Azam imepata ushindi huo kwa mabao yaliyofungwa na mshambuliaji, Jephte Kitambala Bola mapema tu dakika ya 6 na beki, Pascal Msindo dakika ya 42.

Akizungumza baada ya mechi hiyo, Ibenge, amesema licha ya ushindi huo ila bado wachezaji wa kikosi hicho wanatakiwa kufanya vizuri zaidi ya kile walichokionyesha dhidi ya KMKM.

“Malengo yetu ni kuvuka hatua hii lakini niseme wazi bado tuna mechi nyingine ya marudiano ambayo ndiyo itakayoamua kile ambacho kwa umoja wetu tumedhamiria kukifanya msimu huu,” amesema Ibenge na kuongeza.

“Ushindi wa mabao mawili ni mkubwa na unatupa matumaini mechi yetu ya marudio, ila tunapaswa kutambua hizi ni kama dakika 45 za kwanza na tuna nyingine pia za mwisho za kufikia kile tunachokikusudia kwa umoja wetu.”

Azam imefika hatua hii baada ya kuitoa EL Merriekh Bentiu ya Sudan Kusini kwa jumla ya mabao 4-0, ambapo kwa sasa inasaka rekodi ya kutinga hatua ya makundi ya michuano ya CAF kwa mara ya kwanza katika historia ya timu hiyo iliyoanzishwa mwaka 2004.