Mwanza. Zaidi ya washiriki 240 kutoka sekretarieti za mikoa na mamlaka za serikali za mitaa nchini wamepewa mbinu mpya za kukabiliana na changamoto katika usimamizi wa fedha za umma, udhibiti wa ndani na kupunguza hoja za ukaguzi zinazojirudia katika taasisi za umma.
Akizungumza Oktoba 17, 2025 wakati wa kufunga mafunzo ya kamati za ukaguzi yaliyofanyika jijini Mwanza, Mkurugenzi wa Ukaguzi na Ufuatiliaji Fedha katika Ofisi ya Rais Tamisemi, Denis Mbilinyi amesema Serikali imeamua kuwekeza katika mafunzo hayo ili kuhakikisha kamati za ukaguzi zinakuwa chachu ya mabadiliko na nguzo ya uwajibikaji katika taasisi za umma.
“Lengo kuu la mafunzo hayo ni kuwapa maarifa na mbinu za kisasa za kusimamia fedha za umma, kupunguza mianya ya upotevu na kuhakikisha fedha zinazotolewa na Serikali zinatumika kwa tija na matokeo yake yanaonekana kwenye maisha ya wananchi,” amesema Mbilinyi.
Mbilinyi amesema mafunzo hayo yamelenga kuondoa changamoto zilizobainishwa mara kwa mara kwenye ripoti za Mdhibiti na Mkaguzi Mkuu wa Hesabu za Serikali (CAG), ikiwemo kamati kutofanya vikao kwa mujibu wa sheria, kushindwa kupitia taarifa za kifedha kwa kina.
Zingine ni kukosekana kwa tathmini ya vihatarishi, utegemezi mkubwa wa taarifa za menejimenti bila uchambuzi wa kitaalamu pamoja na ukosefu wa mafunzo endelevu kwa wajumbe.
“Kamati hizi ni kinga ya kwanza ya kupambana na mianya ya ubadhirifu, ucheleweshaji wa taarifa za fedha na usimamizi dhaifu. Mafunzo haya yamewapa ujuzi unaohitajika ili kutekeleza jukumu hilo kwa weledi na ujasiri,” ameeleza.
Mbilinyi amewataka washiriki kuhakikisha wanatumia maarifa waliyopata kama silaha ya mapambano dhidi ya rushwa ya kifedha, matumizi holela ya bajeti na uzembe wa kiutendaji katika Serikali za Mitaa.
“Uadilifu, uwazi, ujasiri wa kutoa ushauri wa kitaalamu na kuzingatia sheria vinapaswa kuwa dira yenu. Serikali inawategemea kuwa mabalozi wa mabadiliko chanya,” amesisitiza.
Mafunzo hayo yaliyoandaliwa na Chuo cha Serikali za Mitaa Hombolo, yamefanyika kwa mgawanyo wa kanda sita nchi nzima katika mikoa ya Mbeya, Tabora, Singida, Arusha, Dar es Salaam na Mwanza.
Yamehusisha wenyeviti wa kamati za ukaguzi, makatibu, wakaguzi wa ndani, wahasibu, waweka hazina na baadhi ya wakurugenzi wa halmashauri ambapo jumla ya washiriki 244 walihudhuria mafunzo hayo, huku 66 yao wakishiriki Kanda ya Ziwa.
Mratibu wa Mafunzo na Mwezeshaji kutoka Chuo cha Serikali za Mitaa, Mark Imori amesema mafunzo hayo yamewajengea washiriki uwezo wa kufanya tathmini ya mifumo ya ndani, kutambua mapema vihatarishi vya kifedha, kushauri hatua za kuzuia upotevu wa fedha, na kuimarisha uwajibikaji wa menejimenti.
“Kamati za ukaguzi ni macho na masikio ya wananchi katika kuhakikisha hakuna fedha inayopotea bila kutoa matokeo. Kupitia mafunzo haya, tumeweka msingi imara wa utawala bora na udhibiti wa rasilimali za umma,” amesema Imori.
Nao, washiriki wa mafunzo hayo wameahidi kuendeleza ujuzi waliopata ili kupunguza hoja za ukaguzi, kuimarisha matumizi ya bajeti na kujenga imani ya wananchi kwa serikali zao za mitaa.