Kocha KMKM ajipa matumaini Chamazi

KOCHA Mkuu wa KMKM, Hababuu Ali, amesema licha ya kupoteza mechi ya kwanza kwa kuchapwa mabao 2-0 dhidi ya Azam, ila hajakata tamaa wakati miamba hiyo itakaporudiana Oktoba 24, 2025 kwenye Uwanja wa Azam Complex jijini Dar es Salaam.

Katika mechi hiyo ya kwanza ya raundi ya pili ya Kombe la Shirikisho Afrika iliyopigwa leo Oktoba 18, 2025 kwenye Uwanja wa New Amaan Complex visiwani Zanzibar, mabao ya Azam yamefungwa na Jephte Kitambala Bola dakika ya 6 na Pascal Msindo dakika ya 42.

Akizungumza baada ya mechi hiyo, Hababuu, amesema licha ya kupoteza kwa idadi kubwa ya mabao ila bado wana nafasi nyingine ya kurekebisha makosa yaliyotokea katika mechi hiyo.

“Siwezi kusema tunaenda kupindua meza mechi ya marudiano, lakini tutapambana kadri ya uwezo wetu na tuone kile kitakachotokea baada ya hapo ndipo tutajua hatima yetu msimu huu,” amesema.

Akizungumzia changamoto ya eneo la ushambuliaji la KMKM, Hababuu, amesema sio tatizo la kikosi hicho pekee, bali ni la timu nyingi, isipokuwa ni kweli anapambana nalo kila wanapocheza mechi moja baada ya nyingine.

“Tutaendelea kupambana kwa lengo la kuboresha maeneo yote muhimu ya timu, kikubwa ni kutengeneza balansi ya kikosi kiujumla kwa maana ya maeneo yote mawili uwanjani, wakati tuna mpira na tukiwa hatuna mpira pia,” amesema.

KMKM imefika raundi ya pili ya michuano ya Kombe la Shirikisho Afrika baada ya kuitoa AS Port ya Djibouti kwa jumla ya mabao 4-2, ambapo mechi zote mbili baina ya timu hizo zilichezwa Kwenye Uwanja wa New Amaan Complex visiwani Zanzibar.