Laizer alia na kiungo Fountain Gate

KOCHA wa Fountain Gate, Mohamed Ismail ‘Laizer’ amesema huu ni mwanzo mzuri kwa timu hiyo kupata ushindi nyumbani, licha ya kuwa kikosi hicho bado kuna maeneo yanavuja ikiwemo nafasi ya kiungo.

Fountain Gate jana Oktoba 17, 2025 ilipata ushindi wa kwanza katika Ligi Kuu Bara ikiwa nyumbani baada ya kuifunga Dodoma Jiji bao 1-0.

Kikosi hicho ambacho kilianza vibaya msimu kwa kufungwa mechi tatu mfululizo dhidi ya dhidi ya Mbeye City (1-0), Simba (3-0) na Mtibwa Sugar (2-0), kimepata ushindi huo ikiwa ni siku chache baada ya kukamilisha zoezi la usajili kutokana na awali kukumbana na changamoto iliyowafanya kutumia wachezaji 14 pekee.

Akizungumza na Mwanaposti, Laizer amesema, wamefanikiwa kupata ushindi wa kwanza nyumbani, japo haukuwa mchezo rahisi.

Alisema ameyaona matokeo mazuri ya maelekezo aliyowapa mastaa wa kikosi hicho katika mapumziko yaliyopita ingawa bado kuna maeneo yanashida.

“Mchezo ulikuwa na presha kubwa sana kwa upande wetu, hilo lazima niliseme kwa sababu kila mchezaji alikuwa na shauku na akili ya kufunga.

“Licha ya pointi tatu za kwanza katika mechi nne, ila lazima nikiri kwamba kwenye eneo linalohitaji muda kujijenga zaidi basi ni la kati kwani bado naona kuna mambo hayajakaa sawa.

“Eneo la kiungo linahitaji maboresho ila kwa sasa ili kuwa na muendelezo mzuri nitaendelea kukisuka kikosi zaidi hasa kwa upande wa viungo,” amesema.

Nyota wanaocheza eneo la kiungo ndani ya Fountain Gate ni Falodume Onome, Daniel Joram, Jonathan Habakkuk, Abdallah Kulandana, Frank Nduhije, Shaaban Mgunda, Sadick Ramadan, Henry David, Issa Chole, Hassan Mey na Juma Issa Abushiri.