Mambo ya kipekee ya Raila ndani ya saa 72

Dar es Salaam. Ndani ya saa 72 tangu alipopumua kwa mara ya mwisho na kwa mujibu wa matakwa yake ya kuzikwa ndani ya muda huo, kiongozi mkongwe na gwiji wa siasa za Kenya, Raila Odinga, anapumzishwa kesho Jumapili kijijini kwao Kaunti ya Kisumu.

Si hayo tu, ndani ya muda huo wa saa 72, msiba wake umeambatana na matukio ya kipekee kadhaa ikiwemo kupewa heshima ya mazishi ya hadhi ya urais, licha ya kwamba hakuwahi kushika wadhifa huo, japokuwa aligombea mara tano.

Aidha, ndege iliyosafirisha mwili wake kutoka Mumbai, India ambako alifariki dunia hadi Nairobi, Kenya, imekuwa miongoni mwa ndege zilizofuatiliwa zaidi kimataifa katika kipindi hicho.

Ndege hiyo ilikuwa ikiendeshwa na rubani Saviamaria, binti wa Balozi Brown Ondego  mmoja wa marafiki wa karibu na wa muda mrefu wa Raila Odinga,  jambo lililoongeza uzito wa kihisia katika safari ya mwisho ya kiongozi huyo.

Pia, ndege hiyo ilipotua katika Uwanja wa Ndege wa Kimataifa wa Jomo Kenyatta, ilipokelewa kwa heshima ya saluti ya mizinga ya maji ambapo magari ya zimamoto yaliimwagia ndege hiyo maji kama ishara ya heshima ya juu.

Ndege hiyo ilipowasili Nairobi, ilipewa utambulisho mpya kwa heshima ya Raila  kutoka Kenya Airways Flight KQ203 na kubadilishwa kuwa RAO001, ikimaanisha Raila Amolo Odinga 001, kama ishara ya heshima ya kipekee kwa mchango wake wa kihistoria.

Raila alipokelewa kwa heshima za kijeshi ambazo kwa kawaida hutolewa kwa viongozi waliowahi kushika wadhifa wa urais pekee.

Mwili wake ulisafirishwa kwa gari maalumu la kijeshi la kubeba silaha, likiendeshwa na maofisa wa Jeshi la Ulinzi la Kenya (KDF). Pia, mwili wake kupelekwa katika majengo ya Bunge ambapo wabunge walipata fursa ya kutoa heshima zao za mwisho.

Heshima ya aina hii hapo awali imetolewa kwa marais wa zamani, marehemu Daniel arap Moi na Mwai Kibaki.

Kofia ya Raila inajulikana zaidi kama fedora nyeupe, wakati mwingine hufahamika kama kofia ya “Godfather” kutokana na umaarufu wake katika filamu.

Mara nyingi alivalia kofia nyeupe, ingawa pia alionekana na rangi zingine na ilichukuliwa kuwa zaidi ya pambo, bali ilikuwa ni ishara ya uzee na uongozi.

Wakati wa mapokezi ya mwili wake na mazishi, kofia yake ilionyeshwa kama enzi ya mwisho na ukumbusho wa uwepo wake usiofutika katika maisha ya umma wa Kenya, iliwekwa kwenye jeneza lake.

Binti yake, Winnie Odinga aliyekuwa naye hadi umauti ulipomkuta nchini India ndiye aliyebeba kofia ya baba yake kwa mikono yake na kurudi nayo Kenya.

Alipowasili, alimkabidhi mama yake, Dk Ida Odinga, mbele ya Rais William Ruto, kama ishara ya heshima, kuthibitisha kuwa baba yao ametangulia mbele za haki, na pia kama alama ya kuendeleza urithi aliouacha.

Aidha, mkewe, Dk Ida Odinga, alisimulia safari yao ya ndoa ya miaka 52, akigusia historia yao ya pamoja, changamoto walizopitia.

Dk Ida amesema safari yao ya ndoa ya zaidi ya miaka 52, alianza mwanzoni mwa miaka ya 1970, wakapendana na kufunga ndoa mwaka 1973.

“Safari yetu ya ndoa haikuwa rahisi. Tulikumbana na changamoto nyingi, hasa alipokuwa kizuizini kama mfungwa wa kisiasa. Hata hivyo, tulijifunza kuzungumza kwa uwazi, kusema ukweli, kusamehe na kusonga mbele,” alisema Dk Ida.

Mama Ida alisema mumewe alikuwa mzalendo wa kweli aliyeipenda Kenya kwa dhati na kwamba alihuzunishwa na vitendo vya ufisadi na ubadhirifu wa mali ya umma.

“Raila alichukizwa na watu waliokuwa wakifuja mali ya wananchi na wale waliopata utajiri kwa njia za kifisadi. Aliamini katika haki, uadilifu na uwajibikaji,” aliongeza.

Akizungumza kuhusu majina ya watoto wao alisema kuwa mtoto wao wa kwanza ambaye kwa sasa ni marehemu, Fidel Castro Odhiambo Odinga, alipewa jina hilo na Raila.

Dk Ida alisema alishangaa ni kwa nini mume wake alichagua jina hilo, lakini akamwelezea kwamba alikuwa anampenda sana Fidel Castro kiongozi wa zamani wa Cuba.

Alisema walipojaaliwa mtoto wa pili wa kike, Ida na Raila walimpa jina Rosemary, Rose ni jina la mama mzazi wa Ida na Mary ni jina la mama yake Raila.

Dk Ida alisema mtoto wao tatu Raila Odinga Junior wengi wanaamini ni jina la babake, lakini mama Ida amekosoa hilo akisema alimpa jina la somo yake aliyefahamika kama Raila Kembo.

Kuhusu Winnie Odinga ambaye ni kitinda mimba, alisema jina lake lilitokana na mke wa kiongozi mpigania uhuru nchini Afrika Kusini, Nelson Mandela, ambaye ni Winnie Mandela.

Ufuatiliaji wa ndege ya Raila

Kulingana na data za ufuatiliaji zilizoripotiwa na vyombo vya habari, ambazo zilitajwa pia na BBC, ndege hiyo ilifuatiliwa moja kwa moja na zaidi ya watu 54,000 (Kulingana na Flightradar24, takwimu hii ilipanda kutoka takriban watu 21,000) katika wakati mmoja.

Kiwango hiki cha ufuatiliaji ni cha juu sana na hutokea tu kwa matukio makubwa ya kimataifa, kama vile:  Mazishi ya kifalme (kama ya Malkia wa Uingereza), majanga makubwa ya anga au matukio ya hali ya juu ya kitaifa.

Hii ilionyesha jinsi kifo cha Raila kilivyokuwa tukio la dunia na jinsi mamilioni ya watu walivyoguswa na safari ya mwisho ya kiongozi huyo.

Klabu ya soka ya Arsenal ya Uingereza imetuma salam za rambirambi kwa wananchi wa Kenya na familia kufuatia kifo cha Raila Odinga ikisema klabu hiyo ya Ligi Kuu ya Uingereza ilimtambua Odinga kama kiongozi mwenye maono na mzalendo, ikimtaja kuwa mtu aliyejitolea kwa umoja, demokrasia na haki na kuwatia moyo vizazi vingi nchini Kenya na duniani kote.

Ujumbe huo wa klabu, uliopewa jina “Official Condolence Message”, uliungana na mamilioni ya waombolezaji kote ulimwenguni kuadhimisha maisha na mchango wa Waziri Mkuu wa zamani wa Kenya.

Taarifa hiyo iliendelea kuelezea mchango wa Odinga katika demokrasia na haki za kijamii kama “taa inayoongoza vizazi vijavyo.”

Mapenzi yake kwa kandanda yalijulikana sana. Miaka yote, Raila alikuwa shabiki mkubwa wa Arsenal FC, akijadili mara nyingi matokeo ya mechi kwa mzaha na marafiki pamoja na wanasiasa wenzake.