Dar es Salaam. Tukio la kutoweka na kupatikana akiwa hoi Padri Camillus Nikata wa Jimbo Kuu la Songea, limekuwa mjadala kwenye mitandao ya kijamii likiibua maswali kibao yasiyo na majibu.
Miongoni mwa maswali yanayojitokeza kwenye mijadala ni kwa namna gani Padri Nikata ambaye ni mhadhiri katika Chuo Kikuu cha Mtakatifu Augustino Tanzania (SAUT), Mwanza, aliondoka kazini kwake, alifikaje Songea, ni kwa namna gani alitoka kwenye makazi ya mapadri hadi kwenda nyumbani kwao, aliishi vipi porini alikookotwa na ni upi ukweli kuhusu tukio hilo.
Taarifa ya kwanza ya kutoonekana kwa Padri Nikata ilitolewa na Askofu Mkuu wa Jimbo Kuu la Songea, Damian Dallu akieleza haonekani wala hapatikani kwenye simu yake.
Katika taarifa hiyo, Askofu Dallu alieleza Padri Nikata alikuwa ametokea Dodoma kwenye mafundisho ya moyo ya mapadri wanaofundisha katika vyuo vikuu vya TEC (Baraza la Maaskofu Katoliki Tanzania), akiwa na mhadhiri mwenzake, ambaye ni padri wa jimbo hilo la Songea.
“Hapa Songea alikaa katika nyumba ya mapadri St. Vianney. Alikuwa amepanga kusafiri kwenda Mwanza Oktoba 8, 2025, siku ya Jumatano asubuhi, kwa basi la Superfeo na tiketi alishainunua kwa mtandao,” ilieleza taarifa ya Askofu Mkuu Dallu na kuongeza:
“Lakini siku hiyo ya Jumatano mchana tulianza kuhisi kwamba hajasafiri kwenda Mwanza, kwani katika chumba chake kilichokuwa kimefungwa, ilionekana mizigo yake ambayo alikuwa ameiandaa kwa ajili ya safari.”
Taarifa ilieleza mtumishi wa nyumba ya mapadri alishangaa kwamba mzigo ambao padri alitakiwa auchukue kutoka kwake haukuchukuliwa. Pia mlango wa chumba ulifungwa, lakini ufunguo haukurudishwa kwa mtumishi.
“Baada ya kuona hayo, tulianza kumtafuta kwa simu na kwa kuulizia kwa watu aliokaa nao katika nyumba ya mapadri. Hata hivyo, hatukufaulu kupata chochote, maana hakupatikana kwa simu na watu hawakujua alikokwenda,” ilieleza taarifa ya askofu.
Kwa mujibu wa taarifa hiyo, ilielezwa Mwanza alikotakiwa kwenda pia hakuonekana na hakupatikana.
“Ofisi ya Superfeo ilidhihirisha kuwa Padri Nikata alinunua tiketi lakini hakusafiri kwa basi lile. Baada ya kushindikana kwa jitihada za kumtafuta kila mahali ambapo tulidhani angeweza kuwepo, tumepeleka taarifa Polisi,” ilieleza taarifa hiyo iliyoacha maswali mengi.
Katikati ya sintofahamu, Chuo Kikuu cha Mtakatifu Agustino cha Tanzania (SAUT) nacho kilitoa taarifa kikaeleza kimepokea kwa mshtuko taarifa ya Askofu Mkuu Dallu, iliyoenea kwenye mitandao ya kijamii tangu Jumatano Oktoba 8, 2025.
“Kwa namna ya kipekee uongozi wa SAUT unapenda kuuhabarisha umma kuwa Padri Camillus Nikata ni mhadhiri wetu katika Idara ya Mawasiliano ya Umma na alikwenda Dodoma kwenye mafundisho ya moyo ya mapadri wanaofundisha katika vyuo vikuu vya kikatoliki nchini, vilivyo chini ya TEC na kuwa juhudi zote za kumtafuta zilifanyika bila ya mafanikio.
“Kufuatia tukio hili la kutoonekana kwa mhadhiri wetu SAUT kupitia ofisi ya Chaplaincy, imeandaa sala maalumu kwa ajili ya kumuomba Mwenyezi Mungu kumkinga na maovu yote, kumwimarishia ulinzi na kumwongezea usalama Padri Nikata,” ilieleza taarifa hiyo Oktoba 13, 2025 ikibainisha juhudi za kibinadamu zilizkuwa zinaelekea kushindwa, hivyo kuhitaji msaada wa Mungu.
Zikiwa zimepita siku tisa tangu kutoweka kwa Padri Nikata, Jeshi la Polisi Oktoba 17, 2025 lilitoa taarifa ya kupatikana kwake na kuibua maswali zaidi.
Akizungumza na waandishi wa habari Kamanda wa Polisi Mkoa wa Ruvuma, Marco Chilya alieleza Oktoba 9, 2025 jeshi hilo lilitoa taarifa ya kupotea kwa Padri Nikata.
Kamanda Chilya alieleza baada ya kupotea kwa padri huyo, makachero wabobezi wa Jeshi la Polisi Mkoa wa Ruvuma walianza kufanya upelelezi wa kina wa kumtafuta kwa kutumia njia zote za upelelezi.
Kutokana na upelelezi huo, Oktoba 17, Padri Nikata alipatikana kwenye mashamba ya Kijiji cha Mawa, Kata ya Hanga, mahali alipozaliwa.
“Padri Camillus amepatikana akiwa hai ila akiwa amezoofu kwa njaa baada kutokula kwa siku 10 ambazo alikuwa akishindia karanga na maji,” imeeleza taarifa ya polisi.
Kwa kujibu wa polisi, alikutwa na begi lake dogo aliloondoka nalo likiwa limeanza kuliwa na mchwa, hati ya kusafiria na taulo alilokuwa ametandika chini akilitumia kulalalia.
Vilevile, alikutwa akiwa na Sh13, 500, saa ya mkononi moja, miwani, dawa aina ya Paracetamol, simu na funguo, ukiwamo wa chumba alichokuwa analala jimboni kabla ya kujipoteza.
Kamanda Chilya alieleza upelelezi umebaini sababu za padri huyo kujipoteza kwa kotokomea shambani karibu na kijiji alichozaliwa ni msongo wa mawazo uliotokana na madeni mengi yaliyokuwa chini ya uwezo wake.
Sababu nyingine amesema ni mahusiano baada ya kuachwa na mpenzi wake aliyekuwa naye kwa muda wa takribani miaka tisa, aliyekuwa akimhudumia kwa gharama kubwa.
Kwa mujibu wa polisi, kwa kipindi cha Juni hadi Septemba, imebainika alimuhudumia Sh39.158 milioni kwa kutoa kwenye akaunti yake iliyoko Benki ya CRDB.
Alisema sababu nyingine ni maradhi, kwamba kwa muda mrefu alikuwa anasumbuliwa na presha ya macho na alifanyiwa operesheni jicho moja, hivyo alihitajika kufanyiwa la pili lakini alikosa fedha kutokana na kumuhudumia mpenzi wake.
“Padri huyo alikuwa ameamua kuacha kazi ya upadri kwa sababu za kiafya, mahusiano na hali mbaya ya kifedha, lakini hakupewa nafasi ya kusikilizwa na uongozi wake,” alieleza Kamanda Chilya.
Jeshi hilo limetoa wito kwa watu wote wenye taaluma wa kada mbalimbali, bila kujali taasisi, kushirikisha wanajamii wenzao kwa matatizo yanayowakabili, badala ya kukaa nayo moyoni wenyewe.
Chilya amewaasa wakuu wa taasisi mbalimbali kuhakikisha wanawapa nafasi na kusikiliza changamoto za walio chini yao ili kuzitatua kabla hazijaleta taharuki katika jamii.
Taarifa ya polisi ilieleza hali ya Padri Nikata inaendelea kuimarika baada ya kupata huduma ya kwanza na alipelekwa hospitali ya Mkoa wa Ruvuma kwa matibabu.
Licha ya ufafanuzi wa kina, taarifa ya polisi iliibua mjadala zaidi na maswali lukuki kwenye mitandao ya kijamii, kwa kuoanisha hali hiyo na taratibu za maisha ya mapadri.
Septemba 24, 2025 Jeshi la Polisi Mkoa wa Iringa lilitangaza kumshikilia Padri Jordan Kibiki wa Kanisa Katoliki Jimbo la Mafinga kwa tuhuma za kutoa taarifa za uongo kuwa alitekwa.
Kamanda wa Polisi Mkoa wa Iringa, Alan Bukumbi, alieleza uchunguzi wa awali ulibaini Padri Kibiki alikuwa akikabiliwa na madeni baada ya kukopa fedha kutoka kwa watu mbalimbali na kushindwa kuzirudisha.
Alieleza padre huyo alitoa taarifa kupitia mtandao wa WhatsApp akidai ametekwa na kusafirishwa kuelekea Mbeya, lakini baada ya uchunguzi wa Polisi, alikutwa akiwa Mbalizi, mkoani Mbeya.
Kanisa Katoliki Jimbo la Mafinga lilitoka hadharani na kueleza umma kuwa Padri Kibiki alipata msongo wa mawazo baada ya kupata hasara ya Sh3.5 milioni kwenye biashara ya mtandaoni (eBay).
Septemba 30, 2025 Askofu wa Jimbo Katoliki la Mafinga, Vincent Mwagala, akizungumza na waandishi wa habari alieleza padri huyo alipata tatizo hilo kutokana na hali aliyokuwa anapitia.
Askofu Mwagala alisema unyongefu unaweza kumtokea mtu yeyote kutokana na hali ya kimaisha ambayo anapitia, hivyo kanisa kwa sasa linaangilia afya ya padri huyo ili aweze kurudi katika hali yake ya kawaida.
Alisema Septemba 26, 2025 baada ya kuzungumza naye na kuhisi hakuwa vizuri, walimpeleka Hospitali ya Rufaa Tosamaganga kwa ajili ya kuangaliwa afya yake na ilibainika ana unyongefu (depression), hivyo kuanzishiwa matibabu.
Vilevile, alisema hali hiyo ilichangiwa baada ya padri huyo kugundua kuwa amepata hasara ya Sh3.5 milioni kwenye biashara ya mtandaoni (eBay).
“Alipata hisia kwamba ameibiwa pale alipombiwa atume fedha nyingine kinyume cha makubaliano ya awali,” alisema.
Alisema kati ya fedha ambazo Padri Kibiki alihisi amepata hasara, Sh500, 000 alikuwa ameazima kwa Paroko, Padri Isaac; Sh1.5 milioni alikuwa ameazima kwa Mhasibu wa Jimbo la Mafinga, Padri Godwin Maliga, huku Sh1.5 milioni zilikuwa fedha zake mwenyewe.
“Hivi naweza kuona kwa kweli hakuwa na madeni makubwa kiasi hicho, kwa hali ya kawaida na mtu mwenye afya ya akili asingeweza kutelekeza porini gari lenye thamani ya Sh25 milioni,” alisema.
Alisema Jeshi la Polisi kwa kuzingatia hali ya padri huyo, limefuta tuhuma dhidi yake na kumwachia huru kutokana na kosa lililokuwa linamkabili la kusambaza taarifa za uongo kuwa ametekwa.