KOCHA wa KMC, Marcio Maximo ameonyesha kuwa na imani na ubora wa kiungo wake mshambuliaji Ibrahim Ajibu, licha ya kutompa nafasi ya kucheza mara kwa mara kwenye kikosi cha kwanza cha timu hiyo.
Maximo amesema mchezaji huyo bado yuko kwenye mchakato wa kufikia kiwango bora zaidi kitakachomrudisha kwenye hadhi yake.
“Ajibu ni mchezaji mzuri, lakini anahitaji muda. Tunamuandaa kwa ajili ya baadaye, tunajua kwamba hakutumika kwa muda mrefu hivyo hayupo fiti. KMC hatuchagui mchezaji kwa CV yake, bali kwa kile anachoonyesha uwanjani. Atakuwa muhimu kwa wakati sahihi,” amesema Maximo.
Ajibu, ambaye aliwahi kung’ara akiwa na klabu za Simba na Yanga, alijiunga na KMC kwa matumaini ya kurejea kwenye ubora wake baada ya msimu uliopita kushindwa kuonyesha makali yake akiwa na Dodoma Jiji. Hata hivyo, kocha huyo amekuwa akimpa nafasi taratibu tangu katika mashindano ya Kombe la Kagame.
Maximo amesema anafahamu uwezo mkubwa wa Ajibu katika kutengeneza nafasi, kupiga pasi za mwisho na ubunifu wake uwanjani, lakini alisema kuwa falsafa yake inamtaka kila mchezaji kuwa fiti.
“Tuna mechi nyingi bado mbele yetu na kama msimu ndio kwanza umeanza hivyo subirini mtamuona Ajibu, nahitaji kila mchezaji kuwa tayari, tunaweza kuwa sehemu nzuri baada ya wiki mbili au tatu,” ameongeza.
Katika mechi nne za kwanza za msimu, KMC imeanza kwa kuibuka na ushindi wa bao 1-0 dhidi ya Dodoma Jiji kabla ya kupoteza mbili mfululizo ikifungwa bao 1-0 kwenye kila mechi dhidi ya Singida Black Stars na maafande wa Tanzania Prisons. Leo ikiwa nyumbani, imefungwa tena mabao 3-0 na Mbeya City.
Imeshuhudiwa mechi moja pekee dhidi ya Dodoma Jiji, Ajibu akianza kikosi cha kwanza, huku nyingine dhidi ya Singida Black Stars akiwa benchi. Lakini amekosekana kabisa dhidi ya Tanzania Prisons na Mbeya City.