Samia aahidi kukuza biashara kati ya Tanzania, DRC

Katavi/Morogoro. Samia Suluhu Hassan, mgombea urais kwa tiketi ya Chama cha Mapinduzi (CCM), ameahidi kuufanya Mkoa wa Katavi kuwa njia kuu ya biashara kati ya Tanzania na Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo (DRC) kwa kuimarisha miundombunu ili mizigo kati ya mataifa hayo ipitie Ziwa Tanganyika.

Amesema wameshafanya usanifu ili kuboresha reli ya Kaliua -Mpanda yenye urefu wa kilomita 210, ili kupunguza muda wa usafiri kutoka saa saba hadi nane na kuwa saa mbili hadi tatu.

Hatua hiyo amesema itachochea maendeleo ya kiuchumi na kijamii kwa wakazi wa Katavi kupitia uboreshaji wa miundombinu, ikiwemo barabara na madaraja.

Samia, Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania anayemaliza muda wake aliahidi hayo jana katika mkutano wa kampeni kwenye uwanja wa Azimio, uliopo Mpanda mjini.

Alisema mikoa ya Katavi na Rukwa imefunguliwa kwa njia za barabara, anga, reli na usafiri wa kwenye maji. Pia wameimarisha huduma za jamii na kuwawezesha wananchi kiuchumi.

Alisema katika kuimarisha miundombinu ya usafiri na usafirishaji wamekamilisha ujenzi wa Bandari ya Karema katika mwambao wa Ziwa Tanganyika uliogharimu Sh47.9 bilioni.

Alisema ujenzi wa bandari utarahisisha usafirshaji wa abiria na mizigo kati ya Tanzania na nchi jirani ikiwamo DRC, Burundi na Zambia.

“Ujenzi wa bandari unaenda sambamba na meli mpya za mizigo katika Ziwa Tanganyika na kazi hii inandelea vizuri pia. Kuelekea mwaka 2025/30 tunataka kuona biashara kubwa kati ya Tanzania na DRC inapita katika Bandari hii ya Karema,” alisema.

Mgombea huyo alisema kwa kuwa usafiri wa kwenye maji na reli unaambatana wameshafanya usanifu kwa ajili ya maboresho ya reli ya Kaliua- Mpanda ili kupunguza muda wa kusafiri.

Kuhusu barabara, Samia alisema zipo ikiwamo muhimu inayounganisha Wilaya ya Tanganyika mkoani Katavi na ya Uvinza mkoani Kigoma, inayojengwa kwa kiwango cha lami kutoka Mpanda -Uvinza hadi Kanyani yenye urefu wa kilomita 250.4, ujenzi uliofikia asilimia 13.7 ikiwa inajengwa kwa vipande vinne na kuahidi atahakikisha inajengwa kwa kasi na kukamilika.

Mbali ya hayo, ameahidi Serikali itajenga barabara nyingine zilizoainishwa kwenye ilani ambazo ni muhimu kwa uchumi wa mkoa huo.

Kuhusu madai ya fidia, alisema ana taarifa ya uwepo wa madai hayo kwa wananchi waliopisha miradi ya maendeleo, wakiwamo 243 waliopisha ujenzi wa barabara ya Mpanda – Vikonge iliyokamilika 2021.

Alisema wananchi wengine 830 wanadai fidia kwa kupisha ujenzi wa barabara ya Mpanda hadi Sitalike.

Aliahidi kuelekeza Wizara ya Ujenzi kufanya upembuzi wa madai yatakayothibitika kuwa halali yatalipwa.

Katika hatua nyingine, chama hicho kimeahidi kuufungua Mkoa wa Morogoro kwa kujenga barabara, pia kushughulikia changamoto ya wanyama wanaovamia mazao ya wananchi kwa kutumia ndege nyuki (drones) kuwafukuza.

Mgombea mwenza wa urais wa CCM, Dk Emmanuel Nchimbi aliahidi hayo kwenye mkutano uliofanyika eneo la Mikumi, wilayani Kilosa, mkoani Morogoro.

Dk Nchimbi alisema katika kipindi cha miaka mitano ijayo, wanakwenda kujenga barabara za mkoa huo kwa kiwango cha lami na changarawe ili ziweze kupitika wakati wote na kurahisisha shughuli za usafiri na usafirishaji, ukiwemo wa mazao ya biashara.

Alizitaja barabara zilizo katika ilani kuwa ni Masumbwe Kipange kilometa 17, Miombo- Kilangali- Mbamba hadi Sambamba kilometa 18, Dumila – Mkundi kilometa 3.3, Msongo – Kipande kilometa 17, Mabawa na Matete kilometa sita.

Barabara zingine ni ya Parakuyo- Twatwatwa, kilometa 24, Rudewa – Kisare kilometa 13, Berega- Mwandiga kilometa 6.3,  Fuoni-Idete kilometa sita, Ruaha Mbuyuni- Chad kilometa saba na Rudewa- Unono kilometa 14.

Barabara ya Zombo ya Ulaya 24, Mamboya- Ponela kilometa 17, barabaraya Upo 14, Mvumi -Ngege kilometa 32, barabara ya Ngombe nusu kilometa 18 na barabara Magu- Butimba kilometa 22.

“Hizi zote nilizozitaja zinakwenda kujengwa kwa kiwango cha changarawe ili zipitike muda wote,” alisema.

Barabara zitakazojengwa kwa kiwango cha lami ni Mikumi mjini kilometa mbili, barabara ya Kichangani- Kimamba kilometa 18, Dumila- Kilosa- Mikumi kilometa 143 na sehemu ya Rudewa- Kilosa Kilomita 24.

Dk Nchimbi ametaja mradi wa ujenzi wa barabara ya Kilosa wilayani Mikumi kilomita 72 na daraja la Kondoa. Ujenzi wa barabara ya Miombo- Lumuma hadi Idete kilometa 72.

Akiwa jimbo la Ifaraka, Dk Nchimbi alizungumzia kuhusu wanyama waharibifu hususani tembo akisema: “Tumesema kwa kutumia mfumo wa drones, tutazuia wanyama waharibifu wasiingie kwenye mazao ya wakulima, ili mazao ya wakulima yawe salama na nchi yetu iwe salama,” alisema.