Dar es Salaam. Wakati Tanzania ikiendelea kupiga hatua katika kuboresha viashiria vya afya na kupunguza vifo vya mama na mtoto, bado inakabiliwa na changamoto ya udumavu na ukondefu miongoni mwa watoto.
Uwekezaji katika rasilimali watu na fedha, umetajwa kuwa nguzo muhimu katika kusaidia Taifa kuondokana na changamoto ya udumavu na ukondefu kwa watoto.
Kauli hiyo imetolewa leo, Jumamosi Oktoba 18, 2025, kwenye warsha ya uwasilishaji wa matokeo ya Mradi wa Choice Tanzania, unaotekelezwa na Taasisi ya Afya na Maendeleo ya Kimataifa ya Chuo Kikuu cha Aga Khan, Pakistan.
Mradi huo unalenga kuboresha afya ya akili na ustawi wa jamii kwa kutumia mbinu shirikishi zinazozingatia usawa wa kijinsia.
Kiongozi wa Mradi wa Choice kidunia, Dk Zulfiqar Bhutta amesema: “Tanzania imepiga hatua kubwa katika kuimarika kwa viashiria vya afya pia kuna mafanikio makubwa, ikiwemo kupunguza vifo vya mama na mtoto na mengineyo.
“Changamoto iliyobaki ni katika changamoto za kiafya zitokanazo na mabadiliko ya tabia nchi, majanga ya asili na sasa tunaingia kuhakikisha tunatoa usaidizi katika eneo hili.
“Udumavu na ukondefu imebaki kuwa changamoto kubwa, Tanzania inatakiwa kuwekeza zaidi kutumia rasilimali watu na fedha,” amesema.
Akimwakilisha Katibu Mkuu Wizara ya Afya, Dk Seif Shekalaghe, Mkurugenzi kitengo cha Sheria wizarani hapo, Rahibu Mashombo amesema: “Tunakabiliwa na mabadiliko ya hali ya hewa yanayokuja sambamba na changamoto za kiafya na masuala mtambuka ya afya ya akili, tunashirikiana na wadau mbalimbali upande huu tumeleta Mradi wa Choice.”
Warsha hiyo iliyojadili mabadiliko ya tabianchi na afya ya binadamu, imewakutanisha viongozi wa Serikali, watafiti, washirika wa maendeleo, wanasayansi, wanazuoni na asasi za kiraia kujadili suluhisho jumuishi kwa changamoto za tabianchi na afya nchini.
“Uhalisia wa mabadiliko ya tabianchi, afya ya akili na usawa wa kijinsia unaathiri namna familia zinavyoishi na jinsi Taifa linavyosonga mbele.
“Kupitia mradi wa Choice, tunajenga ushahidi, kuhamasisha hatua za kuchukuliwa, ili kujenga jamii zenye afya na ustahimilivu zaidi,” amesema Mkurugenzi Mtendaji wa Taasisi ya Huduma za Afya ya Aga Khan, Tanzania, Sisawo Konteh.
Amesema mradi umeimarisha uwezo wa kitaifa kwa kutoa mafunzo ya huduma ya kwanza ya afya ya akili kwa watoa huduma 13 na kuingiza huduma hizo katika ngazi ya msingi ya afya.
Kwa upande wa usawa wa kijinsia, amesema umewezesha wafanyakazi wa mstari wa mbele 23 kupata ujuzi maalumu wa kushughulikia ukatili wa kijinsia dhidi ya watoto, sambamba na kampeni za kitaifa za uhamasishaji.
“Katika hatua za kukabiliana na mabadiliko ya tabianchi, mradi umeanzisha msitu mdogo hospitali ya Aga Khan, kuzindua kampeni ya upandaji miti kitaifa katika mikoa sita, na kuchapisha utafiti wa kwanza wa kitaifa kuhusu mabadiliko ya tabianchi na afya kwa watoa huduma za afya nchini Tanzania,” amesema Sisawo.
Daktari Bingwa wa Magonjwa ya Wanawake na Uzazi katika AKHST na Kiongozi wa Mradi wa Choice nchini, Profesa Muzdalifat Abeid amesema vikao hivyo vinalenga kuunda mapendekezo ya vitendo ya kuimarisha ustahimilivu wa mfumo wetu wa afya.”
Kwa kushughulikia changamoto zinazowakabili wanawake, mradi unalenga kuwawezesha na kuongeza uelewa juu ya uhusiano kati ya afya ya akili, usawa wa kijinsia na sababu za kijamii zinazoathiri afya.