Umedhalilishwa kwa kukopa mtandaoni, suluhisho ni hili

Dar es Salaam. “Mwaka jana nilikumbwa na dharura ya kifamilia, nikajikuta sina njia nyingine ya haraka kupata fedha. Kwa haraka nikapakua programu ya mkopo mtandaoni. Nilikuwa na uhitaji wa Sh100, 000 na waliniahidi kwa urahisi, bila dhamana, pesa iliingia dakika tano tu baada ya kuomba, nilifurahi sana.”

Ndivyo anavyoanza simulizi Saada Jasir (si jina halisi). Licha ya kutatua changamoto iliyokuwa ikimkabili, furaha hiyo haikudumu kwani siku tatu kabla ya tarehe ya marejesho alianza kupokea simu kutoka kwa mkopeshaji akitakiwa alipe mkopo.

Simu hizo ziliambatana na ujumbe wa vitisho. Hali ilikuwa mbaya zaidi deni lilipopita siku mbili tangu tarehe aliyopaswa kurejesha mkopo huo.

“Ndugu zangu, marafiki zangu, hadi bosi wangu kazini wote walielezwa kuwa nimekimbia na mkopo na kuwa mimi ni mdanganyifu. Matusi, vitisho na kejeli vikawa sehemu ya maisha yangu. Nilihisi kama dunia imenigeuka maana kuna wakati ujumbe ulibeba tabia ambazo sina,” anasema.

Jambo hilo lilimfanya kupata mfadhaiko, kwani kila aliyekuwa na namba yake alipokea ujumbe mfupi wa maandishi uliomzungumzia vibaya.

Saada, mkazi wa Arusha ni miongoni mwa wale ambao wamepitia udhalilishaji uliofanywa na kampuni ya mikopo mtandaoni ikiwa ni baada ya taarifa zisizo za kweli kuhusu yeye kusambazwa kwa watu waliopo katika simu yake.

Hali hii imewafanya baadhi kushindwa kufahamu namna nzuri ya kushughulikia suala hili ili kufidiwa kutokana na kukosa mawasiliano ya moja kwa moja na kampuni hizo au kutojua ofisi zao zilipo.

Kampuni ambazo zimekuwa zikitoa mikopo kupitia programu mbalimbali za simu zimekuwa zikitoa fedha bila dhamana, isipokuwa mkopaji kuwa na namba ya kitambulisho cha Taifa.

Licha ya kupata fedha na kutatua changamoto zao, lakini mwisho wamekuwa wakikumbana na udhalilishaji kutokana matumizi ya lugha chafu katika kudai fedha hizo.

Mfano wa ujumbe unaotumwa

“Mambo mpenzi (jina la mteja) napatikana hapa mtaani namba yangu ya kazi (namba ya simu ya mteja) leo nina ofa kipenzi najiuza ili niweze kupata pesa kwa ajili mahitaji yangu nadaiwa mikopo na kampuni mbalimbali sasa nahitaji pesa kwa ajili hiyo na mambo yangu binafsi bei ni poa tu tutaelewana, karibu sana mpenzi.”

“Habari za muda huu, 0000000 anatumia kitambulisho chake kutapeli pesa za mtandaoni ni mwizi kibaka mdokozi pia kuwanae makini iwe kazini nyumbani mtaani huyo siyo muaminifu kwa kweli anaweza kukuibia kaa naye mbali, muogope kama ukoma hivyo anatafutwa na kampuni (inatajwa) kwa utapeli, wizi na udanganyifu wa fedha alizokopeshwa kiasi cha 357,000 amekuwa tapeli wa mikopo mtandaoni. Wewe kama mmoja aliowajaza kipindi anakopa pesa hizo mwambie afanye malipo yake sasa. Tumeambatanisha picha na kitambulisho chake whatsapp kwa uthibitisho wa mkopo wake zaidi.”

Mmoja wa wakopaji (jina linahifadhiwa) anasema kutokana na hali hiyo, wateja wamekuwa wakikimbia mikopo hali inayofanya kampuni kupata hasara kutokana na wateja kutoona haja ya kulipa baada ya kudharilishwa.

“Watu wananyanyaswa mno na kampuni kwa kisingizio cha kuwa mikopo hiyo ya mtandaoni eti ina hatari kubwa ya kutolipwa,” anasema.

Hali hii anaitafsiri kuwa wateja ni kama wameshikwa mateka na wafanyakazi, hivyo ili mteja usidhalilishwe inabidi ulipe mkopo kwani kuna baadhi ya wafanyakazi ambao wamekuwa wakiwaonyesha wateja ujumbe mfupi wa maandishi ambao watausambaza ikiwa hawajaanza kulipa.

“Anakuonyesha ujumbe mfupi wa maandishi anaotaka kuusambaza kwa watu wengi ili uogope na uamue kulipa hela kama posho au ulipe huo mkopo kusudi usitangazwe,” anasema.

Mjakani Masesa, anasema jambo hilo ni kama limefumbiwa macho na mamlaka husika kwani hakuna hatua za kisheria zinazochukuliwa kwa wahusika hali inayofanya wananchi kuendelea kufedheheshwa.

“Wamefungua kampuni ndiyo, lakini angalau wangekuwa wanawachukulia hatua kama kuwashtaki kwa udhalilishaji, hii ingesaidia kukomesha vitendo hivi,” anasema.

Haya yanasemwa wakati ambao Novemba 21, 2024, Benki Kuu ya Tanzania (BoT), ilishazifungia kutoa mikopo programu tumizi (application) 69 baada ya kuzibaini zinaendesha shughuli hiyo kidijitali bila kuwa na leseni wala idhini.

Gavana wa BoT, Emmanuel Tutuba, alisema majukwaa na programu hizo vimeshindwa kukidhi matakwa ya mwongozo kwa watoa huduma ndogo za fedha wa daraja la pili kwa wanaotoa huduma za mikopo kwa njia ya kidijitali wa mwaka 2024, uliotolewa na Benki Kuu Agosti 27, 2024.

Licha ya kufungiwa hali hiyo iliendelea kuwapo jambo lililomfanya Makamu wa Rais, Dk Philip Mpango, kuitaka BoT kushughulika tena na suala hilo.

Dk Mpango alisema siku za hivi karibuni limeibuka wimbi kubwa la wakopeshaji kupitia mitandao ya simu ambao wamejipa majina mbalimbali, ambao licha ya kutotambuliwa kisheria, wamekuwa wakiendesha shughuli zao bila kufuata taratibu za ukopeshaji.

Alisema watu hao wamekuwa wakitoa riba kubwa, kuingilia faragha za watu na kusambaza taarifa za wakopaji bila ridhaa yao.

“Kupitia hadhara hii ninavionya vikundi hivyo viache mara moja shughuli hizo kwa kuwa ni kinyume na sheria na ninaiagiza Benki Kuu ya Tanzania kulitupia jicho suala hili, ili kuwahakikishia wananchi wetu ambao wengi ni wakopaji wadogo hawaendelei kutapeliwa,” alisema.

Wakili wa kujitegemea, Dk Onesmo Kyauke amesema kukosekana kwa usimamizi madhubuti kisheria inaweza kuwa changamoto kuu.

Akitoa mfano wa benki zote kusimamiwa na BoT, huku kanuni zikiwabana na kutowapa mwanya wa kutoa taarifa za mteja kwa watu na endapo akifanya hivyo basi iwe kwa mujibu wa sheria kama amri ya mahakama, jambo ambalo kwa watu wa mitandaoni halifanyiki.

“Sijui kama hili linadhibitiwa na Mamlaka ya Mawasiliano Tanzania (TCRA) pia huenda hakuna sheria yenye nguvu inayosimamia hili, inayomtaka anayekopeshaji awe na kibali na kuwekwa njia inayoeleweka ya kudai,” anasema na kuongeza:

“Isiwe ni kuwadhalilisha watu. Lakini ukidhalilishwa unaweza kushtaki kwa kukashifiwa. Ila kama wanapewa leseni na BoT wanaweza kufanya kazi zao kwa weledi,” anasema.

Wakil Dominic Ndunguru, anasema sekta ya kukopesha ni taaluma inayotakiwa kuendeshwa kwa maadili kwani kuna vitu vinatakiwa kufanywa na vingine havitakiwi.

Anasema hilo halifanyiki kwa sababu programu nyingi hazina vibali, bali watu wameamua kuuza bidhaa za mtandanoni hali inayofanya kuwapo pengo kubwa katika maadili ya sekta.

“Mwongozo au kanuni za kusimamia maadili ya kusimamia ukopeshaji mtandaoni hakuna, kwani iliyopo sasa inatumia njia zilizozoeleka, ikiwamo watu kwenda benki kujaza fomu na kufuata taratibu zote,” anasema.

Ili kukomesha hilo ameitaka BoT ije na mwongozo na maadili kwa ajili ya wafanyakazi katika sekta hiyo na wafundishwe namna ya kukopesha kwa staha, huku uwepo wa sheria ya usimamizi wa taarifa za watu binafsi ikiwaidia kuzuia usambazaji taarifa za watu bila ridhaa yao.

“Kwa upande wa waathirika wanaweza kudai fidia kwani kuna sheria inayowalinda, ikiwemo ile ya taarifa binafsi inaweza kushtaki hizo taasisi zilizochukua taarifa zao na kuzitumia bila ridhaa yao,” anasema.

Anasema udhalilishaji unaendelea kwa sababu hakuna aliyejitokeza akafungua kesi.

Anasema zikifunguliwa kesi na wakosaji wakaadhibiwa hali itabadilika.

Katika kusimamia usalama wa mitandao, Ofisa Mawasiliano Mkuu wa Mamlaka ya Mawasiliano Tanzania (TCRA), Semu Mwakyanjala, amesema kutuma ujumbe mfupi kwa kuwasema wakopaji ni jinai na uhalifu.

TCRA inatoa leseni kwa watoa huduma wote na taratibu za kuzingatia kwa watoa huduma.

“Ni jinai, ni uhalifu, inapokwenda kwenye uhalifu sawasawa na sheria kuu ya nchi, Jeshi la Polisi ndilo yenye mamlaka ya kushughulikia suala hili. Kuna kitengo cha Jeshi la Polisi mtandaoni wanafanya doria kwenye mitandao wanaokamatwa TCRA tunaweza kuwasaidia katika kushughulikia kesi hizi,” anasema.

Amesema TCRA yenyewe haihusiki moja kwa moja na usimamizi wa wakopeshaji kwa sababu wanatumia leseni za BoT kufanya huduma za fedha mtandaoni.

Akizungumzia suala hilo, Gavana Tutuba, amesema mtu akikutana na changamoto hiyo anatakiwa kuwasilisha taarifa na ushahidi kwenye dawati la BoT, Dar es Salaam au tawi lolote nchini.

“Pia unaweza kuwasilisha malalamiko pamoja na ushahidi kupitia mfumo wa kielektroniki wa Sema na BoT ambao unapatikana katika tovuti ya Benki Kuu ya Tanzania. Mtu akiingia hapo ataona kiunganishi (link) kwa chini kabisa mwa ukurasa wa tovuti hiyo na malalamiko yake yatapokewa na kufanyiwa kazi,” anasema.