Wanafunzi waonya matumizi ya mitandao kuelekea uchaguzi mkuu

Tanga. Wanafunzi wa shule za sekondari na vyuo mbalimbali nchini wamesema matumizi yasiyo sahihi ya mitandao ya kijamii kama yanaendelea kushamiri, yanaweza kuleta madhara makubwa kwa kundi la vijana.

Wameziomba asasi za kiraia kushirikiana na Serikali katika kubuni mbinu shirikishi zitakazowezesha kutoa elimu itakayosaidia kudhibiti matumizi ya mtandao ya kijamii inayotumika kinyume na maadili.

Wanafunzi hao wametoa ombi hilo Oktoba 18, 2025 wakati wa mdahalo wa umuhimu wa Watanzania wenye sifa ya kupiga kura kushiriki uchaguzi mkuu wa Oktoba 29, 2025 ulioandaliwa na shirika la Tree of Hope na kufanyika jijini Tanga.

Mdahalo huo ulioshirikisha vijana kutoka mitaa mbalimbali pamoja na wanafunzi wa vyuo tofauti kikiwamo Chuo cha Ufundi Stadi (Veta) na shule za sekondari za Galanosi na Tanga Ufundi.

Wamesema katika kipindi hiki cha kuelekea uchaguzi mkuu wapo wanaotumia mitandao ya kijamii kwa lengo la kuipotosha jamii ikiwamo kuhamasisha watu wasijitokeze kupiga kura, jambo ambalo linahatarisha umoja wa kitaifa uliojengwa kwa miaka mingi iliyopita.

Mohamed Nassoro kutoka Chuo cha Afya Katavi amesema kasi ya uhamasishaji maandamano siku ya uchaguzi mkuu ujao inazidi kuongezeka, hivyo kuna haja kwa Serikali kuwadhibiti kwa kuwa madhara yake ni makubwa.

Kwa upande wake, Regina Khatib kutoka Chuo cha Ufundi Stadi – Veta Tanga, amezitaka pia asasi za kiraia kutumia nafasi hiyo kutoa elimu kwa jamii kuelezea faida za wananchi kushiriki uchaguzi mkuu kwa kuwapigia kura wagombea udiwani ubunge na urais wanaowataka bila kukubali vitisho kutoka mitandao ya kijamii.

Akijibu maombi hayo, mkurugenzi wa shirika lisilo la kiserikali la Tree of Hope, Fortunata Manyeresa amewataka Watanzania kukataa kurubuniwa na mitandao ya kijamii kwa kujitokeza kupiga kura Oktoba 29, 2025.

“Wanaohamasisha maandamano siku ya uchaguzi mkuu wapo nje ya nchi likitokea la kutokea wao hawapo…Wewe mwenzangu ambaye hata paspoti huna usikubali, Tanzania ni nchi yetu tujitokeze kupiga kura,” amesema.

Amesema Tanzania ni kisiwa cha amani na kimbilio la wananchi kutoka nchi mbalimbali kwa kuwa imejipambanua kusimamia ukombozi kusini mwa Afrika, hivyo wanaojaribu kuivuruga kupitia uchaguzi mkuu hawatafanikiwa.

“Nimetembelea nchi mbalimbali ndani na nje ya Afrika lakini Tanzania ni nchi pekee ambayo imejaa amani hata mgeni anaweza kutembea bila kubughudhwa…tujitokeze kupiga kura ili kuchagua kesho iliyo bora,” amesema Manyeresa.

Amewataka vijana wanaohamasisha wananchi kushiriki uchaguzi mkuu ujao waeleze hasara zinazopatikana iwapo watashindwa kwenda kupiga kura.

Miongoni mwa hasara ni pamoja na kuchaguliwa kwa mgombea ambaye hatajali maslahi ya wananchi na hivyo kuchelewesha shughuli za maendeleo ya kijamii, kisiasa kiuchumi kwa kipindi cha miaka mitano ijayo.