DAKIKA tisini za ugenini kwa Yanga leo Oktoba 18, 2025 zimekuwa ngumu baada ya kupokea kipigo cha bao 1-0 kutoka kwa wenyeji wao, Silver Strikers ikiwa ni mechi ya mkondo wa kwanza Ligi ya Mabingwa Afrika hatua ya pili iliyochezwa Uwanja wa Bingu uliopo Lilongwe nchini Malawi.
Kipigo hicho kimezidi kuchochea uvumi wa Kocha Romain Folz kibarua chake kuwa hatarini huku taarifa zikieleza muda wowote tangu filimbi ya mwisho iliyopulizwa na mwamuzi kuna kitu kinatokea.
Folz ambaye alitua Yanga Julai 14, 2025 kuchukua mikoba ya Miloud Hamdi, hadi leo alikuwa ameiongoza timu hiyo katika mechi sita za mashindano, akianza kushinda nne mfululizo, kabla ya kutoka suluhu kisha kupokea kichapo hicho.
Tangu mwanzo, licha ya Yanga kuwa na matokeo mazuri mechi nne mfululizo ikiwamo ile ya Ngao ya Jamii ambayo iliichapa Simba bao 1-0 na kutetea taji lake, lakini mashabiki walionesha kutomuelewa kocha huyo aina ya soka analofundisha.
Presha ya mashabiki wa Yanga ilikwenda hadi kwa viongozi ambao walifikia uamuzi wa kusaka mbadala wake huku ikielezwa akitoka Mfaransa huyo, anaingia kocha kutoka Madagascar, Romuald Rakotondrabe ‘Roro’.

Yanga msimu huu ilianza kuichapa Simba bao 1-0 (Ngao ya Jamii), ikaifunga Wiliete SC mabao 3-0 na 2-0 ugenini na nyumbani hatua ya awali ya Ligi ya Mabingwa Afrika, kisha kwenye Ligi Kuu Bara ikaifunga Pamba Jiji (3-0) kisha 0-0 dhidi ya Mbeya City. Ndipo jana ikafungwa 1-0 na Silver Strikers na kuacha maswali kibao kama Folz anatosha kuendelea kuwa kocha mkuu wa kikosi hicho.
Wakati Yanga ikipokea kichapo hii leo, mechi hiyo ilianza kwa mashambulizi ya hapa na pale, wenyeji walitumia vizuri shambulizi la dakika ya 76 lililoanzishwa na kipa George Chikooka, pasi ikaenda kwa beki wa kulia McDonald Lameck ambaye alimpasia kiungo wa kati Uchizi Vunga aliyeukokota mpira kwa muda mrefu hadi amekaribia boksi la Yanga, ndipo akamuachia Ernest Petro aliyempa pasi mfungaji Andrew Joseph na kumuacha kipa wa Yanga, Djigui Diarra na mabeki wake, Dickson Job na Ibrahim Bacca washindwe la kufanya.
Kabla ya kuingia bao hilo, timu zote zilifanya mabadiliko ya wachezaji kadhaa ambapo Yanga ilimtoa Andy Boyeli na kuingia Prince Dube huku Celestine Ecua akichukua nafasi ya Mudathir Yahya. Baadaye Israel Mwenda akampisha Edmund John.
Mechi hiyo imeifanya Silver Strikers kuibuka na ushindi wa kwanza katika mashindano ya kimataifa msimu huu baada ya hatua ya awali kutoka sare mbili na Elgeco PLUS licha ya kufuzu ambapo ilipenya kwa faida ya bao la ugenini. Ilianza ugenini matokeo yakiwa 1-1, nyumbani ikatoka 0-0.
Yanga ina nafasi ya kujiuliza katika mechi ya marudiano itakayochezwa Jumamosi Oktoba 25, 2025 kwenye Uwanja wa Benjamin Mkapa, Dar ambapo inahitaji ushindi wa tofauti ya mabao kuanzia 2-0 ili kufuzu hatua ya makundi ya Ligi ya Mabingwa Afrika kwa msimu wa tatu mfululizo.

SILVER STRIKERS: George Chikooka, McDonald Lameck, Nickson Mwase, Maxwell Paipi, Dan Sandukira, Zebron Kalima, Uchizi Vunga, Chikondi Kamanga, Levison Maganizo, Stanie Davie na Andrew Joseph.
YANGA: Djigui Diarra, Israel Mwenda, Chadrack Boka, Dickson Job, Ibrahim Bacca, Aziz Andabwile, Maxi Nzengeli, Mudathir Yahya, Andy Boyeli, Mohamed Doumbia na Pacome Zouzoua.