Unguja. Tume ya Uchaguzi ya Zanzibar (ZEC) imepokea rasmi karatasi za kura zilizochapishwa na Wakala wa Serikali wa Uchapaji Zanzibar (ZGP), ikiwa ni hatua muhimu katika maandalizi ya Uchaguzi Mkuu wa mwaka 2025.
Wakati karatasi hizo zikipokewa, wawakilishi wa vyama vya siasa wameoneshwa kuridhika na hatua hiyo huku wakipongeza ushirikishwaji unaofanywa na ZEC.
Akizungumza wakati wa hafla ya makabidhiano hayo leo Oktoba 18, 2025, Mkurugenzi wa Uchaguzi, Thabit Idarous Faina amesema mchakato wa kupata mzabuni ulifanyika kwa umakini mkubwa kupitia utaratibu maalumu wa zabuni uliofanya tathmini ya viwanda vinne vya uchapaji.
Kampuni zingine zilizoshindanishwa Lebone Litho Printers (PTY) Ltd, UniPrinter iliyopo Durban, Afrika Kusini, Kampuni ya nchini China ya Electronics Shenzhen Company (CES).
“Baada ya tathmini hiyo, Tume iliamua kumpatia zabuni Wakala wa Serikali wa Uchapaji Zanzibar (ZGP) kutokana na ubora wa huduma, uzoefu, viwango vya kiusalama vya uchapaji na ukaribu wa usimamizi wa kazi hiyo,” amesema.
Mkurugenzi Faina amesema wametumia Sh908.327 milioni wakati bajeti iliyokuwa imetengwa awali ilikuwa Sh 1.245 bilioni jambo linaloonyesha kuwa kazi hiyo imefanyika kwa gharama nafuu bila kuathiri ubora.
“Hii ni dalili ya matumizi bora ya rasilimali za umma na ufanisi katika utekelezaji wa majukumu ya kitaifa,” amesema Mkurugenzi Faina.
Ameongeza kuwa kwa mujibu wa makubaliano, karatasi hizo zilitarajiwa kukabidhiwa ifikapo Oktoba 23, 2025 lakini zimekamilika na kukabidhiwa kabla ya muda huo, jambo linaloashiria ufanisi mkubwa na uzingatiaji wa muda wa mzabuni.
“Kupokelewa kwa karatasi hizi za kura leo ni ishara ya hatua muhimu kuelekea maandalizi ya vifaa vyote vya Uchaguzi. Hivyo, Tume itaendelea na hatua zinazofuata kwa utulivu, umakini na ufanisi,” amesema.
Mkurugenzi Faina amepongeza ushirikiano wa karibu na wadau wote wa uchaguzi wakiwemo Vyama vya Siasa, waangalizi wa uchaguzi, vyombo vya Habari na wananchi kwa ujumla.
“Tunaendelea kuhimiza ushirikiano ili kuhakikisha uchaguzi unafanyika kwa amani, uhuru, haki na uwazi,” ameongeza.
Akizungumza kwa niaba ya Chama Cha Mapinduzi, Omar Kilupi amesema wameridhika na hali hiyo na hawana shaka kwamba wataendeleza umoja wao kuhakikisha uchaguzi unakuwa salama, haki na huru
Naye Omar Said Shaabani, mwanasheria mkuu wa ACT Wazalendo, amesema hatua hiyo inathibitisha kuwa maandalizi ya uchaguzi yanakwenda vizuri kwa upatikanaji wa karatasi hizo.
“Nasisi tunawatakia Tume kila la kheri katika maandalizi yao mengine ya mchakato wa upigaji wa kura,” amesema Omar.
Ali Mohamed Ali kutoka chama cha Ada Tadea, amesema wameridhishwa na hatua hiyo na kwamba hiyo ndio falsafa yao ya kutaka kushirikishwa katika kila hatua, jambo ambalo linaondoa sintofahamu zinazoweza kujitokeza
“Unapomshilikisha mtu, hatua kwa hatua kila kinachoendelea basi inaondoa malalamiko, hata sisi wadau wa uchaguzi tumekuwa tukishirikishwa kila hatua, hili ni jambo la kupongeza hatuwezi kulalamika katika hili,” amesema.