Hai. Baraza Kuu la Waislamu Tanzania (Bakwata) mkoani Kilimanjaro, limewataka wananchi kutambua umuhimu wa kupiga kura, ikisisitiza kuwa ni wajibu wao wa Kikatiba.
Wito huo umetolewa leo Jumapili Oktoba 19, 2025 na Sheikh wa Mkoa wa Kilimanjaro, Shaabani Mlewa alipozungumza katika Msikiti wa Shafii, Bomang’ombe wilayani Hai.
Sheikh Mlewa amewataka waumini wa dini hiyo kuhakikisha wanatekeleza wajibu wao wa Kikatiba kwa kujitokeza kupiga kura na kudumisha amani wakati wa uchaguzi huo.
Amesema bila amani, hakuna maendeleo yanayoweza kupatikana.

Waumini wa Dini ya Kiislamu,msikiti wa Safii Bomang’ombe Wilaya ya Hai mkoa wa Kilimanjaro ,wakimsikiliza sheikh wa mkoa Shaabani Mlewa
“Uislamu maana yake ni amani, hivyo haiwezekani Muislamu akawa chanzo cha kuvunja amani. Nawaomba sana, baada ya kupiga kura turudi majumbani, tupumzike na tusubiri matokeo kwa utulivu,” amesema Sheikh Mlewa.
Ameongeza kuwa, kipindi cha kuelekea uchaguzi mara nyingi huambatana na changamoto nyingi, hivyo ni muhimu kwa wananchi wote kuwa watulivu na kuepuka kushawishiwa kushiriki katika vitendo vya vurugu.
Sheikh Mlewa amewataka Maimamu na Masheikh wa wilaya zote za mkoa kuendelea kuhimiza waumini wao kujitokeza siku ya uchaguzi, akisisitiza kuwa, kupiga kura ni wajibu wa Kikatiba na njia ya kuchagua viongozi wenye nia ya kuleta manufaa kwa wananchi.
Mustaphar Munisi mmoja wa waumini waliohudhuria ibada hiyo, amesema wito wa kuhimiza amani na ushiriki wa wananchi kupiga kura ni jambo muhimu linaloonesha uzalendo.
Amesema kuna nchi ambazo amani imetoweka na watu wanateseka kutokana na migogoro, hivyo ni wajibu wa Watanzania kuendelea kulinda amani waliyonayo.
“Sheikh amesema kweli. Bila amani hakuna maendeleo. Tujitokeze kupiga kura na tuendelee kulinda amani yetu,” amesema Munisi.