Dar es Salaam. Wakati Idara ya Uhamiaji Tanzania ikisema Makamu Mwenyekiti wa Chama cha Demokrasia na Maendeleo (Chadema), John Heche ameondoka nchini kwa kuvuka mpaka na kuingia nchi jirani (Kenya) bila kufuata utaratibu na kanuni za uhamiaji, kiongozi huyo amejibu kuwa, yupo kijijini kwao Tarime mkoani Mara.
Heche ambaye Jumamosi Oktoba 18, 2025 uongozi wa Chadema Kanda ya Serengeti ulidai amezuiwa kusafiri kwenda Kenya kuhudhuria maziko ya aliyekuwa Waziri Mkuu wa Kenya, Raila Odinga amezungumza kwa simu na Mwananchi leo Oktoba 19, 2025 na kueleza sakata hilo lilivyotokea.
Licha ya taarifa iliyotolewa na Msemaji wa Idara ya Uhamiaji, Paul Mselle kueleza Heche ameondoka nchini na kuvuka mpaka kuingia nchi jirani bila kufuata utaratibu na kanuni za uhamiaji, kiongozi huyo wa Chadema amesema hajasafiri kwenda Kenya, akidai pasipoti yake imechukuliwa na kwa sasa (leo Oktoba 19, 2025 saa 5:39 mchana) yupo kijijini kwao Tarime.
Katika mahojiano na Mwananchi, Heche amedai zuio hilo la kusafiri ni la kisiasa na sio mambo ya kutofuatwa kwa utaratibu kama taarifa ya msemaji wa uhamiaji inavyoeleza.
Taarifa ya uhamiaji iliyotolewa jana Oktoba 18 usiku, inaeleza Heche ameondoka nchini kwa kuvuka mpaka na kuingia nchi jirani bila kufuata utaratibu na kanuni za uhamiaji zilizoundwa chini ya Sheria ya Uhamiaji Sura ya 54.
“Oktoba18 2025 katika Kituo cha Uhamiaji cha mpaka wa Sirari mkoani Mara, Makamu Mwenyekiti wa Chadema (Heche) ameondoka nchini kwa kuvuka mpaka na kuingia nchi jirani bila kufuata taratibu na kanuni za uhamiaji.
“Idara ya uhamiaji inatoa wito kwa raia wa Tanzania na wageni wote wanaotoka na kuingia nchini kufuata taratibu na kanuni zinazoongoza uingiaji, ukaazi na utokaji wa watu nchini ili kuepuka kutenda kosa na kuchukuliwa hatua za kisheria,” inaeleza taarifa hiyo iliyotolewa na Mselle.
Akizungumza na Mwananchi kuhusu zuio hilo, Heche amesema si kweli kwamba, hakufuata utaratibu kama taarifa hiyo inavyodai.
“Hapa Sirari kuingia Kenya hakuna ukuta, ni kwetu, nazifahamu njia zote kama ningetaka kuingia bila kufuata utaratibu ningepita njia za panya, kunizuia nisisafiri ni masuala ya kisiasa tu.
“Kama viongozi wa Chadema wana shida yeyote na idara ya uhamiaji wangepaswa kuitwa na kuelezwa, lakini kinachofanyika hivi sasa ni mambo ya kisiasa na hakuna utaratibu wowote aliovunja.
“Hata wakinihitaji sasa hivi nipo nyumbani, sijavuka nipo nyumbani nimekaa wakinihitaji nipo tayari kwenda,” amesema Heche.
Amesema alifuata utaratibu wote unaohitajika na idara ya uhamiaji huku akihoji kuwa kama asingefuata utaratibu, angepita njia za panya ili kuingia Kenya na si uhamiaji kusema hakufuata utaratibu.
“Mipaka ya Tanzania na Kenya haina ukuta, sasa ningetaka kupita ningepita kwa sababu nimezaliwa hapa nazijua njia, hivyo suala la kusema sijafuata utaratibu sio kweli,”amesema.
Heche amesema hoja alizopewa hadi kuzuiwa kwake na ofisa uhamiaji ni kwamba ana kesi, ilhali hana kesi yeyote inayomzuia kusafiri nje ya nchi.
“Hoja waliyoitoa wakati wananizuia ni kwamba eti mimi nina kesi sitakiwi kusafiri, lini wamenihitaji wakanikosa?
“Sina zuio lolote la Mahakama la kunizuia kusafiri kwenda nje ya nchi, sina zuio lolote la polisi au mtu yeyote, wamenizuia kusafiri na hadi sasa (Oktoba 19, 2025 saa 5:39 asubuhi, wamechukua pasipoti yangu hawajanirejeshea,” amedai Heche.
Mselle alipotafutwa kuulizwa juu ya madai ya Heche kuchukuliwa hati yake ya kusafiria, simu yake haikupokewa na alipotumiwa ujumbe mfupi wa maneno (meseji) hakujibu.
Hata hivyo, Heche amedai yeye si kiongozi wa kwanza wa Chadema kuzuiwa kusafiri na kuwataja wengine.
“Hata Naibu Katibu Mkuu wa Chadema Amani Golugwa alizuiwa Uwanja wa Kimataifa wa Mwalimu Julius Nyerere (JNIA). Alizuiwa mkurugenzi wetu wa habari na mawasiliano, Brenda Rupia kusafiri kwenda nje ya nchi, mjumbe wa kamati kuu Chadema, Godbless Lema alizuiwa, yaani ni kweli viongozi wote wa Chadema wanavunja utaratibu…?”amehoji Heche.
Waliowahi kuzuiwa na ufafanuzi
Kwa mujibu wa taarifa ya Juni 13, 2025 ya Polisi Kanda Maalumu ya Dar es Salaam, Golugwa alikamatwa usiku katika Uwanja wa Ndege wa Kimataifa wa Julius Nyerere lango namba 03 (terminal 03) akiwa katika maandalizi ya kusafiri kuelekea Brussels nchini Ubelgiji.
“Jeshi la Polisi lilimkamata Naibu Katibu Mkuu huyo kufuatia taarifa za siri kuwa amekuwa na mienendo ya kuondoka na kurudi nchini bila kufuata taratibu za kisheria hapa nchini,”taarifa ya polisi inaeleza.
Polisi inaeleza kuwa, inaendelea na uchunguzi wa kina wa taarifa hizo kwa kushirikiana na vyombo vingine vya usalama kuhusu suala hilo.
“Jeshi la Polisi linatoa wito kwa wananchi kuendelea kuwa watulivu wakati uchunguzi ukiendelea na kupuuza taarifa za upotoshaji kuhusu hatua hizi za kisheria zinazomhusu mtajwa,” inaeleza.
Pia, Juni 6, 2025 Lema kupitia mitandao yake ya kijamii alilalamika kuzuiwa kutoka nchini kupitia mpaka wa Namanga.
Lema kupitia mitandao yake ya kijamii aliandika kuwa zuio lake katika mpaka wa Namanga linawalenga viongozi wote wa Chadema.
Juni 13, 2025 Idara ya Uhamiaji ilitoa ufafanuzi ikisema, “idara ya uhamiaji inatoa wito kwa wananchi kupuuza taarifa za uongo zilizochapishwa na Lema kupitia mkitandao ya kijamii kuwa zuio hilo linawalenga viongozi wote wa Chadema.”
Idara ya Uhamiaji kupitia taarifa yake hiyo ilikiri kushikilia hati ya kusafiria mbunge huyo mstaafu wa Chadema.
“Idara inapenda kuufahamisha umma kuwa utaratibu uliotumika kumzuia kutoka nchini ni wa kawaida na unatumika kwa raia yeyote pale idara ikipata taarifa zinazohitaji mhusika kuhojiwa,” taarifa ya uhamiaji inaeleza.
Julai 12, 2025, Brenda ambaye ni Mkurugenzi wa Mawasiliano na Uenezi Chadema, akiwa mpaka wa Namanga akielekea Kenya alikamatwa kwa madai kuwa ana kesi ya uchochezi.
Msemaji wa Jeshi la Polisi David Misime kupitia taarifa yake kwa umma aliyoitoa Julai, mwaka huu alithibitisha kukamatwa kwake kwa mahojiano.
“Jeshi la Polisi lingependa kutoa taarifa kuwa, limemkamata Brenda Rupia kwa ajili ya mahojiano kutokana na tuhuma zinazomkabili za kutoa taarifa za uongo na uchochezi, baada ya mahojiano taratibu zingine kwa mujibu wa sheria za nchi zitafuata.”
Siku hiyo hiyo Chadema ilieleza kuwa, Mtaalamu wa Rasilimali, Miradi na Uwekezaji, Leonard Magere naye alishikiliwa na Idara ya Uhamiaji Uwanja wa Kimataifa wa Julias Nyerere (JNIA), akijiandaa kuelekea nchini Uingereza.
Katika tukio la Heche, itakumbukwa Mwenyekiti wa Chadema, Tundu Lissu Oktoba 17, 2025 akiwa kizimbani Mahakama Kuu jijini Dar es Salaam, aliwataka viongozi wenzake wa chama hicho kuhakikisha wanahudhuria mazishi ya Waziri Mkuu wa zamani wa Kenya, Odinga aliyefariki dunia hivi karibuni nchini India na maziko yake yanafanyika leo nchini kwake.