MAHAKAMA Kuu Masijala Ndogo ya Dar es Salaam kesho, Oktoba 20,0225 inatarajia kusikiliza hoja za upande wa Jamhuri juu ya mapingamizi yaliyowasilishwa na Mwenyekiti wa Chama chaDemokrasianaMaendeleo (CHADEMA), Tundu Lissu, kuhusu kupokelewa kwa vielelezo vya shahidi wa tatu katika kesi ya uhaini inayomkabili.
Shahidi huyo ni mtaalamu wa uchunguzi wa masuala ya picha mjongea na mnato aliyejitambulisha kuwa ni Mkaguzi wa Jeshi la Polisi kutoka Kitengo cha Picha Kamisheni ya Uchunguzi wa Sayansi Jinai Makao Makuu Dar es salaam, Samwel Kaaya (39).
Hatua hiyo inakuja kufuatia shahidi huyo aliyekuwa akiongozwa na Wakili wa serikali Mwandamizi Thawabu Issa kueleza mbele ya jopo la majaji watatu wakiongozwa na Jaji Dunstan Ndunguru akisaidizana na Jaji James Karayemaha na Ferdinand Kiwonde
namna alivyofanya uchunguzi na kubaini picha mjongeo yenye maudhui ya Lissu yanayodaiwa kuwa ni jinai ilikuwa ni halisi na si ya kupandikizwa.
Baada ya ushahadi wa siku mbili, shahidi akiongozwa na Wakili wa Serikali Mwandamizi, Tawabu Issah aliiomba mahakama kupokea vielelezo alivyopeleka ikiwemo flashi diski, kadi ya kumbukumbu na taarifa ya uchunguzi, kama sehemu ya ushahidi wa msingi katika kesi hiyo.
Lissu alipinga hoja hiyo akidai kuwa na sababu nne ya kwanza alidai kuwa vielelezo hivyo havikuonyeshwa katika Mahakama Kabidhi ambayo ni Mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu kwa mujibu wa kifungu cha 263(2) cha CPA.
Alidai mshitakiwa anapopelekwa katika mahakama ya ukabidhi anasomewa maelezo ya mashahidi na kutolewa nyaraka za ushahidi ambazo DPP anatazamia kuzitoa kama sehemu ya ushahidi, alidai shahidi namba moja hadi 30 maelezo yote waliambatanisha.
Alidai pia yalisomwa Kisutu na vielelezo tisa vya nyaraka viliorodheshwa, lakini havikusomwa na vielelezo halisi ambavyo ni flashi diski na kadi ya kumbukumbu havikuonyeshwa wakati wakisoma maelezo ya mashahidi Kisutu.
Sababu ya pili ni kwamba vitu hivyo vimepelekwa kabla ya wakati wake, na kwamba aliyepeleka vitu hivyo si shahidi wa kawaida ambao walirekodi maudhui hayo na si mtaalamu aliyefanya uchunguzi juu ya hivyo vitu, alidai alitakiwa kuwasilisha ripoti kwanza.
Lissu alidai shahidi huyo hakuwa na sifa ya kupeleka kielelezo hiko mahakamani kwa sababu kwa mujibu wa gazeti la serikali alilodai kupewa mamlaka ya uchunguzi ilikuwa ni uchunguzi wa picha za mnato na si za mjongeo, hivyo hana utaalamu aliouleleza mahakamani.
Pia Lissu alidai kuwa shahidi hajafuata mnyororo wa matukio kwamba alisema alipokea kielelezo kutoka kwa Mkaguzi Msaidizi, Michael Gyumi lakini hajaeleza kuwa huyo aliyempatia alikitoa wapi, kwani hakutaja mnyororo uliolezwa na mashahidi wengine waliopita.
Hivyo, aliiomba mahakama isipokee vielelezo hivyo kwa sababu alizoziainisha.
Kesi hiyo itaendelea kesho saa tatu asubuhi. Mshtakiwa yuko rumande