Huzuni yatanda Raila Odinga akizikwa leo Jumapili

Dar es Salaam. Mwili wa aliyekuwa Waziri Mkuu wa Kenya, Raila Odinga aliyefariki dunia nchini India unatarajiwa kuzikwa nyumbani kwa baba yake leo Jumapili, Oktoba 19 huko eneo la Bunge la Bondo, Kaunti ya Siaya.

Maelfu ya waombolezaji wamemiminika katika Chuo Kikuu cha Sayansi na Teknolojia cha Jaramogi Oginga Odinga ambapo hafla ya maziko inafanyika. Kisha atazikwa katika eneo hilo ambalo baba yake alizikwa.

Odinga alifariki Jumatano, Oktoba 15, alipokuwa akipatiwa matibabu katika hospitalini huko Kerala, India.

Kifo chake kilifanya maelfu ya Wakenya kujitokeza barabarani kuomboleza msiba huo hali iliyopelekea vurugu katika Uwanja wa Kasarani huku wengine wakiomboleza katika barabara za miji kama Nairobi.

Mapema leo viongozi mbalimbali, familia ya marehemu wameendelea kutoa heshima zao za mwisho ikiwa ni kuelekea maziko ya kiongozi huyo kipenzi cha Wakenya.

Mkewe, Ida Odinga, watoto , Rosemary, Raila Junior na Winnie   wameonekana kuwa na wakati mgumu katika kipindi hiki wakishiriki kumzika mpendwa wao.

Rais wa Kenya, William Ruto, Rais mstaafu Uhuru Kenyatta tayari  wamewasili pamoja na Rais wa zamani wa Nigeria Olusegun Obasanjo.

Endelea kufuatilia Mwananchi kwa taarifa zaidi.