KIONGOZI UVCCM TAIFA APANDA BASI KUOMBA KURA ZA SAMIA,LUTANDULA

Mgombea Ubunge wa Jimbo la Chato kusini, Paschal Lutandula, akishuka kwenye basi baada ya kumaliza kuomba kura za CCM

Naibu Katibu mkuu wa UVCCM Bara,Mussa Mwakitinya, akiomba kura za CCM stendi ya Bwanga Chato

………………………..

CHATO

NAIBU Katibu mkuu wa Umoja wa Vijana wa Chama Cha Mapinduzi (UVCCM) Tanzania Bara, Mussa Mwakitinya pamoja na Mgombea Ubunge wa Jimbo la Chato kusini kwa tiketi ya Chama hicho,Paschal Lutandula, wamelazimika kupanda kwenye mabasi ya usafirishaji kwaajili ya kuomba kura za Chama hicho ifikapo Oktoba 29 mwaka huu.

Mbali na hilo, wamewatembelea wafanyabiashara mbalimbali kwenye soko kuu la mji wa Bwanga kwa lengo la kuwasisitiza kujitokeza kupiga kura kwenye Uchaguzi mkuu wa Rais,Wabunge na Madiwani nchini.

Baadhi ya waliofikiwa ni wauza nafaka, samaki, ndizi, vinyozi, mitumba, wasusi, pamoja na wauza kahawa kabla ya kuelekea kwenye stendi ya mabasi Bwanga.

Awali akiwa katika soko hilo, Mwakitinya ametoa elimu ya mpiga kura na kuwataka kukichagua Chama Cha Mapinduzi (CCM) ili kiendelee kuleta maendeleo,amani, utulivu na mshikamano.

Kadhalika amesisitiza kuwa serikali ya CCM itaendelea kutoa mikopo ya Wanawake, Vijana na watu wenye ulemavu, mikopo ya elimu ya juu, sambamba na kuboresha sektabya afya,maji, kilimo, uvuvi, uchimbaji madini, uhifadhi mazingira pamoja na kuinua utalii.

Kwa upande wake Mgombea Ubunge wa Jimbo hilo, Paschal Lutandula, akiwa katika stendi ya mabasi Bwanga akalazimika kupanda ndani ya mabasi ili kumwombea kura Rais Samia.

Amesema Maendeleo yaliyopo nchini yametokana na mifumo mizuri iliyoasisiwa na viongozi wa CCM na kwamba siri kubwa ya maendeleo ni kuendelea kukichagua chama hicho katika Uchaguzi mkuu wa Oktoba mwaka huu.

Amesema miundombinu ya barabara imeboreshwa na kuwavutia wawekezaji wengi kushiriki kwenye sekta hiyo ikiwa ni pamoja na vijana wengi kujiajiri kupitia sekta ya usafirishaji wa pikipiki (bodaboda). 

Pia Lutandula, amewataka wananchi wa Bwanga na Buziku kuwachagua wagombea wa Chama hicho (mafiga matatu) ili washirikiane kutatua changamoto za jamii, kuimalisha amani na utulivu ulioasisiwa na Hayati Baba wa Taifa Mwl. Julius Kambarage Nyerere.

                          Mwisho.