Tabora. Mgombea wa ubunge wa Jimbo la Bukene, Wilaya ya Nzega mkoani Tabora kwa tiketi ya Chama cha Mapinduzi (CCM), John Luhende ameahidi kuhakikisha vitongoji 30 ambavyo bado havijafikiwa na huduma ya umeme, vinaunganishwa mara atakapochaguliwa kuwa mbunge.
Luhende ametoa ahadi hiyo leo Jumapili Oktoba 19, 2025 wakati akinadi sera za chama hicho katika mkutano wa kampeni uliofanyika kijijini Shigamba, Kata ya Shigamba, jimboni Bukene.
“Mkinichagua nitahakikisha umeme unawafikia wananchi wote wa Bukene. Tunajua vimebaki vitongoji 30 tu, niseme tu kwamba umeme utawaka ndugu zangu,” amesema Luhende.
Amesema katika utekelezaji wa Ilani ya CCM, zahanati zitajengwa kwenye kata mbalimbali ikiwemo Shigamba, zikiwa na vifaatiba vya kisasa, dawa za kutosha na watoa huduma wa afya, ili kuhakikisha wananchi wanapata matibabu bora.

Wananchi wa kijiji cha Shigamba jimbo la Bukene wakisikiliza sera za mgombea ubunge wa jimbo hilo John Stephano Luhende. Picha na Hawa Kimwaga
“Zahanati zitajengwa Bukene, na huduma zitakuwa bora bila changamoto yoyote. Hatuwezi kuzungumzia maendeleo bila afya bora,” amesema.
Kuhusu sekta ya kilimo, Luhende ameahidi kuwa atahakikisha wakulima wanaunganishwa na kampuni zitakazowakopesha matrekta ili kuongeza tija katika uzalishaji.
Aidha, amesema maofisa ugani watatoa vyeti kwa wakulima vitakavyobainisha mazao yanayofaa kulimwa kulingana na aina ya udongo wa maeneo husika.
“Kilimo ni uti wa mgongo wa uchumi wetu. Tunapaswa kulima kwa tija ili kujihakikishia mavuno na kipato bora,” amesisitiza.

Mjumbe wa halmashauri kuu ya chama cha mapinduzi CCM taifa Mohamedi Nassoro Hamdani akizungumza katika mkutano wa kampeni za chama cha mapinduzi CCM katika kata ya Shigamba jimbo la Bukene wilaya ya Nzega mkoani Tabora.Picha na Hawa Kimwaga
Kwa upande wake, Mjumbe wa Halmashauri Kuu ya Taifa ya CCM, Mohamed Nassoro Hamdani amesema chama hicho ni imara na kimeweka wagombea wenye uwezo wa kuleta maendeleo, wakiwemo vijana kama Luhende.
“Msihofu, mgombea huyu ni kijana mwenye nguvu na uwezo wa kushirikiana na serikali kuhakikisha mahitaji muhimu na maendeleo kwa wananchi wa Bukene yanapatikana,” amesema Hamdani.
Naye mgombea wa udiwani wa Kata ya Shigamba, Aron Shija amesema maendeleo makubwa yaliyofanywa na CCM yanaonekana wazi, hivyo wananchi wanapaswa kukipa tena ridhaa chama hicho ili kiendelee kutekeleza miradi ya maendeleo.
“Chama cha Mapinduzi kimeleta maendeleo makubwa. Barabara zimejengwa, vituo vya afya vimeboreshwa na sekta ya elimu imeimarika, madarasa mengi yamejengwa na ada kwa wanafunzi imeondolewa,” amesema Shija.
Catherine Ndoda, mkazi wa Kata ya Shigamba, ameomba kipaumbele kiwekwe katika sekta ya afya kutokana na ongezeko la watu katika eneo hilo.
“Zahanati tuliyonayo ni ndogo mno. Tunamuomba mbunge atakayechaguliwa ahakikishe inapanuliwa na kuongezewa watoa huduma,” amesema Ndoda.
Naye Shilaja Masanja amemtaka mgombea huyo endapo atapatiwa ridhaa, ahakikishe anaboresha miundombinu ya barabara ili kurahisisha usafirishaji wa mazao na huduma za kijamii.
“Barabara ni muhimu kwa uchumi wetu. Tunalipa kodi, hivyo tunahitaji barabara nzuri zinazopitika mwaka mzima,” amesema Masanja.