MAHUBIRI: Bwana Yesu anakuja kuchukua kanisa lake

Ukiangalia kichwa cha somo hapo unaweza usielewe lakini ndio programu ya mwisho ya Mungu itakayotokea katika kizazi hiki. Mimi na wewe tupo enzi ya mwisho ya kanisa.

Bwana Yesu anakuja kuwachukua watakatifu wake waliopo duniani, duniani wenye haki na wenye dhambi wapo sehemu moja lakini wakati wa unyakuo wenye haki ndio wataondolewa na waovu wataenda kuingia katika dhiki kuu.

Biblia inasema Matendo ya Mitume 1:11 “Wakasema, Enyi watu wa Galilaya, mbona mmesimama mkitazama mbinguni? Huyu Yesu aliyechukuliwa kutoka kwenu kwenda juu mbinguni, atakuja jinsi hiyo hiyo mlivyomwona akienda zake mbinguni.”

Hii ahadi inaenda kutimizwa katika kizazi hiki.

Suala la unyakuo ni suala la maandalizi. Bwana Yesu anachukia dhambi, Tujiandae kwa maisha ya toba, tukiri dhambi zetu na kuziacha na kubadili mitazamo yetu na kurudi kwa Mungu.

Biblia inasema   Luka 21:34 Basi, jiangalieni, mioyo yenu isije ikalemewa na ulafi, na ulevi, na masumbufu ya maisha haya; siku ile ikawajia ghafla, kama mtego unasavyo.” .  

Hii siku ambayo Bwana Yesu anakuja kulichukua kanisa lake hakuna anayeijua, hakuna anayeweza kutabiri siku, mwaka au mwezi lakini tumeambiwa kuna dalili tukiziona tunapaswa kuwa makini na kujua unyakuo upo mlangoni Mathayo 24:3-15 , [3] Hata alipokuwa ameketi katika mlima wa Mizeituni, wanafunzi wake wakamwendea kwa faragha, wakisema, tuambie, mambo hayo yatakuwa lini?

Nayo ni nini dalili ya kuja kwako, na ya mwisho wa dunia? [4]Yesu akajibu, akawaambia, Angalieni, mtu asiwadanganye. .[5]Kwa sababu wengi watakuja kwa jina langu, wakisema, Mimi ni Kristo; nao watadanganya wengi. [6]Nanyi mtasikia habari za vita na matetesi ya vita; angalieni, msitishwe; maana hayo hayana budi kutukia; lakini ule mwisho bado. [7]Kwa maana taifa litaondoka kupigana na taifa, na ufalme kupigana na ufalme; kutakuwa na njaa, na matetemeko ya nchi mahali mahali. [8]Hayo yote ndiyo mwanzo wa utungu. [9]Wakati huo watawasaliti ninyi mpate dhiki, nao watawaua; nanyi mtakuwa watu wa kuchukiwa na mataifa yote kwa ajili ya jina langu. [10]Ndipo wengi watakapojikwaa, nao watasalitiana, na kuchukiana. [11]Na manabii wengi wa uongo watatokea, na kudanganya wengi. [12]Na kwa sababu ya kuongezeka maasi, upendo wa wengi utapoa. [13]Lakini mwenye kuvumilia hata mwisho, ndiye atakayeokoka. [14]Tena habari njema ya ufalme itahubiriwa katika ulimwengu wote, kuwa ushuhuda kwa mataifa yote; hapo ndipo ule mwisho utakapokuja.

Ukisoma Biblia dalili ni hizi, uwepo wa mitume na manabii wa uongo, uwepo wa vita baina ya mataifa na mataifa, uwepo njaa na matetemeko ya nchi, usaliti ndani ya Wakristo na matengano, uwepo wa maasi makubwa katika jamii, uamsho wa injili watu kumjua Bwana Yesu. ukiangalia unaona dalili zote zimetimia. Kwenye runinga, redio, mtandaoni unaona mambo haya. Je, umejiandaaje? Dalili zote zimetimia tupo dakika za nyongeza.

Bwana Yesu anatuagiza tutubu Biblia inasema Matendo ya Mitume 17:30 “Basi, zamani zile za ujinga Mungu alijifanya kama hazioni; bali sasa anawaagiza watu wote wa kila mahali watubu.”

Tubu dhambi zako leo, kesho ni fumbo yamkini kifo kikakutembelea. Hatujui siku au saa atakayokuja mwokozi wetu lakini dalili zinaonesha yupo mlangoni kwa sababu dalili zote zimetimia katika taifa letu na mataifa yetu ukiangalia taarifa mbalimbali za ulimwengu.

Pia Biblia inatuambia habari za watu wa siku za mwisho 2 Timotheo 3:1-5 [1]Lakini ufahamu neno hili, ya kuwa siku za mwisho kutakuwako nyakati za hatari. [2]Maana watu watakuwa wenye kujipenda wenyewe, wenye kupenda fedha, wenye kujisifu, wenye kiburi, wenye kutukana, wasiotii wazazi wao, wasio na shukrani, wasio safi, [3]wasiowapenda wa kwao, wasiotaka kufanya suluhu, wasingiziaji, wasiojizuia, wakali, wasiopenda mema, [4]wasaliti, wakaidi, wenye kujivuna, wapendao anasa kuliko kumpenda Mungu; [5]wenye mfano wa utauwa, lakini wakikana nguvu zake; hao nao ujiepushe nao.

Hapa tunaona Biblia inataja watu wa siku za mwisho. Je hawa watu hawapo kwenye jamii zetu mfano makazini,shuleni na kanisani pia. Hawa watu wapo kwa hiyo hili andiko limetimia tayari lakini watu bado hawajajiandaa na unyakuo.

Maandiko yote yanayoonesha siku za mwisho yametimia tayari kwa sababu hizo ishara tunaziona.

Katika maandiko haya yote niliyokupitisha yamekwishatimia tayari, tunapaswa kufanya nini katika majira haya?  Biblia inasema Matendo 2:37 “37 waliposikia haya wakachomwa mioyo yao, wakwambia Petro na mitume wengine, tutendeje ndugu zetu? 38 Petro akawaambia tubuni mkabatizwe kila mmoja kwa jina lake Yesu Kristo, mpate ondoleo la dhambi, nanyi mtapokea kipawa cha Roho Mtakatifu”.

Hapa tunaona watu wanaagizwa watubu na Mtume Petro vilevile Mtume Paulo aliagiza watu watubu. Kwa hiyo ukitaka ujiandae vizuri na unyakuo unapaswa kuwa mtu wa kutubu, kuwa na maisha ya kutubu.

Kutubu maana yake ni kukiri kwa kinywa chako makosa yako mbele za Mungu na unabadilisha mtazamo wako na mitindo yako ya maisha na unarudi kwa Mungu.

Unapotubu wewe ni mvuta sigara hakikisha unaacha kuvuta sigara, ukiwa una mali za watu za wivi unazirudisha na unakuwa mtu wa ibada na kumpendeza Mungu.