Mapigano kwenye ndoa sawa na uhayawani

Canada. Kuna usemi maarufu kuwa mke hapigwi kwa kofi bali kwa upande wa khanga/kitenge. Pia, upo ule wa mke ni pambo la nyumba.

Nani anaweza kuharibu pambo la nyumbani kwake akatenda haki au kuwa timamu na mzima kiakili?

Wanyama ni viumbe wanaosifika kwa mapigano wakigombea majike, milki, hata vyakula. Hii hutokana na kuwa na uwezo mdogo wa kufikiri namna ya kutatua matatizo yao. Ni mahayawani.

Inakuwaje binadamu japo si wote mnashindwa kutatua tofauti zenu hadi muumizane kwa ngumi na mateke hata kuuana mkihusisha na kuathiri hata wasio na hatia?

Wanaofanya hivi wana tofauti gani na hayawani? Hupata faida au burdani gani? Hujenga taswira gani? Leo, tutaongelea aibu jinai, na kadhia ya mapigano kwenye ndoa.

Waathirika wengi wa kadhia hii ni wanawake. Kabla ya kufikiria, achilia mbali kuamua, kumpiga mkeo, jiulize. Ungekuwa ndiye yeye, ungejisikiaje au kufanyaje? Unajua madhara ya kitendo hiki kwake na watoto wenu mbali nawe?

Upigaji, licha ya kuwa uhayawani na ukatili, ni kielelezo cha changamoto ya akili, ubinafsi uliopitiliza, uhayawani, uwezo mdogo wa kufikiri, ukatili, unyanyasaji/ushamba, na ujinga wa hali ya juu. Kabla ya kumpiga mwenzio, kumbuka mkuki kwa nguruwe, kwa mja mchungu.

Japo waathirika wengi wa kadhia hii ni wanawake, siku hizi, hata wanaume ‘wanaundwa’ kama wasemavyo Wakenya au wanadundwa na wake zao.

Tunapinga jinai hii. Kwa mujibu wa gazeti la kila siku la The Standard (2022), kumekuwapo na ongezeko na kujiua au kuua kwa sumu nchini Kenya hasa kwa kinababa wanaopigwa na wake zao au kinamama wanaopigwa na waume zao.

Kupiga ni ukatili na unyama bila kujali jinsi ya mwathirika. Ni udhalilishaji licha ya kuwa unyama na utaahira. Unapompiga mwenzio, unamdhalilisha na kujidhalilisha hata watoto wenu.

Pia, unafundisha tabia mbaya kwao kutokana na ukweli wa kisayansi kuwa watoto huiga tabia za wazazi wao. Japo, wapo wanaokulia kwenye familia hatarishi zilizojaa mapigano na udhalilishaji wanaochukia jinai hii, uwezekano wa watoto kuchukua tabia hii ni mkubwa.

Hamjasikia watoto wadogo, wanapoudhiwa au kunyimwa kitu na mama yao wakisema ‘ndiyo maana baba anakupiga au baba akija nitamwambia?’ Ili iweje? Japo watoto hawasemi, wapo wanaowachukia wazazi wao wapigaji kiasi cha kukua na kuwatenza vibaya.

Hivyo, unapompiga mwenzio, unajiandalia wewe na mwenzio uzee mbaya. Maana, vipigo havimjengi kiakili wala kimwili bali kumbomoa. Matokeo yake hujitokeza na kuonekana wakati wa uzee.

Hivyo, wapigaji wajue japo wanajiridhisha kuwa wanawaadhibu wanaowapiga, wanajiadhibu bila kujua. Wanajionyesha kama watu wa ovyo na katili mbele ya jamii hasa watoto wao.

Pia, wanatengeneza chuki ambapo baadhi ya waathirika hulipiza kisasi.

Kuna kisa cha baba aliyekuwa akimpiga mkewe mara kwa mara aliyepata ajali akawa kiwete. Alikimbizwa hospitali alikokaa kwa miezi kadhaa. Mkewe alimuuguza hadi akapona na kurejea nyumbani.

Baada ya kurejea nyumbani, mkewe alilipua bomu. Alimwambia kuwa alikuwa anaondoka. Mume, kwa masikitiko na mshangao, alimuuliza anakwenda wapi na kwanini anafanya hivyo.

Mama alimjibu kuwa ulikuwa wakati wa kulipiza kisasi kutokana na vipigo alivyokuwa amempa. Baba alilia na kuomba msamaha. Mama hakumsikiliza zaidi ya kufunga virago na kutimka. Japo hatuungi mkono uamuzi wa mama, ni ushahidi kuwa ukipanda miba, unavuna miba.

Tumalizie. Acha kumpiga mwenza wako. Hupati faida bali hasara. Licha ya kujisababishia mateso, unawasababishia wengine pia.

Waathirika wana akili timamu. Wanaweza kuwa na hasira hata visasi kama visa vya kupeana sumu hapo juu vinavyoonyesha. Japo hatuungi mkono jinai hii itokanayo na jinai nyingine, tunajua kuwa penye udhalilishaji lazima pawe na ukombozi. Na ukombozi mwingine unaweza kufanywa kikatili.

Kwa sababu, ukishamdhalilisha mwathirika, huwa humuoni kama binadamu. Naye kadhalika, anakuona kama mnyama ambaye akimuua, haui binadamu bali mnyama. Kwanini kufikishana hapa wakati mlikutanishwa na upendo?

Kimsingi, unapompiga mwenzio, unajipiga mwenyewe bila kujua.Nani mpumbavu huyu ajipigaye akidhani anampiga mwingine. Tunashauri isiwe wewe, kwani wewe si taahira wala hayawani.