Masomo ya dini yatajwa msingi wa maadili, amani ya Taifa

Dar es Salaam. Kamishina wa Elimu katika Wizara ya Elimu, Sayansi na Teknolojia, Dk Lyabwene Mtahabwa, ameahidi kuchukua hatua kuhusu suala la ufaulu wa masomo ya dini kama kipengele cha kujiunga na vyuo vya kati na juu.

Dk Mtahabwa amesema kwamba masomo ya dini, kama vile Islamic Studies na Bible Knowledge, ni muhimu kwa jamii na yanapaswa kuzingatiwa zaidi katika muktadha wa elimu ya juu.

Amezungumza hayo leo Jumapili Oktoba 19, 2025 katika mahafali ya 13 ya kidato cha nne ya Shule za Islamic Development Foundation (IDF), yaliyofanyika katika uwanja wa Ilala Bungoni, jijini Dar es Salaam.

Kamishina wa Elimu Wizara ya Elimu Sayansi na Teknolojia Dk Lyabwene Mtahabwa akizungumza na wanafunzi kwenye mahafari ya 13  kidato cha nne ya Islamic Development Foundation (IDF) yaliofanyika kwenye uwanja wa Ilala Bunngoni jijini Dar es Salaam leo Octoba 19, 2025

Dk Mtahabwa amesema kuwa masomo hayo yamekuwa na manufaa makubwa kwa jamii na yanastahili kupewa umuhimu katika mfumo wa elimu wa kitaifa.

“Masomo ya dini ni msingi wa ujenzi wa jamii bora, walimu waliweka masomo haya kwa nia maalumu, na ni muhimu kuwa na maadili mema ili tuweze kuendelea kuwa jamii yenye maadili na amani,” amesema Dk Mtahabwa.

Dk Mtahabwa amekiri changamoto inayojitokeza kwa baadhi ya wanafunzi ambao wamefaulu masomo ya dini lakini wanakosa nafasi za kuendelea na masomo kutokana na kutotambulika kwa ufaulu wao wa masomo hayo, katika mchakato wa kujiunga na vyuo vya kati.

“Niwaahidi kwamba tutachukua maoni yenu na kuyafanyia kazi ili suala hili liweze kutatuliwa, na elimu yetu iweze kusonga mbele,” amesema Kamishina huyo.

Kwa upande mwingine, Dk Mtahabwa ametoa pongezi kwa wahitimu wa shule hizo na kuwaomba waendelee kuwa watu wema na kujitahidi kuwa na maadili katika maisha yao, huku akiwashauri kuzingatia mambo matatu makuu: elimu, umoja, na utu wema, na kusema kuwa kujikweza hakutawafikisha popote maishani.

Mwenyekiti wa Kamati ya Amani Taifa, Alhadi Musa, amesisitiza umuhimu wa amani katika Taifa akisema kuwa ni jukumu la viongozi wa dini kuhakikisha kwamba amani inazidi kudumishwa.

“Tanzania ni kisiwa cha amani, na tunawahimiza wanafunzi na wananchi kuwa na tabia za kistaarabu na kuacha kushiriki katika vurugu au maandamano,” amesema Musa.

Mwenyekiti wa Kamati ya Amani Taifa Dk Alhadi Musa akizungumza na wanafunzi na wazazi waliojitokeza kwenye mahafari ya (IDF) yaliyofanyika leo kwenye uwanja wa Ilala Bunngoni jijini Dar es Salaam.

Musa amewashauri wahitimu kuwa na maadili mema na kutumia elimu yao kwa faida ya Taifa, akisema kuwa kwa kufanya hivyo, watachangia maendeleo ya nchi.

“Tunahitaji watu wema na waadilifu katika nyanja mbalimbali za kijamii, ili tuweze kuleta maendeleo endelevu,” ameongeza.

Mkurugenzi wa shule hiyo, Issa Buhelo, ameeleza kuwa masomo ya dini, ikiwa ni pamoja na Islamic Studies na Bible Knowledge, yamekuwa kikwazo kwa baadhi ya wanafunzi katika kuendelea na elimu ya juu. Ameitaka Wizara ya Elimu ikabiliane na changamoto hiyo ili wanafunzi wanaofaulu masomo hayo waweze kuendelea na elimu ya juu.

“Dini ni msingi wa amani na umoja wa Taifa hili, na tunaiomba Serikali kutambua umuhimu wa masomo haya katika mchakato wa elimu ya juu,” amesema Buhelo.

Mwalimu Mkuu wa shule hiyo, Bashiri Haji, amezungumzia juhudi zinazofanywa na shule hiyo katika kuwajengea wanafunzi uwezo wa kujimudu baada ya kumaliza masomo yao. Amesema kuwa shule inatoa mafunzo ya kijamii ili wanafunzi waweze kujiajiri na kuwa na nidhamu katika jamii.

Ally Kabambura, mmoja wa wahitimu, amesema: “Tuna furaha kumaliza kidato cha nne, na tunahidi kufanya vyema kwenye mtihani wetu wa mwisho utakaofanyika Novemba mwaka huu.”