Na Said Mwishehe,Michuzi TV- Rukwa
MGOMBEA Urais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania kwa tiketi ya Chama Cha Mapinduzi(CCM) Dk.Samia Suluhu Hassan amewaahidi wakulima wa mahindi mkoani Rukwa kwamba Serikali inaangalia uwezekano wa kuendelea kununua mahindi ya wakulima.
Dk.Samia ametoa ahadi leo Oktoba 19,2025 alipokuwa akizungumza katika mkutano mkubwa wa kampeni uliofanyika Uwanja wa Shule ya Sekondari Kizwite uliopo Sumbawanga Mjini mkoani Rukwa.
“Nipo hapa na Waziri wa Fedha na Waziri wa Kilimo. Najua bajeti tuliyoitoa ya ununuzi wa mahindi tuliimaliza lakini wanasema jungu kuu halikosi ukoko. Sasa Waziri wa Fedha kachungulie katika jungu kuu tuone tutapata kiasi gani tuendelee kununua mahindi.
“Kilichotokea ni kwamba tumetoa mbolea nyingi watu wamezalisha, tumepima udongo, tumeleta mbegu watu wamezalisha kwa wingi. Sasa uzalishaji kwa wingi kutahitajika maghala yawe mengi ili tuweze kuhifadhi na kutahitajika fedha kununua mahindi kwa wakulima tuweze kuyahifadhi.
“Tukiweza kuuza nje tutaweza kuyahifadhi yale ambayo tutayanunua sasa hivi. Niwaombe kapekueni tuone uwezekano tuendelee kununua mahindi kwa wakulima,”amesema Dk.Samia
Kuhusu ombi la shamba la NARCO kugawiwa wakulima wilayani Kalambo, Dk.Samia amesema kwamba suala hilo amelichukua na atakwenda kulifanyiakazi.
Akizungumzia ombi la Waziri Mkuu Mstaafu Mzengo Pinda kuhusu ujenzi wa barabara ya Sumbawanga – Matai – Kasanga amesema imelichukua ombi hilo.