Dar/Chalinze. Katika kijiji kimojawapo wilayani Chalinze, sauti ya kicheko cha Mwanaidi Seleman bibi mwenye umri wa miaka 63 inasikika kwa mbali. Ninaposogea macho yake yanang’aa, na sura yake imejaa tabasamu la furaha.
Kwa miaka mingi, Mwanaidi ambaye pia ni mkunga wa jadi, aliteseka na ugonjwa wa vikope maarufu trakoma.
Jicho lake la kushoto lilikuwa limepoteza uwezo wa kuona, na kila siku alihisi maumivu makali. Watu kijijini walimshauri atafute msaada wa waganga wa kienyeji, wakiamini ugonjwa huo unasababishwa na kuzalisha sana au hata nguvu za giza. Lakini leo, anasimulia kwa furaha:
“Nilikuwa nimekata tamaa, lakini baada ya kupata matibabu kupitia programu ya Serikali, sasa naona vizuri. Mungu ni mwema.”
Nyuma ya tabasamu la Mwanaidi, yupo Margreth Mumbua, Ofisa Tabibu mwenye moyo wa huduma anayejulikana zaidi Wilayani Chalinze kutokana na huduma za afya anazozitoa.
Alimaliza masomo yake katika Chuo cha Mafunzo ya Maofisa Tabibu Mvumi mwaka 2005, na kupokea stashahada ya tiba ya kliniki. Baadaye, alipata mafunzo maalum ya upasuaji wa TT (Trichiasis) kupitia mpango wa Wizara ya Afya wa kukabiliana na trakoma.
Kwa miaka kadhaa sasa, Margreth amekuwa mstari wa mbele katika kutoa huduma za upasuaji mdogo wa macho kwa watu wa vijijini. Anasimulia kuwa kazi hiyo imemjengea faraja na fahari kubwa.
“Ninapowaona wagonjwa wangu wakiona tena, nafurahi mno. Nimebahatika kuwa sehemu ya mabadiliko katika maisha yao,” anasema kwa tabasamu.
Licha ya mafanikio hayo, Margreth anakiri kuwa changamoto kubwa anayokutana nayo ni imani za kishirikina zinazohusishwa na magonjwa ya macho.
“Watu wengi huamini kuwa wazee wanaougua vikope au trakoma ni wachawi. Inachukua muda mwingi kuwaelimisha na kuwajenga imani kuwa ugonjwa huu unatibika,” anasema.
Anasema ilibidi ajifunze hata lugha za wenyeji katika maeneo tofauti ili kuwafikia kirahisi. “Kuelewa lugha zao ilikuwa njia pekee ya kuvunja ukuta wa hofu,” anabainisha.

Lakini si kila siku ni rahisi. Kati ya wagonjwa zaidi ya 200 aliowahudumia kufikia Agosti mwaka 2025, kuna mmoja ambaye kumbukumbu yake haimwachi ‘Emmanuel’, dereva wa daladala kutoka Bagamoyo.
Siku moja, Emmanuel alifika hospitalini akilalamika macho yake kuchoma na kope kumuumiza.
Kilichoongeza hatari ni kwamba alikuwa akiugua ugonjwa wa moyo na alikuwa anatumia dawa zinazofanya damu kuwa nyepesi. Hata hivyo, hali yake ilikuwa mbaya kiasi kwamba alihitaji kufanyiwa upasuaji mara moja.
“Tulijipa moyo. Tulijua ni hatari, lakini pia tulijua anahitaji msaada wa haraka,” anasema Margreth kwa sauti ya upole.
Baada ya upasuaji, Emmanuel aliruhusiwa kurudi nyumbani. Lakini saa chache baadaye, akarejeshwa hospitalini akiwa anatokwa damu jichoni. Walimrudisha kwenye chumba cha huduma, wakamsafisha na kumfunga bandeji upya. Baada ya hali kutulia, aliruhusiwa tena kwa uangalizi maalumu.
Lakini usiku wa Aprili 28, 2025, simu kutoka kwa daktari wa Bagamoyo ilimshtua Margreth.
“Mage… mgonjwa wako ana hali mbaya, jicho linatoa damu isiyokoma.”
Bila kusita, Margreth alijipanga na kusafiri usiku huo kutoka Chalinze hadi Bagamoyo safari ya saa kadhaa. Alipofika saa tano usiku, alimkuta Emmanuel damu ikitiririka hata kwenye kanga aliyofunika uso wake.
“Nilihisi moyo kusimama. Nilijua niko peke yangu, lakini nikajiambia, lazima nimsaidie,” anakumbuka kwa sauti ya kipekee.
Waliendelea na huduma hadi saa 8:30 usiku, ndipo damu ilipoanza kukoma. Walimuweka chini ya uangalizi maalumu, na baada ya siku 14, aliporudi kufungua bandeji, alikuta jicho lake limepona kabisa.
“Nilishusha pumzi kwa nguvu. Nikamshukuru Mungu. Siku hiyo sitaisahau maishani mwangu,” anasema huku akitabasamu.
Kwa Margreth, kazi yake ni zaidi ya taaluma ni wito. Anaamini elimu na uelewa ndivyo vinavyoweza kuokoa macho ya Watanzania wengi zaidi.
“Ukiona hali isiyo ya kawaida kwenye macho yako kwa siku mbili hadi tatu, nenda hospitalini. Usikae nyumbani ukisubiri muujiza,” anasisitiza.
Kazi yake ni ushuhuda kwamba kila jicho linalookolewa ni hadithi mpya ya matumaini na kila mgonjwa anayepata nafuu, ni ushindi dhidi ya giza la imani potofu na upofu unaoweza kuzuilika.
Mwanaidi anasema kabla ya kukutana na Margreth jicho lilimsumbua kwa zaidi ya miaka miwili.
“Siku niliyokwenda hospitali, Mage akanifanyia upasuaji. Alinishona na kunisafisha jicho na kuliziba na plasta akaja akanishughulikia tena, akanitoa nikawa naona na wala sikuchukua hata miezi miwili nimepona kabisa mpaka sasa,” anasimulia.
Mkazi wa Fukayosi, Bagamoyo mkoani Pwani, Rosemary Masanja anasimulia kama mnufaika na kipawa cha Margreth ingawaje alichelewa kubaini kuwa anaugua ugonjwa huo.
Amesema miaka 20 nyuma, alikuwa anafanya kazi lakini ilikuwa inamsumbua, “Walikuja watu wanaandikisha vikope nikawaambia waniandikishe nikapime nijue shida ni nini maana kulikuwa na vitu nasikia vinanichomachoma machoni.”
“Nilivyofika hospitali walivyoniangalia wakasema nina trakoma katika macho yangu yote mawili, kutokana na mateso ya muda mrefu na waliponiambia kwamba natakiwa kufanyiwa upasuaji nilikubali haraka,” anasimulia Rosemary, maarufu Bibi Tito.
Meneja udhibiti wa kutokomeza ugonjwa wa matende namabusha, kutoka Mpango wa Taifa wa kudhibiti magonjwa yasiyopewa kipaumbele (NTDs) Wizara ya Afya, Dk Faraja Lyamuya amesema changamoto kubwa wanayokumbana nayo ni ushiriki wa jamii.
“Maana ili tuweze kutokomeza magonjwa haya jamii inapaswa kushiriki kwa kiasi kikubwa, lengo kubwa la Serikali ni kuikinga jamii,” anasema.
Meneja wa Mpango wa Taifa wa kudhibiti magonjwa yasiyopewa kipaumbele (NTDs) Wizara ya Afya, Dk Clarer Mwansasu anasema zaidi ya wagonjwa 41,000 wamefanyiwa upasuaji tangu mwaka 2014.
Amesema tangu kuanza kwa utekelezaji wa mkakati wa SAFE ulioanza mwaka 1999 katika baadhi ya jamii zilizochaguliwa mwaka 2004 hadi 2012 jamii 69 zilikuwa na wagonjwa wa trachoma hai, halmashauri 84 zilikuwa na wagonjwa wa TT (trachoma trichiasis).
“Hali ya sasa (2025) wilaya 64 zimefanikiwa kufikia vigezo vya kutokomeza ugonjwa huo. Wilaya saba bado zina kiwango cha maambukizi kinachozidi asilimia tano. Idadi ya wagonjwa waliokuwa na TT mwaka 2004 walikuwa 167,000 na mwaka 2023 ni wagonjwa 10,440 katika wilaya 20,” anasema.
Dk Mwansasu anasema zaidi ya watu milioni moja katika halmashauri saba nchini Tanzania wapo kwenye hatari ya kupata maambukizi, changamoto kadhaa zinakwamisha juhudi za kutokomeza ugonjwa huo.
“Trakoma imeathiri zaidi jamii za wafugaji ambao wanahama hama kufuata malisho, unakuta msimu ambao mnamezesha dawa wengine wameenda nchi jirani au mikoa mingine isiyo na ugonjwa kwenda kuchunga mifugo yao.
“Sasa kama walikuwa na vimelea wanarudi tena kuja kuambukiza huku ndugu zao, tulikuwa na mkakati kushirikiana na nchi jirani lakini changamoto kila nchi ina mfadhili tofauti muda mnaotaka kumezesha dawa mwenzako hana dawa na wafugaji wamehamia upande wake,” anasema Dk Mwansasu.
Hata hivyo anasema wamejaribu kutafuta suluhu kwa jumuisha jamii husika hasa wafugaji, “Tunakaa na kujadiliana nao ni msimu upi wanafikiri utafaa zaidi kumezesha dawa, wanatuelekeza.”