Katikati ni MNEC,Mussa Mwakitinya,Kushoto akiwa ni mgombea Ubunge Jimbo la Chato kusini,Paschal Lutandula, na kulia mwenyekiti wa UVCCM wilaya ya Chato
:::::::::
MJUMBE wa halmashauri kuu ya CCM Taifa, Mussa Mwakitinya, amewahimiza wazee kuwahamasisha vijana wao kuendelea kukipenda CCM na kwamba busara zao ni kubwa katika kuielimisha jamii umuhimu wa amani kwa Taifa.
Amesema yapo mataifa mengi ambayo yanafuatilia uchaguzi mkuu wa Rais, Wabunge na Madiwani na kwamba ipo haja kubwa ya wazee kuendelea kusimama misingi mizuri ya Chama hicho.
Mwakitinya ambaye pia ni Naibu Katibu mkuu wa UVCCM Tanzania Bara, amesema hayo wakati akizungumza na wazee wa Jimbo la Chato kusini, huku akiwasisitiza kuendelea kuielimisha jamii.
Mwenyekiti wa Baraza la wazee wilaya ya Chato, Deograthias George, amesema wao kama wazee wameendelea kukemea mambo maovu yanayojitokeza katika jamii na kwamba wapo mstari wa mbele kumtetea mgombea wa urais kwa tiketi ya CCM,Dkt. Samia Suluhu Hassan, kutokana na mambo makubwa aliyoyatekeleza katika kipindi chake cha utawala.
Aidha amewataka wazee wengine katika wilaya hiyo kila mmoja kutimiza wajibu wake na kujiepusha na propaganda za mitandaoni zinazoenezwa kwa lengo la kupotosha jamii kutokana na maslahi yao binafsi.
“Niwasihi sana wazee wenzangu tuendelee kukemea maovu yote yenye lengo la kutundolea amani na utulivu tulionao, hatupendi kuona nchi yetu inaingia kwenye machafuko kama yaliyowahi kutokea kwa baadhi ya nchi” amesema.
Vilevile George ametumia fursa hiyo kumshukuru sana Dkt. Samia kwa moyo wake wa upendo kwa makundi yote ikiwemo wazee, na kwamba wapo tayali Oktoba 29, mwaka huu kumchagua kwa kura za kishindo.
Kwa Upande wake Katibu wa UVCCM Mkoa wa Geita, Abel Shamakala, amemshukuru Mwakitinya kufika mkoani humo na kuzungumza na viongozi mbalimbali wa CCM pamoja na wazee maarufu wa Jimbo la Chato Kusini kwa lengo la kuongeza hamasa ya kuwachagua wagombea wanaotokana na Chama hicho.
“Nikushukuru sana MNEC kwa kazi kubwa uliyoionyesha kwenye Jimbo letu la Chato kusini, lakini pia nikushukuru sana mwenyekiti wa Baraza la wazee wa wilaya ya Chato kwa kukiunga mkono CCM na kuendelea kusimamia maadili ya vijana wetu, kwa niaba yao ninapokea changamoto zote na nikuhakikishie kuwa tutaendelea kuzungumza nao kwa maana wabovu ni wachache sana” amesema Shamakala.
Jimbo la Chato Kusini ni miongoni mwa majimbo mapya nane yaliyoidhinishwa na Tume huru ya taifa ya Uchaguzi (INEC) na kwamba Oktoba 29 mwaka huu ndiyo utakuwa Uchaguzi mkubwa wa kwanza tangu kuundwa kwa Jimbo hilo.
Mwisho.