Mwalimu: Mkinipeleka Ikulu, waziri mkuu wangu ni Kigaila

Dar es Salaam. Mgombea urais kupitia Chama cha Ukombozi wa Umma (Chaumma), Salum Mwalimu, amesema endapo atachaguliwa kuwa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, atamteua Benson Kigaila kuwa Waziri Mkuu wake.

Mwalimu ametoa kauli hiyo leo Jumapili Oktoba 19, 2025, katika mkutano wa kampeni za kunadi sera za chama hicho uliofanyika katika Soko la Kivule, jijini Dar es Salaam.

“Naombeni wananchi wa Kivule muende na Kigaila akatetee haki zenu, kwani hakuna mwingine anayeweza kusimamia changamoto zenu kama yeye. Nimefanya naye kazi, namjua vyema ni mchapakazi, mwenye hadhi na heshima kubwa nchini.

Akiwa waziri mkuu, hakuna mkuu wa mkoa, wilaya au ntendaji atakayemdanganya, maana ni mzee wa ‘pori kwa pori’, anaijua Tanzania na anawajua Watanzania,” amesema Mwalimu, ambaye pia ni Katibu Mkuu wa Chaumma.

Mwalimu amesema matatizo yanayowakabili Watanzania hayajatokea kwa bahati mbaya wala kwa sababu za kimaumbile, bali ni matokeo ya mfumo wa utawala wa chama tawala ambacho kimepoteza dira.

“Chama hicho kimefika ukingoni, kimeishiwa pumzi. Wanaendelea kuwepo madarakani kwa mazoea tu, si kwa uwezo wa kuleta mabadiliko. Msitegemee mabadiliko kutoka kwao zaidi ya kuendelea kuishi katika mfumo wa ‘afadhali ya jana,” amesema.

Akitaja vipaumbele vyake iwapo atachaguliwa kuwa Rais, Mwalimu amesema atapambana na tatizo la ajira na ukali wa maisha.

Amesema tatizo la ajira limekuwa kubwa, kwa sababu hata vijana waliomaliza shule au waliostaafu wanakimbilia kazi ya bodaboda, hali inayodhihirisha ukosefu wa ajira rasmi.

“Kama hali hii ikiendelea, tutafika mahali ambapo idadi ya bodaboda itazidi abiria. Ni lazima tubadilishe mwelekeo huu kwa kuanzisha viwanda, kuboresha miundombinu na kuwezesha wakulima kuuza mazao yao kwa bei nafuu kupitia usafirishaji rahisi,” amesema Mwalimu.

Kuhusu ukali wa maisha, amesema ni aibu kwa nchi yenye ardhi kubwa na yenye rutuba wananchi wake kushindwa kupata mlo mmoja kwa siku.

Ameahidi kuboresha kilimo na kuhakikisha mazao yanachakatwa ndani ya nchi ili kuongeza thamani na ajira.

Kigaila ataja changamoto za Kivule

Mgombea ubunge wa Jimbo la Kivule, Benson Kigaila

amesema jimbo hilo lenye kata sita na mitaa 76 linakabiliwa na changamoto nyingi, ikiwemo miundombinu ya barabara, ukosefu wa mikopo nafuu, ukosefu wa walimu, na uhaba wa huduma za afya.

Amesema mvua zinaponyesha, wakazi wa maeneo mengi hulazimika kushika viatu mikononi ili kuvuka matope, jambo linaloongeza gharama za usafiri.

“Mahali ambapo nauli ilikuwa Sh500, sasa inalipwa Sh1,000, na yenye Sh1,000 imepanda hadi Sh2,000 au Sh3,000,” amesema Kigaila.

Amesema shule nyingi hazina miundombinu bora, watoto wanakaa juu ya matofali na wazazi wanalazimika kuchangia fedha nyingi kwa ajili ya chakula na walimu wa ziada.

“Mfano, mzazi mwenye mtoto mmoja analazimika kutoa Sh3,000 kwa mwezi, na mwenye watoto watatu analipa Sh9,000 — jambo linalowapa mzigo mkubwa,” amesema Kigaila.

Ameongeza kuwa mfumo wa mikopo hauwatendei haki wananchi, kwani wanatakiwa kuunda vikundi na hata kulipia uandikishaji wa katiba, lakini mwisho wa siku mikopo hutolewa kwa upendeleo.

“Hii imewafanya akinamama na vijana kukimbilia mikopo ya ‘kausha damu’. Wakishindwa kulipa, wananyang’anywa mali zao kama vitanda, magodoro na hata vyombo, hali inayosababisha kuvunjika kwa ndoa nyingi. Hii haitakuwepo chini ya uongozi wetu,” amesema Kigaila.

Kuhusu afya, Kigaila amesema hospitali zimegeuka kuwa sehemu za biashara, ambapo wagonjwa huandikiwa dawa wanunue madukani.

“Mbaya zaidi, hata mtu akifiwa, familia inalazimika kulipia maiti ili iondolewe hospitalini. Ikiwa imechelewa kuchukuliwa, ada inaongezeka kama vile mtu amelala hotelini,” amesema.

Amesisitiza chini ya uongozi wa Chaumma, huduma hizo zitarudishwa kwa wananchi ili haki ya msingi ya kuishi na kuhudumiwa isibaki kwa wachache wenye uwezo.