Namna ya kushughulikia hofu,wasiwasi kwa watoto wadogo

Dar es Salaam. Kushughulikia hofu na wasiwasi kwa watoto ni safari inayohitaji uvumilivu, upendo na uelewa.

Watoto wanapopata usalama wa kihisia kutoka kwa wazazi wao, hujenga misingi imara ya kujiamini na uwezo wa kukabiliana na changamoto za maisha wakiwa watu wazima.

Mzazi anayechukua muda kusikiliza, kueleza na kuonyesha mfano wa utulivu, humsaidia mtoto wake si tu kushinda hofu za utotoni, bali pia kuwa na uthabiti wa kihisia katika maisha yake yote.

Tunaelezwa na wataalamu wa saikolojia na malezi kuwa, hofu na wasiwasi ni sehemu ya kawaida ya ukuaji wa mtoto.

Wanasema kila mtoto katika hatua fulani ya maisha yake, hupitia kipindi cha kuogopa vitu fulani, iwe ni giza, wanyama, wageni, au hata kujitenga na wazazi.

Ingawa kwa mtu mzima hofu hizi huonekana kuwa ndogo au zisizo na maana, kwa mtoto wanaziona kama halisi na kubwa sana.

Lakini kuelewa chanzo cha hofu na namna ya kumsaidia mtoto kukabiliana nayo, mtaalamu wa Saikolojia Freddy Mtweve anasema  ni jukumu la mzazi au mlezi kuhakikisha mtoto anakua katika mazingira salama na yenye afya ya kihisia.

Anasema watoto hupata hofu kutokana na mambo mbalimbali, yakihusiana na umri na hatua ya ukuaji wake.

Mtaalamu huyo anasema watoto wachanga mara nyingi huogopa sauti kubwa au watu asio wafahamu.

Lakini kadiri wanavyokua, hofu zao hubadilika na kuhusiana zaidi na mambo ya kufikirika au uzoefu waliopata.

“Kwa mfano, mtoto mwenye umri wa miaka miwili hadi mitatu anaweza kuogopa kutengana na mzazi wake (separation anxiety), jambo ambalo ni la kawaida katika umri huo,” anasema Mtweve.

Hata hivyo, katika utafiti wangu mdogo nilioufanya, nimebaini kuwa mtoto wa miaka minne au mitano anaweza kuanza kuogopa giza,  au ndoto mbaya. Kadiri anavyokua zaidi, hasa kuanzia umri wa miaka saba na kuendelea, hofu inaweza kuhusishwa na masuala ya kijamii kama vile kuogopa kukosea darasani, kukejeliwa na wenzao au kushindwa kufikia matarajio ya wazazi.

Vyanzo vingine vya hofu ni pamoja na mabadiliko katika maisha ya mtoto, kama kuhama nyumba, kupata ndugu mpya, au wazazi kutengana.

Pia, watoto wanaweza kuiga hofu kutoka kwa watu wazima wanaowazunguka; kwa mfano, kama mzazi anaonyesha woga mkubwa kwa mbwa, wadudu na mambo kadha wa kadha, mtoto naye anaweza kujifunza kuogopa vitu hivyo.

Hata hivyo, katika kukabiliana na hili, mzazi unaweza kumsaidia mwanao kwa kumsikiliza na kuthibitisha hisia zake za hofu ni zipi.

Kisha unaweza kumuambia kwama asiogope, na awe mtulivu na ukazungumza naye juu ya hicho anachokiogopa. Hii humsaidia mtoto kuelewa kuwa hisia zake ni halali na anayo nafasi ya kuzieleza.

Pili, kuwapa watoto uelewa wa kinachowatisha ni hatua muhimu. Wakati mwingine hofu hutokana na kutokuelewa kitu. Kwa mfano, mtoto anaweza kuogopa radi akifikiri ni kitu kinachoweza kumdhuru. Mzazi anaweza kueleza kwa lugha rahisi kwamba radi ni mlio unaotokana na mvua na umeme wa anga, si kitu kinachoweza kumdhuru akiwa ndani ya nyumba salama.

Lakini pia mzazi unapaswa kumfundisha mbinu za kujituliza, hii ni njia bora ya kuwasaidia watoto kukabiliana na hofu.

 Mbinu kama kupumua kwa utaratibu, kuimba nyimbo wanazozipenda, au kufanya mazoezi madogo ya utulivu husaidia kupunguza wasiwasi.

Wataalamu wa saikolojia wanasema wazazi wanaweza kufanya mazoezi hayo sambamba na watoto wao wakilenga kuwafunza kwa vitendo.

Lakini tukumbuke kuwa watoto hujifunza kwa kuangalia. Mzazi anapokabiliana na hali ya woga kwa utulivu, mtoto naye hujifunza kufanya hivyo.

Ikiwa mtoto anaogopa kuingia darasani siku ya kwanza, mzazi anaweza kumsaidia kumuongoza hadi ndani, kumtambulisha kwa mwalimu, kwa wanafunzi wenzake kisha akaondoka akiwa anatabasamu, hapo utakuwa umempunguzia hofu na atajifunza kwamba kumbe pale alipo ni mahali salama na wale aliokutana nao ni watu wema.

Mazingira ya nyumbani yanapaswa kumhakikishia mtoto usalama wa kimwili na kihisia.

Mzazi anaweza kuhakikisha kuwa mtoto ana ratiba ya muda wa kulala unaoeleweka na mazungumzo ya familia yenye upendo. Utaratibu na uthabiti husaidia kupunguza wasiwasi kwa sababu mtoto anajua nini cha kutarajia.

Wakati mwingine, hofu au wasiwasi wa mtoto unaweza kuwa mkubwa kiasi cha kuathiri maisha yake ya kila siku. Dalili kama kukataa kwenda shule kwa muda mrefu, kulia kupita kiasi, ndoto mbaya za mara kwa mara, au kujitenga na wenzake zinaweza kuashiria wasiwasi unaohitaji msaada wa kitaalamu.

Wazazi hawapaswi kuogopa kumpeleka mtoto kwa mshauri wa saikolojia au mtaalamu wa watoto, kwani msaada wa mapema huleta matokeo mazuri zaidi.