Nangu apewa mchongo wa maana Simba

INGAWA jina la beki wa Simba, Willson Nangu halitajwi sana kama ilivyokuwa wakati anasajiliwa, kuna mastaa wa zamani wa Simba na Yanga walioona kitu kikubwa kwake na kumpa mbinu za kung’ara.

Katika nafasi ya beki wa kati anayocheza anashindania namba na Chamou Karaboue, Abdulrazack Hamza na Rushine De Reuck, jambo aliloshauriwa kupambana zaidi mazoezini ili kumshawishi kocha kumpanga.

Beki huyo mzawa, amefanikiwa kuanza katika kikosi kilichocheza mechi ya Ligi ya Mabingwa dhidi ya Nsingizini Hotspurs ugenini Eswatini akizima pale kati nyuma pamoja na Rushine ambaye ameng’ara tangu aliposajiliwa msimu huu. Nangimu baada ya kuanza kwa mara ya kwanza,  ameweka kambani bao la kichwa dakika ya mwisho kipindi cha kwanza akimalizia kona ya Neo Maema wakati Simba ikishinda 3-0.

Mshambuliaji wa zamani wa timu hiyo, Meddie Kagere amempa mbinu Nangu kuangalia ubora na upungufu wa washindani wake, kisha ajitafutie kitu cha kipekee kitakachomtambulisha.

NAN 01

 “Wakati najiunga na Simba nikitokea Gor Mahia ya Kenya, nilikutana na Emmanuel Okwi aliyekuwa mzuri wa kupatikana kila eneo na kupiga chenga, nikajua siyo mtu anayependa kukaa eneo moja la kufunga, nikaamua kutumia udhaifu huo ili kuhakikisha napata nafasi,” amesema Kagere aliyeandika rekodi ya kushinda tuzo ya mfungaji bora wa Ligi Kuu Bara kwa misimu miwili mfululizo (2018-2019, mabao 23) na (2019-2020, mabao 22).

Kagere amesema kitendo cha Simba kumsajili Nangu maana yake walitambua uwezo wake ambao anapaswa kuupambania na kuuonyesha kwa makocha ili apewe nafasi ya kumpanga.

Kwa upande wa beki wa zamani wa Simba, Yanga na Taifa Stars, Amir Maftah amemtaka Nangu kuwa mvumilivu na kuendelea kupambana ili kuja kuwa tunu ya Simba na taifa kwa baadaye.

NAN 02

“Nangu akivumilia, akipambana na kuwa mfano wa nidhamu nina uhakika Simba itakuja kujivunia kama ilivyo kwa Shomari Kapombe wanayemuona ndiye mkongwe wa timu,” amesema.

Staa wa zamani wa Yanga, William Mtendamema amesema: “Nangu aige mfano wa Ibrahim Bacca ambaye wakati anajiunga na Yanga hakuanza moja kwa moja kuaminiwa katika kikosi cha kwanza, ilimchukua takribani mwaka lakini kwa sasa ni panga pangua, akikosekana ana adhabu ama anaumwa.”