KIUNGO Pacome Zouzoua alijiunga na kikosi cha Yanga nchini Malawi na kucheza mechi ya hatua ya pili ya Ligi ya Mabingwa Afrika dhidi ya Silver Stricker leo Jumamosi Oktoba 18,2025 akitokea kuipambania Ivory Coast iliyofuzu Kombe la Dunia 2026, huku kocha Mfaransa akisema mtihani alionao staa huyo na Yanga ijipange.
Muivory Coast huyo amekuwa staa wa kwanza anayecheza Ligi Kuu Bara kulisaidia Taifa lake kukata tiketi ya kwenda kwenye Fainali za Kombe la Dunia 2026, baada ya nchi hiyo kuichapa Kenya 3-0.
Pacome ambaye mwanzoni mwa msimu huu aliongeza mkataba wa miaka miwili kuitumikia Yanga, alikuwa kwenye majukumu ya timu ya Taifa Ivory Coast ambayo imekwisha kufuzu michuano ya Kombe la Dunia zitakazochezwa Ma-rekani, Canada na Mexico Mwaka 2026.
Akizungumza na Mwanaspoti kocha wa zamani wa staa huyo, Julie Chevalier amesema, Pacome ni mchezaji anayependwa sana Ivory Coast, ndio maana imekuwa rahisi kuitwa timu ya taifa, lakini pia hata klabuni kwake ameendelea kufanya makubwa.
Alisema rekodi anazoendelea kuwa nazo zinazidi kuipaisha Yanga, lakini pia inaipa hatari zaidi kwani ofa zinaweza kuwa nyingi msimu huu au ujao kama ataendelea hivi.
“Kama ataendelea kufanya vizuri sitashangaa kumuona anakwenda Kombe la Dunia, lakini kwa sasa mtihani alionao ni kuhakikisha anaendelea kufanya vizuri klabuni kwake ili kocha azidi kumuamini na kumuita zaidi kwenye timu ya taifa.
“Kwa jinsi alivyo na bidii na kile alichokifanya miaka miwili iliyopita, ndicho kimempa fursa wakati huu kucheza timu ya Taifa, hivyo afanye muendelezo na zaidi,” amesema kocha huyo.
Mfaransa huyo amesema kuwa, kiwango cha Pacome kinatoa picha kubwa hasa kwa Yanga, kwani wakati wowote mambo yatakwenda kubadilika.
“Hatua anazopiga kiungo huyo hazina muda mrefu zitakuwa moto kwa klabu yake, kwani ataanza kupokea ofa kubwa kutoka Ulaya na Uarabuni.
“Wenzetu wamejaaliwa sana kugundua mchezaji mzuri yukoje, lakini hawaoni shida kutoa pesa ndefu, hivyo Yanga inaweza kuwa na mtihani wa kumzuia staa huyo,” amesema Chevalier.
Ivory Coast inaungana na mataifa mengine nane kutoka Afrika ambayo yamefuzu moja kwa moja Fainali za Kombe la Dunia 2026. Mataifa hayo mengine ni Misri, Cape Verde, Tunisia, Morocco, Algeria, Ghana, Afrika Kusini na Senegal, huku kukiwa na uwezekano ikaongezeka nyingine kupitia mechi za mtoano.
Fainali za Kombe la Dunia 2026 zitafanyika kwa uaandaaji wa mataifa matatu ambayo ni Marekani, Canada na Mexico zitakazoyahusisha majiji 16, zikitarajiwa kuanza Juni 11, 2025 na kumalizika Julai 19, 2025.
Kwa mara ya kwanza, Pacome alijumuishwa kwenye kikosi cha awali cha wachezaji 53 kilichoandaliwa kwa ajili ya AFCON 2023 lakini baadae jina lake likatolewa baada ya mchujo kufanyika.
Mara ya pili kiungo huyo kujumuishwa kwenye kikosi cha Ivory Coast ilikuwa mwaka 2024, timu hiyo ilialikwa kushiriki michezo miwili ya kirafiki dhidi ya Uruguay na Benin, Machi 2024, na kutokana na majeraha aliyokuwa nayo kipindi hicho, akashindwa kucheza. Ya tatu ni hii akicheza mechi mbili za kufuzu Kombe la Dunia, akimaliza dakika tisini Ivory Coast ilipoichapa Shelisheli 7-0, kisha akaingia kipindi cha pili kwenye ushindi wa 3-0 dhidi ya Kenya siku waliyofuzu.
Huu ukiwa ni msimu wa tatu Pacome anaitumikia Yanga baada ya kujiunga nayo Julai 2023 akitokea ASEC Mimosas ya kwao Ivory Coast, kiungo huyo amekuwa na rekodi nzuri ya mchango wa mabao kikosini hapo.
Msimu wa kwanza 2023-2024 kwenye Ligi Kuu Bara, Pacome alihusika na mabao 11, akifunga saba na asisti nne. Kisha 2024-2025, akahusika na mabao 22, akifunga 12 na asisti 10. Msimu huu, 2025-2026, bado hajafunga lakini ana asisti moja, huku akiwa tayari ameisaidia kubeba Ngao ya Jamii akifunga bao pekee katika ushindi wa 1-0 dhidi ya Simba.